Institute of Kiswahili Studies
Permanent URI for this community
Browse
Browsing Institute of Kiswahili Studies by Subject "Aids (Disease)"
Now showing 1 - 4 of 4
Results Per Page
Sort Options
Item Fasihi simulizi na ukimwi: Mifaano kutoka katika nyimbo za ngoma ya wigashe ya wasukuma(University of Dar es Salaam, 2012) Nzobe, Lucia RaphaelUtafiti huu umechambua nyimbo za ngoma ya Wigashe. Utafiti ulihusisha nyimbo mbalimbaliza ngoma ya Wigashe zinazohusu UKIMWI. Lengo katika utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza usawiri wa ugonjwa wa UKIMWI katika nyimbo za ngoma ya Wagashe Data na taaarifaa za utafiti huu zimekusanywa kutoka maktabani na uwandani, na mbinu zilizotumika katika kutupatia data ni mbinu za uchambuzi matini, mbinu ya mahojiano pamoja na majadiliano ya vikundi amabzo zilitupatia data za msingi na data za upili. katika utafiti wetu zimetumika nyimbo nane na uchunguzi wa nyimbo hizo umefanyika kwa kutumiua mkabala wa kimaelezo kwa kuongozwa na nadharia ya Usosholojia. Baada ya uchambuzi wa nyimbo hizo imebainika kuwa dhamira katika nyimbo hizo zinaujadili ugonjwa wa UKIMWI kwa namna mbalimbali. Kuna dhamira zinazohusu sababu za maabukizi, dalili za UKIMWI, ushauri na uhamasishaji juu ya ugonjwa huu na zile zinazozungumzia juu ya tiba ya UKIMWI. Pia, imedhihirika kuwa ushindani katika nyimbo za ngoma ya Wigashe pamoja na matumizi ya tamadhali za semi vimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuibua dhamira mbalimbali zinazohusu ugojwa wa UKIMWI. Mwisho, limetolewa hitimisho la utafiti mzima pamoja na mapendekezo ya maeneo ambayo yanahiotaji kutafitiwa zaidi ili kuweza kukuza uelewa wa nafasi ya kazi za fasihi simulizi za kabila la Wasukuma katika kuzungumzia masuala ya kijamiiItem Mandhari na usawiri wa ukimwi katika riwaya ya kiswahili 2000-2010(University of Dar es Salaam, 2016) Bulaya, JovietUtafiti huu umechunguza jinsi ugonjwa wa UKIMWI unavyosawiriwa katika fasihi kwa kuiangalia riwaya ya Kiswahili kupitia katika kipengele cha mandhari. Utafiti unalenga kujibu maswali yafuatayo: kwanza, ni jinsi gani mandhari ya riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI inafungamana na dhamira zinazosawiriwa na riwaya husika? Pili, riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI inatumiaje mandhari kuumba wahusika wake? Na mwisho, waandishi wa riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI wanatumiaje mandhari kujenga lugha inayoibua athari na changamoto za UKIMWI katika riwaya zao? Sambamba na maswali hayo, tumefafanua malengo ya utafiti huu kuwa ni: mosi, kujadili jinsi mandhari inavyofungamana na dhamira zinazoelezwa na riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI. Pili, kueleza jinsi riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI inavyotumia mandhari kuumba wahusika wake. Na tatu ni kubainisha namna waandishi wa riwaya ya Kiswahili ihusuyo UKIMWI wanavyotumia mandhari kuumba lugha inayoibua athari na changamoto za UKIMWI katika riwaya zao. Ili kufikia kusudi la utafiti huu , tumetumia mbinu mbalimbali za utafiti zikiwamo za utafiti wa nyaraka na mahojiano. Mbinu hizi kwa pamoja zimetumika kukusanya data zilizosaidia kujibu maswali ya utafiti