Mfuatano wa mofimu ambatizi katika kitenzi cha Kiluguru
Loading...
Date
2016
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu umechunguza mfuatano wa mofimu ambatizi katika kitenzi cha Kiluguru. Malengo ya utafiti huu ni pamoja na kubaini aina za mofimu ambatizi na dhima zake katika kitenzi cha Kiluguru, kufafanua mfuatano wa mofimu hizo na kueleza kanuni zinazojitokeza wakati wa uambatizi. Sababu ya kuchunguza kipengele hiki ni kutoa mchango wa uelewa wetu wa suala la uambatizi katika lugha za jamii ya kibantu ikiwemo lugha ya Kiluguru. Uambatizi ni dhana inayojitokeza sana katika lugha za kibantu lakini udadavuzi wake huwa na changamoto za pekee katika lugha husika. Kuna kuachana na kutofautiana kwingi katika taratibu za uchambuzi. Na katika lugha hii ya Kiluguru suala hili halijafanyiwa utafiti wa kutosha. Ili kufikia malengo hayo, ilikusanywa data ya utafiti toka uwandani ambako vitenzi mbalimbali vyenye ukomo viliteuliwa na kuchambuliwa. Ukusanyaji wa data ulifanyika katika vijiji viwili, yaani Nyandira katika wilaya ya Mvomero na Kibangile katika wilaya ya Morogoro vijijini, mkoani Morogoro, Tanzania. Taarifa zilikusanywa kwa njia ya mahojiano na ushuhudiaji. Mahojihano yalitumika sambamba na dodoso. Aidha utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Mofolojia Leksika ya Kiparsky (1982) ambayo msingi wake unadai kuwa maneno yanaundwa na vipande vidogo vidogo ambavyo hupangwa katika ngazi na kuonesha uhusiano wa kanuni zinazojenga maumbo ya kimofolojia na kanuni zinazodhibiti namna maumbo haya yanavyotamkwa. Matokeo ya utafiti yameonesha uwepo wa mofimu nyingi ambatizi katika Kiluguru kama vile mofimu za nafsi, njeo, ukanushi, yambwa, urejeshi na hali. Imebainika pia kuwa mifuatano kubalifu ya mofimu ambatizi katika vitenzi vya Kiluguru si huru bali hutawaliwa na kanuni mahususi; imebainika pia kuwa mifuatano hiyo kisintakisia huukilia dhima tofauti tofauti za mofimu husika. Pia utafiti umebaini kuwepo kwa kanuni mbalimbali zinazojitokeza wakati wa uambatizi kama vile kanuni ya udondoshaji wa irabu, uyeyushaji, usimilishaji wa nazali na muungano au mvutano wa irabu.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8025.1.E44)
Keywords
Luguru language, Bantu language, Morphology
Citation
Elias, L. (2016) Mfuatano wa mofimu ambatizi katika kitenzi cha Kiluguru, Tasnifu ya uzamili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam