Masters Dissertations
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Masters Dissertations by Subject "Bantu language"
Now showing 1 - 14 of 14
Results Per Page
Sort Options
Item Jinsi nyimbo zinavyomjenga mwanamke wa Kikagulu kimaadili(University of Dar es Salaam, 2013) Mageni, Martha DudleyLengo kuu la tasinifu hii ni kuchunguza jinsi nyimbo zinavyomjenga mwanamke wa Kikagulu kimaadili. Tasinifu hii ina sura sita ambapo sura ya kwanza ni utangulizi kwa ujumla, usuli wa tatizo, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti na mawanda ya utafiti. Sura ya pili ni mapitio ya maandiko yanayohusu nyimbo, maadili, uchanganuzi wa mfumo wa kijinsia uliochanganuliwa na wataalamu tofauti pamoja na nadharia ya Ufeministi iliyotumika katika utafiti huu. Sura ya tatu inaelezea mbinu na njia zilizotumika katika ukusanyaji wa data, vifaa vya utafiti pamoja na eneo la utafiti. Sura ya nne ni mkusanyiko wa mambo yanayomjenga mwanamke na mwanamume katika kabila la Wakagulu pamoja na kubainisha nafasi ya mwanamke kiuchumi, kisiasa na kijamii. Sura ya tano ni uchambuzi wa dhamira za nyimbo zinazoimbwa na wanawake pamoja na kuchunguza uhusiano wake na sifa za kimaadili zinazotakiwa kwa mwanamke wa Kikagulu. Sura ya sita ni muhtasari wa tasinifu nzima, matokeo ya utafiti, mapendekezo na mwisho ni hitimisho. Matokeo yanaonesha kuwa dhamira zilizojitokeza katika nyimbo zinamjenga mwanamke kimaadili ili aweze kuwa na sifa zinazokubalika katika jamii. Pia kuna uhusiano kati ya dhamira zilizojitokeza kwenye nyimbo na sifa zinazotakiwa kimaadili kwa mwanamke wa Kikagulu. Mwanamke hupewa mafunzo kupitia nyimbo, familia, jamii, unyago, methali, hadithi na ngoma. Nafasi ya mwanamke katika jamii imetokana na mafunzo anayopata kupitia nyimbo ambazo humfanya awe na maadili ingawa mafunzo mengine humfanya akandamizwe kijinsia. Hivyo, jamii haina budi kuendeleza mafunzo ambayo yanamjenga mwanamke kimaadili na kuyapiga vita mafunzo yanayomkandamiza ili aweze kupata fursa sawa katika jamii.Item Kirai kitenzi cha kibantu ulinganishi wa muundo wa kirai kitenzi cha Kiswahili na Kizigua(University of Dar es Salaam, 2014) Abdallah, NasibuUtafiti huu ulilenga kulinganisha muundo wa Kirai Kitenzi cha Kiswahili na Kirai Kitenzi cha Kizigua. Utafiti ulichunguza kufanana na kutofautiana kwa muundo wa virai vitenzi hivyo na vipashio mbalimbali vinavyoandamana nacho. Katika utafiti huu tumetumia hojaji, majadiliano, ushuhudiaji na ushiriki wa mazungumzo ya wazigua wazawa ili kupata data ambapo watoa taarifa 40 kutoka vijiji vya Misima, Kwachaga, Suwa, Chogo, Chogo-Makazi, Mdoe na Vibaoni walishirikishwa. Nadharia iliyotuongoza katika uchanganuzi wa data ni nadharia ya Sarufi Miundo Virai Jumuishi (SMVJ) iliyoanzishwa mwaka 1970 na Gerald Gazdar, inayotumika kuelezea sintaksia ya lugha. Nadharia hii inaachana na sarufi zilizozingatia ugeuzaji maumbo na sheria za muundo virai na badala yake inatumia kanuni ya utawala wa moja kwa moja na kanuni ya utangulizani katika kuchunguza muundo wa kirai kitenzi cha Kizigua ili kuonesha uhusiano wa kiwima na kiulalo uliopo baina ya kitenzi na vipashio vinavyoandamana nacho. Matokeo yamebaini miundo 17 ya kirai kitenzi cha Kizigua, ambapo ipo miundo ambayo kitenzi huweza kusimama peke yake bila kufuatiwa na kipashio chochote. Ipo pia miundo ambayo kitenzi chake kinaweza kufuatiwa na vipashio mbalimbali. Matokeo pia yanaonesha kuwa vipo vipashio vya aina mbalimbali vinavyoweza kuandamana na kitenzi cha Kizigua. Vipashio hivyo ni pamoja na kikundi nomino, kikundi kielezi, kikundi kihusishi, kitenzi kisaidizi, kishazi tegemezi na hata sentensi. Pia, matokeo yanaonesha kuwa kuna kufanana na kutofautiana baina ya miundo ya kirai kitenzi cha Kizigua na ile ya kirai kitenzi cha Kiswahili, ambapo miundo 14 kati 17 ya Kirai Kitenzi cha Kizigua ambayo ni sawa na 82.4% inafanana na miundo ya kirai kitenzi cha Kiswahili na miundo mitatu kati ya 17 ya KTZ ambayo ni 17.6% inatofautiana na ile ya Kiswahili. Tumebaini pia kuwa karibu kila kitenzi cha Kizigua kinaweza kuwa na dhima ya uelekezi, yaani kinaweza kuwa kitenzi elekezi au si elekezi. Hii ina maana kwamba si lazima kwa kitenzi cha Kizigua na hata cha Kiswahili kiwe na uyambwa, yaani kuwa na uwezo wa kuchukua nomino, bali kinaweza kuchukua vipashio vingine visivyokuwa yambwa kama vile kikundi kielezi na kikundi kihusishi.Item Maana na misingi ya uteuzi wa majina ya watu katika lugha ya kiha(Unversity of Dar es Salaam, 2014) Jonas, LeotheliaUtafiti huu umechunguza Maana na Misingi ya Uteuzi wa Majina ya watu katika lugha ya Kiha. Utafiti ulilenga kubainisha na kujua maana, dhima na sababu zinazochochea utoaji wa majina ya watu. Utafiti umefanyika katika kata za Muhinda na Mwayaya, wilaya ya Buhigwe mkoa wa Kigoma, Tanzania. Ili kufanikisha kazi hii, Nadharia ya Ufungamanishi ya Hallowell (1955) ilitumika kuongoza utafiti huu. Nadharia hii hueleza kwamba kuna mfungamano kati ya wanadamu na mazingira ambapo binadamu hudumisha na kuendelea kujitambua kwa njia ya kujikumbusha uzoefu wa nyuma. Utafiti ulihusisha sampuli ya watafitiwa 90 ambapo usampulishaji nasibu tabakishi ulitumika kwa kutumia kigezo cha umri. Data za utafiti zilikusanywa kwa kutumia mbinu za hojaji, mahojiano na hifadhi ya maandishi na kisha kuchanganuliwa kwa kutumia mkabala wa kimaelezo. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kuwa majina ya watu katika jamii ya Waha hudokeza maana mbalimbali kama vile tabia, matukio, mahusiano, uzazi au ugumba, matatizo, kushukuru na kueleza nyakati au majira. Vilevile ni nyenzo muhimu ya kutunza kumbukumbu na kueleza historia na uchumi wa jamii. Vilevile utafiti umebaini sababu mbalimbali zinazochochea utoaji wa majina ya watu katika jamii ya Waha kuwa ni mila na desturi, sifa au tabia za mtoto au mtu, imani kwa wahenga na mizimu, imani kwa Mungu, maumbile na muonekano, masaibu mbalimbali, hali ya ujauzito na matatizo ya uzazi yaliyotangulia, mfuatano katika kuzaliwa, muda na kipindi ambacho mtoto alizaliwa, pamoja na kuendeleza ukoo. Hivyo majina ya watu hutumika kama njia ya ya kueleza utamaduni, maisha, mahusiano na kutunza kumbukumbu za jamii husika. Kulingana na umuhimu huo, kuna haja ya kufanya tafiti juu ya lugha na mazingira kwani vijana wengi wameathiriwa na utandawazi, huku suala la utamaduni wao likiachwa. Ingefaa kutumia hazina ndogo ya wazee iliyobaki ili kuhifadhi tamaduni zetu hususani jamii ya WahaItem Matumizi ya Taswira katika nyimbo za Kisazi za jamii ya Wazigua kutoka Somalia(University of Dar es salaam, 2011) Kussaka, Mariam BakariLengo la utafiti huu ni kuchunguza vipengele vya fasihi simulizi vinavyosaidia kutoa ujumbe katika jamii. Utafiti huu umefanya uchambuzi wa nyimbo kumi za kisazi za jamii ya Wazigua kutoka Somalia na kubainisha aina za taswira zinazopatikana katika nyimbo hizo. Zaidi ya hayo, utafiti umejadili jinsi matumizi ya taswira hizo yanavyofikisha ujumbe kwa walengwa. Nyimbo hizo zimechambuliwa ili kuweza kubainisha umuhimu wa taswira hizo katika kutoa ujumbe kwenye kumuandaa binti katika maisha yake ya utu uzima. Aidha, kwa kutumia nadharia ya Semiotiki, tasnifu hii imejenga hoja zilizoongoza utafiti huu kwamba taswira zina matumizi makubwa katika kutoa mafunzo kwa wari. Matokeo ya utafiti yamedhihiriswa kuwa taswira za kuonekana ndizo hutumika kwa wingi katika nyimbo za Kisazi ya wazigua kutoka Somalia na kwamba taswira hizi husaidia kufikisha ujumbe kwa walengwa kwa haraka.Item Maumbo na dhima ya uradidi wa vitenzi vya lugha ya chindali(University of Dar es