PhD Theses
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing PhD Theses by Subject "Bantu language"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Ruwaza za toni katika vitenzi na nomino za kirombo(University of Dar es Salaam, 2020) Mramba, Peter ThobiasUtafiti huu unahususu Ruwaza za Toni katika Vitenzi na Nomino za Kirombo. Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza ruwaza za ujitokezaji wa toni katika vitenzi na nomino za Kirombo na kanuni zinazotawala utokeaji huo. Utafiti umeongozwa na Nadharia ya Fonolojia Vipandesauti Huru kwa kutumia Mkabala wa Tonijuu Msingi kama ulivyoasisiwa na Goldsmith (1976) na kuboreshwa na wanazuoni mbalimbali katika taaluma ya tonolojia. Utafiti ulifanyikia katika Vijiji vya Mengwe Juu na Mengwe Chini, Kata ya Mengwe, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro. Wango la utafiti ni nomino na vitenzi na wazungumzaji wazawa wa Kirombo. Aidha, mbinu ya usampulishaji iliyotumika ni Nasibu Tabakishi. Pia, Mbinu za ukusanyaji data zilizotumika ni: mahojiano na ushuhudiaji. Katika mahojiano nomino na vitenzi viliandaliwa kwa Kiswahili na watoataarifa walihitajika kuyatamka kwa Kirombo huku mtafiti akirekodi na kualamisha toni katika maneno hayo. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa kuna ruwaza mbalimbali za kitoni zinazoleteleza utokeaji wa kanuni za kitoni ambazo hutofautiana kutegemeana na idadi ya silabi na uwepo au kutowepo kwa yambwa. Kwa vitenzi na nomino za silabi moja hutawaliwa na kanuni ya uhusishaji wa tonichini na vitamkwa na sharti la ukubalifu, wakati vitenzi na nomino za silabi tatu hadi ama tano au sita za shina hutawaliwa na kanuni ya msambao wa tonijuu kuelekea kulia mwa shina, uhamaji wa TJM kutoka silabi ya kwanza kwenda katika silabi ya pili ya shina, unakiliji wa TJM katika silabi ya mwisho kasoro moja. TJM katika vitenzi na nomino za silabi moja ya shina hubiruka nyuma na khupachikwa katika kiambishi awali kwa nomino na vitenzi visoukomo sahili, wakati TJM hupachikwa katika mofimu ya yambwa kwa vitenzi visoukomo changamani vya silabi moja ya shina. Pia, kwa upande wa vitenzi visoukomo sahili matokeo yanaonesha kwamba kuna TJM mbili, yaani, ya kwanza ni ya yambwa na ya pili ikiwa ya shina, ambapo katika mchakato wa ukokotozi wa uibuzi wa toni, TJM ya shina hudondoshwa kwa kuwa yambwa ina nguvu zaidi. Aidha, inapendekezwa tafiti fuatizi zifanyike katika viwango vya kirai na sentensi, uradidi katika nomino na vitenzi na tonolojia linganishi katika jamiilugha za Kichaga. Utafiti huu umesaidia kujua namna toni zinavyojitokeza katika Kirombo kwa ujumla.Item Ulinganishi wa lugha za ‘’Runyaċitara’’(Chuo kikuu cha Dar es Salaam, 2019) Asiimwe, CarolineUtafiti, huu ulihusu ulinganishi wa lugha za ‘’Runyaċitara’’ ili kufanunua kama zina uhusiano wa kimnasaba baina yake au la. Malengo mahususi yaliyoshughulikiwa ni kubainisha historia ya lugha hizi, kufanunua kutofautiana na kufanana kulikopo kati ya lugha hizi na tatu ni kutathmini kama hizi ni lugha moja, makundi mawili au kila lugha inajitegemea. Nadharia ya mwanachano na