Mfuatano wa mofimu nyambulishi katika vitenzi vya Kikinga
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Suala la unyambulishaji na mfuatano wa mofimu nyambulishi limewavuta wataalamu wengi. Hata hivyo, hakuna utafiti ambao umefanyika katika lugha ya Kikinga. Kwa hiyo utafiti huu ulikuwa jaribio la kuchunguza unyambulishaji wa vitenzi katika lugha hii na kubainisha kanuni za mfuatano wa mofimu nyambulishi hizo. Aidha, utafiti umechunguza unyambulishi wa aina tano. Utafiti umefanyika katika kata za: Mbalatse, Ipepo na Ukwama, wilaya ya Makete mkoa wa Iringa, Tanzania. Ili kufanikisha kazi hii, Kanuni Tazamishi (KAT) iliongoza utafiti huu, yaani unyambulishaji wa vitenzi kimofolojia unaakisi unyambulishaji wa vitenzi kisintaksia. Mbinu za utafiti zilihusu: usampulishaji, ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Data ya utafiti ni ya kutoka uwandani ambapo vitenzi viliteuliwa na kuwekwa katika kategoria mbili; vitenzi visoukomo katika kundi moja na vitenzi vya silabi moja katika kundi jingine. Kazi imegawanyika katika sura tano. Sura ya kwanza, imeeleza kiini cha utafiti na utaratibu uliozingatiwa katika kufanikisha utafiti. Sura ya pili, imeshughulikia mapitio ya maandiko kuhusiana na unyambulishaji na mfuatano wa mofimu katika lugha. Mapitio haya yamebainisha kuwa minyambuliko na mifuatano ya mofimu katika lugha ipo. Sura ya tatu, imehusu mbinu za utafiti ambapo populesheni, sampuli, usampulishaji pamoja na njia tatu za ukusanyaji data zilibainishwa. Sura ya nne, imeshughulikia uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Kwa ujumla data, iliyopatikana imechanganuliwa kwa njia ya maelezo na kanuni. Kanuni Tazamishi ya Baker (1985) ndiyo iliyoongozo mjadala na uchanganuzi wa data hii. Sura ya tano imeshughulikia matokeo, hitimisho, na tafiti fuatishi. Matokeo ya utafiti yamebainisha minyambuliko mitano na kwamba, lugha ya Kikinga inapangilia mofimu nyambulishi zake kwa mujibu wa Kanuni Tazamishi inayodai unyambulishaji kimofolojia huakisi unyambulishaji sintaksia. Aidha, kanuni ya uukiliwaji iliyoundwa ina tenda kazi pia, katika mfuatano wa mofimu nyambulishi katika lugha ya Kikinga, yaani mofimu moja ikitangulia ina kawaida ya kuukilia mofimu ambazo zinaweza kuifuata na ama kutoifuata yenyewe.