Salaam, 2014) Mshani, EdwardUtafiti huu unahusu maumbo na dhima ya uradidi wa vitenzi katika lugha ya Chindali inayozungumzwa nyanda za juu, kusini mwa Tanzania katika wilaya za Ileje, Mbozi, Kyela, Rungwe, Mbeya Vijijini, Mbeya Mjini na Mbarali. Jumla ya kata 3 za Isongole, Malangali na Kafule zilihusika. Utafiti huu ulichunguza maumbo na dhima ya uradidi wa vitenzi vya lugha ya Chindali, aina za uradidi, muundo wa maumbo ya uradidi wa vitenzi vya lugha ya Chindali, mazingira ya utokeaji wa uradidi na dhima zake zilichunguzwa na kufafanuliwa. Vitenzi vya aina tatu vilichaguliwa ambavyo ni vitenzi visoukomo, vitenzi vya silabi moja na vitenzi nyambulishi ambapo tuliangalia vitenzi hivyo vinavyonyambuliwa katika kauli za vitenzi. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Utangamani (uelekeani) ili kujibu maswali ya utafiti huu ambayo yalikuwa ni: Mosi, kuna aina ngapi za uradidi kwa ujumla katika lugha ya Chindali? Pili, muundo wa maumbo ya uradidi wa vitenzi vya lugha ya Chindali ni upi? Tatu, uradidi wa vitenzi katika lugha ya Chindali una dhima zipi? Utafiti huu umebaini kuwa kuna aina mbili za uradidi katika Chindali; (i), uradidi kamili ambao unahusu urudiaji wa shina au neno lote; (ii), uradidi nusu ambao ni urudiaji wa sehemu tu ya neno au shina na umeonekana katika vitenzi vinavyoonesha njeo pamoja na vitenzi visoukomo vinavyoandamana na kiambishi kisoukomo na aina nyingine za viambishi awali vinavyojitokeza kabla ya mzizi wa kitenzi. Uradidi nusu katika Chindali unahusu unakili wa mzizi wa kitenzi na viambishi tamati. Mazingira ya utokeaji wa uradidi yalichunguzwa na kubaini kuwa viradidiwa katika lugha ya Chindali hutokea kabla au baada ya mzizi au shina la kitenzi kwa kunakili kuanzia upande wa kushoto kuelekea upande wa kulia wa shina au mzizi wa kitenzi. Aidha, dhima mbalimbali zimebainika kama vile kusisitiza jambo, kujirudia kwa jambo, udhoofishaji wa maana, hali ya mazoea na dhima ya kuendelea kwa jambo. Tafiti zingine zinaweza kufanywa juu ya uradidi katika aina zingine za maneno katika lugha ya Chindali. Aidha, kuna haja ya kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya isimu kama vile mofolojia, fonolojia, semantiki na sintaksia katika lugha ya Chindali.Item Mfuatano wa mofimu ambatizi katika kitenzi cha Kiluguru(University of Dar es Salaam, 2016) Elias, LusticaUtafiti huu umechunguza mfuatano wa mofimu ambatizi katika kitenzi cha Kiluguru. Malengo ya utafiti huu ni pamoja na kubaini aina za mofimu ambatizi na dhima zake katika kitenzi cha Kiluguru, kufafanua mfuatano wa mofimu hizo na kueleza kanuni zinazojitokeza wakati wa uambatizi. Sababu ya kuchunguza kipengele hiki ni kutoa mchango wa uelewa wetu wa suala la uambatizi katika lugha za jamii ya kibantu ikiwemo lugha ya Kiluguru. Uambatizi ni dhana inayojitokeza sana katika lugha za kibantu lakini udadavuzi wake huwa na changamoto za pekee katika lugha husika. Kuna kuachana na kutofautiana kwingi katika taratibu za uchambuzi. Na katika lugha hii ya Kiluguru suala hili halijafanyiwa utafiti wa kutosha. Ili kufikia malengo hayo, ilikusanywa data ya utafiti toka uwandani ambako vitenzi mbalimbali vyenye ukomo viliteuliwa na kuchambuliwa. Ukusanyaji wa data ulifanyika katika vijiji viwili, yaani Nyandira katika wilaya ya Mvomero na Kibangile katika wilaya ya Morogoro vijijini, mkoani Morogoro, Tanzania. Taarifa zilikusanywa kwa njia ya mahojiano na ushuhudiaji. Mahojihano yalitumika sambamba na dodoso. Aidha utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Mofolojia Leksika ya Kiparsky (1982) ambayo msingi wake unadai kuwa maneno yanaundwa na vipande vidogo vidogo ambavyo hupangwa katika ngazi na kuonesha uhusiano wa kanuni zinazojenga maumbo ya kimofolojia na kanuni zinazodhibiti namna maumbo