Makutano ya lugha za kibantu na nadhariatete yake ya ndugu na ndugu wa mbali kiisimu ambazo ziliasisiwa na Massamba (2007) zimetumiwa kueleza historia ya lugha hizi pamoja na kutathamini uhusiano wa lugha hizi kwa kuegemea kiwango cha ukaribu kiisimu. Aidha, ya Isimu historian na linganishi ambayo mwasisi wake ni William Jones 1786 imetumiwa kuelezea vipengele vya kiisimu na msamiati wa msingi kisinkroniki na kidikronuki. Mikabala mchanganyiko imetumiwa katika utafiti huu, na maeneo ya utafiti yamehusisha Wilaya za Kabarole, Hoima, Mbarara na Kabale ambazo zimo nchini Uganda. Vilevile, usampulishaji hatua ulitumiwa kuchagua maeneo mahususi na watoa taarifa kimaksudi na pia kwa kutumia usampulishaji tajwa. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya hojaji, kuptia maandiko, mahojiano, uthibitishaji kauli na usaili. Data hizi zilihusu historia ya wazungumzaji na lugha zaopamoja na taarifa za kiisimu; msamiati wa msingi, mfumo wa sauti na sauti mrejeo, mofolojia, ngeli za nomino na hali na njeo ili kufanunua uhusiano wa lugha hizi. Data zimechanganuliwa kwa kutumia mbinu linganishi, takwimu leksika, maelezo na programu ya ‘linganishi lugha kwa mfumo wa kompyuta’. Matokeo yamewasilishwa kwa njia ya maelezo nay a kitakwimu ili kuelezea uhusiano wa lugha za ‘’Runyacitara’’. Matokeo yanaonesha kwamba hizi ni lugha zenye mnasaba ambazo zilitokana na mame- lugha moja. Lugha hiz zinajibainisha katika makundi mawili ya Runyoro na Rutooro na kundi la Runyankore na Ruċiga kutokana na mabadiliko ya lugha na kila kundi ni ndugu ya mbali kwa kundi jingine. Hali ya lugha hizi tunayoiona leo hii inaweza kufafanuliwa kidikroniki kama matokeo yanavyoonesha mabadiliko ya lugha yaliyotokea kiisimu. Kwa upande mwingine, kwa sababu yawazungumzaji kutaka kujibainisha kama watu wa jamii tofauti huwa wanaibuka na miundo mipya ili kujitofautisha na wenzao. Hitimisho ni kwamba lugha hizi zina uhusiano wa kimnasaba kwa kuhusisha mfanano wa 85.39% katika msamiati wa msingi na vipengele vingine vya kiisimu. Matokeo ya uundaji upya yalionesha kwamba maumbo tunayoyaona leo hii ya;itokana na maumbo ya awali. Kwa hivyo, lugha hizi ni kundi moja la lugha lenye makundi ndani mwake ambayo ni lahaja. Matokeo haya yana mchango mkubwa katika kufafanua uhusiano wa lugha za Runyoro, Rutooro, Runyankore na Ruċiga kwa kuegemea historia ya wazungumzaji wake na maendelo ya lugha kiisimu, nadharia, utafiti umethibitisha kwamba hali ya lugha kisinkronia inaweza kufafanuliwa kidikronia na vilevile kuthibitisha kwamba mijongeo ya watu inaweza kusababisha mwanachano na makutano ya lugha. Aidha, matokeo yanachangia katika data za kisiimu za lugha za kibantu na nadharia ya isimu kwa ujumla pamoja na data zilizoko makavazini. Inapendekezwa kuwe na utafiti zaidi juu ya; lugha nyingine zinazoonesha mfanano na hizi; nafasi ya teknolojia katika mwachano na makutano ya lugha; athari ya uhusiano wa lugha hizi katika vipengele vingine vya kijamii na vipengele mahususi vya kiisimu katika lugha hizi. Aidha, kuna haja ya kuwa na usanifishaji wa mfumo rasmi wa ‘’Runyaċitara’’.