huu. Nadharia ya Mwingiliano-matini ndiyo imeongoza utafiti huu. Nadharia hii inasisitiza kuwa hakuna matini asilia, bali uhai wa matini moja hutegemea matini nyingine. Kwa hiyo, matini za kifasihi hutegemeana katika kukamilisha maana. Kwa kutumia nadharia hii tumeona kuwa, mandhari zinaingiliana, kukamilishana na kutegemeana katika kuliumba tatizo la UKIMWI. Hii inatokana na ukweli kuwa, riwaya zinazochunguzwa zimetumia mandhari mbalimbali kuwaumba wahusika, kuibua dhamira na kuchomoza lugha inayoelezea athari na changamoto za UKIMWI. Kutokana na utafiti huu, upo uhusiano mkubwa kati ya mandhari na uibuaji wa dhamira za kazi ya fasihi. Pili, kuna uhusiano kati ya mandhari na ujenzi wa wahusika. Wasifu, tabia na mienendo ya wahusika wa riwaya teule kwa sehemu kubwa ni matokeo ya mandhari wanamokuwa. Vilevile, mandhari inahusiana na lugha kwani, lugha inayotumiwa na wahusika katika riwaya inategemea mandhari wanamokuwa. Hii inathibitisha kuwa, mandhari ina umuhimu mkubwa katika kuibua dhamira, kuwaumba wahusika pamoja na kutolea ujumbe uliokusudiwa katika kazi ya fasihi hasa riwaya. Kutokana na uchunguzi wa riwaya teule, kazi ya fasihi hasa riwaya haikamilishwi na mandhari moja, bali upo mwingiliano mkubwa wa mandhari mbalimbali ambao unaifanya riwaya ikamilishe maana na kusudi la mwandishi. Na kwa hiyo, mandhari ni mojawapo ya mihimili muhimu katika kuumba maana ya kazi ya fasihi.Item Tamthilia za kiswahili kuhusu ukimwi: ulinganishi wa upokezi kutoka kwa wanafunzi wa sekondari tanzania(University of Dar es Slaam, 2011) Omary, MwanahamisiLengo la utafiti huu lilikuwa ni kubainisha na kulinganisha upokeaji wa tamthilia zinazohusu UKIMWI miongoni mwa wanafunzi wa sekondari katika Tanzania. Ili kukamilisha kazi hii, wanafunzi wa sekondari kutoka katika mkoa wa Dar es Salaam waliteuliwa kutoka katika shule tatu ambazo ni sekondari Tegeta, Benjamin Mkapa na Jitegemee. Aidha, Katika utafiti huu, tamthilia teule tatu zilitumika katika kufanya uchambuzi wa data ambazo ni Ngoswe Penzi Kitovu Cha Uzembe,Kilio Chetu na Orodha. Katika kukusanya na kuchambua data, marejeo mbalimbali yalitumika kutoka maktabani na uwandani. Pia mbinu mbalimbali zilitumika kukusanyia data. Zaidi ya hayo, uchambuzi wa data uliongozwa na nadharia ya Upokezi au Mwitiko wa msomaji kwa mujibu wa Stanley Fish (1980). Katika utafiti huu ingawa dhamira nyingi zinafanana, ilibainika kuwa wanafunzi wanapendelea zaidi tamthilia zinazoongelea UKIMWI kuliko zisizokuwa za UKIMWI. Jambo hili ni kinyume na matarajio ya kawaida, kwani katika tafiti nyingi (Taz. Dorothy Nelkin na wenzake, 1991) wasomaji hawapendelei kusoma kazi zinazohusu magonjwa au vifo. Upokezi wa tamthilia hizi miongoni mwa mbinu nyingine umehamasishwa na matumizi ya mbinu mbalimbali za lugha ya ubunifu ambayo imesheheni katika kazi hizi. Utafiti huu wa kiulinganishi utawasaidia wanafasihi hasa wale wa fasihi linganishi.Vilevile utafiti huu unapendendekeza kufanyika kwa kina tafiti katika tanzu nyingine za fasihi ili kuangalia upokezi na mwitiko wa jamii kwa ujumla kwa kuhususisha watu mbalimbali kama wazee na vijana ambao si wanafunzi.Item Ufanisi wa elimu ya ujinsia shuleni katika kukuza maarifa na stadi