haya yanavyotamkwa. Matokeo ya utafiti yameonesha uwepo wa mofimu nyingi ambatizi katika Kiluguru kama vile mofimu za nafsi, njeo, ukanushi, yambwa, urejeshi na hali. Imebainika pia kuwa mifuatano kubalifu ya mofimu ambatizi katika vitenzi vya Kiluguru si huru bali hutawaliwa na kanuni mahususi; imebainika pia kuwa mifuatano hiyo kisintakisia huukilia dhima tofauti tofauti za mofimu husika. Pia utafiti umebaini kuwepo kwa kanuni mbalimbali zinazojitokeza wakati wa uambatizi kama vile kanuni ya udondoshaji wa irabu, uyeyushaji, usimilishaji wa nazali na muungano au mvutano wa irabu.Item Mfuatano wa mofimu nyambulishi katika vitenzi vya Kikinga(University of Dar es Salaam, 2011) Gawasike, ArnoldSuala la unyambulishaji na mfuatano wa mofimu nyambulishi limewavuta wataalamu wengi. Hata hivyo, hakuna utafiti ambao umefanyika katika lugha ya Kikinga. Kwa hiyo utafiti huu ulikuwa jaribio la kuchunguza unyambulishaji wa vitenzi katika lugha hii na kubainisha kanuni za mfuatano wa mofimu nyambulishi hizo. Aidha, utafiti umechunguza unyambulishi wa aina tano. Utafiti umefanyika katika kata za: Mbalatse, Ipepo na Ukwama, wilaya ya Makete mkoa wa Iringa, Tanzania. Ili kufanikisha kazi hii, Kanuni Tazamishi (KAT) iliongoza utafiti huu, yaani unyambulishaji wa vitenzi kimofolojia unaakisi unyambulishaji wa vitenzi kisintaksia. Mbinu za utafiti zilihusu: usampulishaji, ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Data ya utafiti ni ya kutoka uwandani ambapo vitenzi viliteuliwa na kuwekwa katika kategoria mbili; vitenzi visoukomo katika kundi moja na vitenzi vya silabi moja katika kundi jingine. Kazi imegawanyika katika sura tano. Sura ya kwanza, imeeleza kiini cha utafiti na utaratibu uliozingatiwa katika kufanikisha utafiti. Sura ya pili, imeshughulikia mapitio ya maandiko kuhusiana na unyambulishaji na mfuatano wa mofimu katika lugha. Mapitio haya yamebainisha kuwa minyambuliko na mifuatano ya mofimu katika lugha ipo. Sura ya tatu, imehusu mbinu za utafiti ambapo populesheni, sampuli, usampulishaji pamoja na njia tatu za ukusanyaji data zilibainishwa. Sura ya nne, imeshughulikia uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Kwa ujumla data, iliyopatikana imechanganuliwa kwa njia ya maelezo na kanuni. Kanuni Tazamishi ya Baker (1985) ndiyo iliyoongozo mjadala na uchanganuzi wa data hii. Sura ya tano imeshughulikia matokeo, hitimisho, na tafiti fuatishi. Matokeo ya utafiti yamebainisha minyambuliko mitano na kwamba, lugha ya Kikinga inapangilia mofimu nyambulishi zake kwa mujibu wa Kanuni Tazamishi inayodai unyambulishaji kimofolojia huakisi unyambulishaji sintaksia. Aidha, kanuni ya uukiliwaji iliyoundwa ina tenda kazi pia, katika mfuatano wa mofimu nyambulishi katika lugha ya Kikinga, yaani mofimu moja ikitangulia ina kawaida ya kuukilia mofimu ambazo zinaweza kuifuata na ama kutoifuata yenyewe.Item Mfumo wa njeo na hali katika lugha ya Ki-bena.(University of Dar es Salaam, 2011) Sehelele, MagdalenaUtafiti huu unahusu mfumo wa njeo na hali katika lugha ya Ki-bena. Ingawa kuna tafiti zilizofanywa na Nurse (1979) na Priebusch (1935) kuhusu mfumo wa njeo na hali katika lugha hii, bado tafiti hizi zilikuwa za kiwango cha arabi na hivyo hazikufafanua kwa kina mfumo wa njeo na hali wa lugha ya Ki-bena. Utafiti huu ulilenga kuchunguza mfumo wa njeo na hali katika lugha ya Ki-bena hasa lahaja ya Ki-Lupembe kwa kuangalia ni vipengele vipi vya kimofolojia hubainisha njeo na hali. Pia, utafiti ulilenga kuchunguza mchango wa vielezi vya wakati na hali katika kubainisha muda na hali mahususi ya tukio katika sentensi yakinishi za Ki-bena. lli kutimiza malengo ya utafiti huu nadharia ya Ulalo iliyoasisiwa na Reichenbach (1947) ndiyo iliyotumika kuchambua data za ulafiti nadharia hii imefaa kutumiwa katika kuelezea mfumo wa njeo na hali katika lugha ya Ki-bena baada ya kufanyiwa marekebisho na wataalamu kama, Johnson (1977), Smith (1978) na Besha (1985). Data zilizotumiwa katika utafiti huu zilikusanywa kutoka katika vijiji vitatu vilivyopo katika tarafa ya Lupembe wilayani Njombe. Vijiji hivyo ni Kanikelele, Soliwaya na Lupembe Data za utafiti zilikusanywa kwa njia ya, mahojiano, dodoso na uchambuzi matini. Utafiti huu umebainisha kuwa katika lugha ya Ki-bena kuna mofimu sita (6) za njeo ambaza hujitokeza kabla ya mzizi wa kitenzi.Vile vile kuna mofimu nne (4) za hali ambapo mofimu tatu (3) hujitokeza baada ya mzizi wa kitenzi na mofimu moja (1) ambayo ni ya hali endelevu hujitokeza kabla ya mzizi wa kitenzi Utafiti huu pia umebainisha kuwa mofimu za njeo na hali hutumiwa pamoja na vielezi vya wakati na hali ili kubainisha muda na hali mahususi ya tukio.Item Muundo wa kirai nomino cha Kibena.(University of Dar es Salaam, 2011) Mbogela, EnockTasinifu hii ni matokeo ya utafiti ulioshughulikia Muundo wa Kirai Nomino cha Kibena, na imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza imeshughulikia Tatizo la Utafiti na Kiunzi cha Nadharia kilichotumika katika utafiti huu. Sura ya pili imeangazia mapitio mbalimbali ya maandiko yaliyoibua utaflti huu. Sura ya tatu imetalii mbinu anuuai zilizotumika kucndcsha utafiti huu. Sura ya nne imejihusisha na uchanganuzi data ulioibua mchango mpya wa utaflti huu ambapo suu ya mwisho imehitimisha kwa kutoa muhtasari wa tasinifu nzima. Matokeo ya Utafiti huu yanaonyesha kuwa Muundo wa Kirai nomino cha Kibena kwa upande. mmoja una sifa zinazofanana na zile za virai nomino vya lugha nyingine za Kibantu kikiwemo Kiswahili. Miongoni mwa sofa hizo ni pamoja na viandami vinavyounda KN hiya ambavyo ni vibainishi (vimilikishi na vionyeshi) na vikumushi (vivumishi vya sifa na idadi, virai husishi na vishazi rejeshi). Vile vile viandami vingi katika mpangilio wa KN hiyo hutokea kulia kwa neno kuu (nomino). Katika mkururo wa viandami hivyo, kibainishi kimilikishi huliandamia neno kuu, kisha vijenzi vingine hufuata. Si hivyo tu bali pia uamilifu wa KN ya Kibena katika sentensi ni ule unaojibainisha katika lugha nyingine, ukiwa ni kiima cha sentensi, yambwa ya kitenzi, yambiwa, kijalizo cha kihusishi na kikumushi cha kirai nomino, mpangilio wa vijenzi wake, unaoruhusu utokeaji wa kionyeshi kabla ya nomino na hivyo kuwa na mpangilio wa: (B) + N + (B) (KV) (F) (S). Katika KN ya Kibena kuna kiandami de kinachokumusha nomino, kivumishi au kibainishi kionyeshi. lli kufanya hivyo kiandami hiki kinatalii katika maeneo mbalimbali ya kirai hicho. KN ya Kibena pia inaruhusu kutumia ama kutotumia kiambishi awali tangulizi (augment). Kuhusu suala la ubebaji viandami, utafiti umebaini kwamba KN ya Kibena inakubali kuturnia kijenzi kimoja hadi vitano katika mazugumzo ya kawaida. Miundo ya kiuchamko (yenye viandami vingi) inaonekana kuwa ni ya kinadharia tu. Hivyo haitumiki kiuhalisia. Kwa jumla KN ya Kibena ina viandami vinavyofuata na visivyofuata ruwaza maalum zilizobainishwa k"'a kind katika kali hii.Item Ruwaza za uradidi wa vitenzi katika lugha ya Shisafwa(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2012) Mwashota, PendoUtafiti huu unahusu ruwaza za uradidi wa vitenzi katika lugha ya Shisafwa inayozungumzwa katika nyanda za juu Kusini mwa Tanzania katika wilaya za Mbeya Vijijini, Mbeya Mjini na Chunya. Jumla ya kata tatu za Inyala, Tembela na Ulenje zilihusika. Utafiti huu ulichunguza ruwaza za uradidi wa vitenzi katika lugha ya Shisafwa ambapo aina za uradidi na ruwaza zake, mazingira ya utokeaji wa uradidi na dhima zake mbalimbali zilichunguzwa. Vitenzi vya namna tatu viliteuliwa: vitenzi visoukomo, vitenzi vya silabi moja na vitenzi