kuhusu kujikinga na mimba na VVU Tanzania(University of Dar es Salaam, 2012) Bilinga, Margareth JosephMadhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza ufanisi wa elimu ya ujinsia (EU) shuleni katika kukuza maarifa na stadi zinazohusiana na uzuiaji wa mimba na kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. Mantiki ilikuwa kwamba uelewa wa jinsi walimu na wanafunzi wanavyopata uzoefu kuhusiana na elimu ya ujinsia katika shule pengine ungeweza kuchangia kubuni njia bora zaidi za kukabiliana na maambukizi ya VVU/UKIMWI na kuzuia mimba. Kwa kuzingatia suala hili, utafiti huu uliongozwa na malengo matano ya utafiti: kuchunguza ni elimu ipi ya ujinsia inatolewa katika shule za msingi na inatolewa kwa namna gani; kuchunguza maarifa ya walimu kwa ajili ya kutoa EU yenye ufanisi; kuchunguza uelewa wa wanafunzi kuhusu EU; kutathmini mitazamo ya wanafunzi, walimu, na wazazi kuhusu EU; na mwisho, kutathmini changamoto zinazoathiri utoaji wa EU. Utafiti huu ulitumia mbinu mchanganyiko ambapo mikabala yote miwili, yaani ule wa kitakwimu na ule wa kimaelezo, ilitumika. Walengwa wa utafiti walitokana na jumla ya washiriki wapatao 390 ambao walijumuisha wakuu wa shule, wazazi, walimu na wanafunzi. Mbinu za ukusanyaji wa data zilikuwa ni pamoja na uchunguaji, hojaji, usaili/mahojiano, na mapitio ya nyaraka. Data zilichambuliwa na kuwasilishwa kitakwimu na kimaelezo. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba ingawa EU imetoa maarifa fulani kuhusu masuala mbalimbali shuleni, wanafunzi walikosa stadi stahiki ambazo ni muhimu katika kuzuia mimba na maambukizi ya VVU. Matokeo pia yanaonyesha kwamba wakati wanafunzi walionyesha maarifa ya kutosha juu ya VVU/UKIMWI, hawakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya mambo mengine yanayohusiana na ujinsia. Hali hii ilitokana na walimu kukosa maarifa na stadi sahihi za kufundisha kwa ufanisi mada za EU. Hali hiyo pia ilitokana na mijadala finyu ya umma juu ya masuala ya ngono. Kipekee, utafiti unaonyesha kwamba walimu, wanafunzi na wazazi walikuwa na mitazamo chanya juu ya utoaji wa EU katika shule za msingi. Hata hivyo, changamoto mbalimbali ziliwavunja moyo walimu na wanafunzi kujifunza mada za EU. Changamoto hizo ni pamoja na sera duni, ukosefu wa mafunzo, vikwazo vya kiutamaduni, na tabia binafsi. Utafiti unapendekeza hatua kadhaa za kuboresha ufundishaji wa EU katika shule za msingi. Nazo ni pamoja na, miongoni mwa nyinginezo, kuanzisha mafunzo na mafunzo kazini ili kuboresha maarifa na stadi za taaluma ya ufundishaji miongoni mwa walimu ili waweze kufundisha EU kwa ufanisi na hali kadhalika kufundisha EU kwa kutilia mkazo nyanja zote jumuishi ili kuboresha maarifa ya wanafunzi kuhusu EU kwa jumla. Kwa hakika, maudhui kuhusu mimba hayana budi kuanzishwa mapema iwezekanavyo kama ilivyo kwa VVU na UKIMWI. Vilevile inapendekezwa kwamba majadiliano na mijadala ya wazi kuhusu EU miongoni mwa wadau mbalimbali kama vile wazazi, wanafunzi, viongozi wa dini na wanasiasa inapaswa kuhamasishwa na kukuzwa. Utafiti pia unatoa wito kwa tafiti nyingine kuchunguza jinsi wanafunzi wanavyotumia maarifa na stadi za EU kujikinga dhidi ya hatari za kingono, hususani mimba na VVU.