nyambulishi. Kwa kuongozwa na Nadharia ya Uelekeani, utafiti huu ulikusudia kujibu maswali yafuatayo; kwanza, je, kuna aina ngapi za uradidi na ruwaza zake ni zipi? Pili, ni mazingira gani ambamo huukilia utokeaji wa uradidi katika lugha ya Shisafwa? Tatu, je, uradidi una dhima gani katika lugha ya Shisafwa? Utafiti huu uligawanyika katika sura tano, ambapo sura ya kwanza imeeleza taarifa za awali ikijumuisha eneo la utafiti, usuli wa utafiti, mfumo sauti wa lugha ya Shisafwa na historia ya Wasafwa. Aidha, tamko la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti, na mawanda ya utafiti vilishughulikiwa katika sura hii. Sura ya pili ilihusu mapitio ya maandiko mbalimbali kuhusiana na uradidi wa vitenzi katika lugha za Kibantu na mwega wa kinadharia ulioongoza utafiti huu. Sura ya tatu ilihusu mbinu za utafiti zilizotumika katika mchakato wa kukusanya data. Hojaji, ushuhudiaji na usaili ni mbinu ambazo zilitumika kukusanyia data za utafiti huu. Aidha, sampuli ya watafitiwa 30, ambao ni wazungumzaji wazawa wa lugha ya Shisafwa ndio waliotumika katika utafiti huu. Sura ya nne ilihusu uchambuzi na uwasilishaji wa data kuhusu ruwaza za uradidi wa vitenzi katika lugha ya Shisafwa ambapo aina za uradidi wa vitenzi na ruwaza zake mbalimbali zilifafanuliwa. Pia, mazingira ya utokeaji wa uradidi pamoja na dhima zake zimechambuliwa katika sura hii. Sura ya tano ilihusu matokeo ya utafiti, hitimisho na mapendekezo.Item Suala la uzazi katika ontolojia ya Kibantu na jinsi lilivyojitokeza katika riwaya za kiswahili(Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2012) Kajosi, SofiaUtafiti huu ulilenga kuchambua suala la uzazi katika ontolojia ya Kibantu kama lilivyosawiriwa kwenye riwaya za Kiswahili. Utafiti ulijikita katika hoja ya kwamba suala la uzazi ni miongoni mwa maudhui nyeti ya ustaarabu wa Kibantu uliosawiriwa kwenye riwaya za Kiswahili ingawa wahakiki hawajalipa nafasi yake stahiki katika kazi zao, ama kwa kulifumbia macho kabisa au kwa kulipa nafasi ndogo sana kinyume na unyeti wake. Hivyo, kazi hii imevibainisha na kuvijadili vipengele mbalimbali vya utamaduni wa Kibantu juu ya dhana ya uzazi. Data zilizotumika katika kazi hii zimekusanywa kupitia vitabu vilivyoteuliwa na vya ziada katika riwaya za Kiswahili. Uchambuzi wa data umeongozwa na Kiunzi cha nadharia ya Ontolojia ya Kibantu na kutumia mkabala wa kidhamira. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa suala la uzazi katika ontolojia ya Kibantu lina mitazamo mikuu mitatu. Mtazamo wa kwanza, unaonyesha kuwa uzazi ni baraka na ugumba ni laana. Mtazamo wa pili ni imani kuwa uzazi ndio mhimili au nguzo ya ndoa. Na mtazamo wa tatu ni imani kuwa uzazi ndio nguzo ya ujenzi wa ukoo. Utafiti huu unaonyesha kuwa imani ya Wabantu kuhusu uzazi imejikita katika mitazamo hiyo mitatu. Hata hivyo, mtazamo mama ulioonekana kujitokeza kwa kiasi kikubwa katika riwaya takribani zote ni ule wa kuwa uzazi ni baraka na ugumba ni laana. Zaidi ya utafiti huu, hitajio bado lipo kwa tafiti nyingine kufanywa katika eneo hili kwa kuchunguza mambo kadha wa kadha katika upande huu wa ontolojia ya Kibantu. Kwa mfano, dhana ya familia pana, dhana ya ujaala, dhana ya wakati, na hadhi ya mwanamke na mwanamume katika ontolojia ya Kibantu.Item Utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha ya kisubi(University of Dar es salaam, 2020) Jasson, TasianaUtafiti huu umechunguza utokeaji wa kimbishi tangulizi katika lugha ya Kiswahili. Lengo lilikuwa ni kuweka bayana maumbo na mazingira ya utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha hiyo. Data ya utafiti huu ulikusanywa uwandani katika eneo la kata ya Nyaruhungo iliyopo wilayani Biharamuro, Mkoani Kagera. Mbinu ya hojaji na majadiliano ya vikundi lengwa zilitumika kukusanya data ya utafiti huu ulichambuliwa kwa mkabala wa kitaamuli ambapo mbinu ya uchambuzi wa data kimaudhui ilitumika.Nadharia ya Utangamano wa mfuatano wa mofimu ya McCalthy na princes (1995) imetumika katika uchanganuzi wa data. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa kiambishi tangulizi katika lugha tya kisubi kina maumbo sahili, yaani; maumbo ya irabu pekee. Maumbo hayo ni [a,e, i,o]. Aidha imebadilika kuwa maumbo hayo hutokea katika mazingira maluum ambayo ni bainifu. Mazingira hayo ni ya kategolia bainifu za maneno ya lugha hiyo zikiwa pwekepweke. Kulingana na utafiti huu kategolia hizo ni nomino, kivumishi, kielezi na kibainishi.Hata hivyo, kuna vighairi vichache vya kategolia hizo visivyokuwa na kiambishi tangulizi, hususan vivumishi viulizi na nomino zinazotaja majina ya ndugu kama vile maha (mama), kaaka (bibi) guuku (babu). Aidha ,imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliopo kwenye kiima au kiarifu cha tungo hatakama tungo hiyo ina ukanushi , taarifa au masharti. Pia, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika kielezi kinapoandamana na kitenzi katika tungo.Kadhalika,imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kabla ya kibainishi kioneshi. Zaidi ya hayo, imebainilka kuwa kiambishi tangulizi hakitokei katika nomino iliyopo baadaya kibainishi kioneshi. Vilevile, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea kwenye kivumishi cha pekee kinachotanguliwa na nomino. Pia, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyotanguliwa na kihusishi nomino ya uhusika milikishi na nomino iliotanguliwa na kiunganishi huru.Utokeaji huo hutokana na michakato udondoshaji, uunganishaji ua urefushaji wa irabu ya kihusishi, irabu ya kimilikishi au kiunganishi huru kilichotangulia nomino husika. Kwa hiyo, utafiti huu umebaini kuwa bazingira ya kimofolojia na kisintaksia ndiyo huamua kutokea au kutokutokea kwa kiambishi tangulizi katika lugha ya kisubi .Aidha utafiti huu umependekeza utafiti mwingine ufanyike katika kipengele cha ulinganishi wa ruwaza za utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha mbalimbali za kibantu au zisizo za kibantu.Item Utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha ya kisubi(University of Dar es Salaam, 2020) Jasson, TasianaUtafiti huu umechunguza utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha ya Kisubi Lengo lilikuwa kuweka bayana maumbo na mazingira ya utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha hiyo. Data ya utafiti huu ilikusanywa uwandani katika eneo la Kata ya Nyarubungo iliyopo Wilayani Biharamulo, Mkoani Kagera. Mbinu ya hojaji na majadiliano ya vikundi lengwa zilitumika kukusanya data ya utafiti huu. Aidha, data ya utafiti huu ilichambuliwa kwa mkabala wa kitaamuli ambapo mbinu ya uchambuzi wa data kimaudhui ilitumika. Nadharia ya Utangamano wa Mfuatano wa Mofimu ya McCarthy na Prince (1995) imetumika katika uchanganuzi wa data. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kiambishitangulizi katika lugha ya Kisubi kina maumbo sahili, yaani; maumbo ya irabu pekee. Maumbo hayo ni [a, e, i, o]. aidha, imebainika kuwa maumbo hayo hutokea katika mazingira maalumu ambayo ni bainifu. Mazingira hayo ni ya kategoria hizo ni nomino, kivumishi, kielezi na kibainishi. Hata hivyo, kuna vighairi vichache vya kategoria hizo visivyokuwa na kiambishi tangulizi, hususan vivumishi viulizi na nomino zinazotaja majina ya ndugu kama vile maha (mama), kaaka (bibi) na guuku (babu). Aidha, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kwenye kiima au kiarifu cha tungo hata kama tungo hiyo ina ukanushi, taarifa au ,asharti. Pia, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika kielezi kinapoandamana nakitenzi katika tungo. Kadhalika, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kabla ya kibainishi kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kabla ya kibainishi kioneshi. Zaidi ya hayo, imenainika kuwa kiambishi tangulizi hakitokei katika nomino iliyopo baada ya kibainishi kioneshi. Vilevile, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea kwenye kivumishi cha pekee kinachotanguliwa na nomino. Pia, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyotanguliwa na kihusishi, nomino ya uhusika milikishi na nomino iliyotanguliwa na kiunganiishi huru. Utokeaji huu hutokana na michakato ya udondoshaji, uunganishaji na urefushaji wa irabu ya kihusishi, irabu ya kimilikishi au kiunganishi huru kilichotangulia nomino husika. Kwa hiyo, utafiti huu umebaini kuwa mazingira ya kimofolojia na kisintaksia ndiyo huamua kutokea au kutokutokea kwa kiambishi tangulizi katika lugha ya Kisubi. Aidha, utafiti huu umependekeza utafiti mwingine ufanyike katika kipengele cha ulinganishi wa ruwaza za utokeaji wa kiambiishi tangulizi katika lugha mbalimbali za Kibantu au zisizo za Kibantu.Item Utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha ya kisubi(University of Dar es salaam, 2020) Jasson, TasianaUtafiti huu umechunguza utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha ya Kisubi. Lengo lilikuwa ni kuweka bayana maumbo na mazingira ya utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha hiyo. Data ya utafiti huu ilikusanywa uwandani katika eneo la Kata ya Nyarubungo iliyopo Wilayani Biharamulo, Mkoani Kagera. Mbinu ya hojaji na majadiliano ya vikundi lengwa zilitumika kukusanya data ya utafiti huu. Aidha, data ya utafiti huu ilichambuliwa kwa mkabala wa kitaamuli ambapo mbinu ya uchambuzi wa data kimaudhui ilitumika. Nadharia ya Utangamano wa Mfuatano wa Mofimu ya McCarthy na Prince (1995) imetumika katika uchanganuzi wa data. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kiambishi tangulizi katika lugha ya Kisubi kina maumbo sahili, yaani; maumbo ya irabu pekee. Maumbo hayo ni [a, e, i, o]. Aidha, imebainika kuwa maumbo hayo hutokea katika mazingira maalumu ambayo ni bainifu. Mazingira hayo ni ya kategoria bainifu za maneno ya lugha hiyo zikiwa pwekepweke. Kulingana na utafiti huu, kategoria hizo ni nomino, kivumishi, kielezi na kibainishi. Hata hivyo, kuna vighairi vichache vya kategoria hizo visivyokuwa na kiambishi tangulizi, hususan vivumishi viulizi na nomino zinazotaja majina ya ndugu kama vile maha (mama), kaaka (bibi) na guuku (babu). Aidha, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kwenye kiima au kiarifu cha tungo hata kama tungo hiyo ina ukanushi, taarifa au masharti. Pia, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika kielezi kinapoandamana na kitenzi katika tungo. Kadhalika, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyopo kabla ya kibainishi kioneshi. Zaidi ya hayo, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hakitokei katika nomino iliyopo baada ya kibainishi kioneshi. Vilevile, utafiti huu umebaini kuwa kiambishi tangulizi hutokea kwenye kivumishi cha pekee kinachotanguliwa na nomino. Pia, imebainika kuwa kiambishi tangulizi hutokea katika nomino iliyotanguliwa na kihusishi, nomino ya uhusika milikishi na nomino iliyotanguliwa na kiunganishi huru. Utokeaji huo hutokana na michakato ya udondoshaji, uunganishaji na urefushaji wa irabu ya kihusishi, irabu ya kimilikishi au kiunganishi huru kilichotangulia nomino husika. Kwa hiyo, utafiti huu umebaini kuwa mazingira ya kimofolojia na kisintaksia ndiyo huamua kutokea au kutokutokea kwa kiambishi tangulizi katika lugha ya Kisubi. Aidha, utafiti huu umependekeza utafiti mwingine ufanyike katika kipengele cha ulinganishi wa ruwaza za utokeaji wa kiambishi tangulizi katika lugha mbalimbali za Kibantu au zisizo za Kibantu.