Ufanisi wa elimu ya ujinsia shuleni katika kukuza maarifa na stadi kuhusu kujikinga na mimba na VVU Tanzania

No Thumbnail Available
Date
2012
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza ufanisi wa elimu ya ujinsia (EU) shuleni katika kukuza maarifa na stadi zinazohusiana na uzuiaji wa mimba na kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. Mantiki ilikuwa kwamba uelewa wa jinsi walimu na wanafunzi wanavyopata uzoefu kuhusiana na elimu ya ujinsia katika shule pengine ungeweza kuchangia kubuni njia bora zaidi za kukabiliana na maambukizi ya VVU/UKIMWI na kuzuia mimba. Kwa kuzingatia suala hili, utafiti huu uliongozwa na malengo matano ya utafiti: kuchunguza ni elimu ipi ya ujinsia inatolewa katika shule za msingi na inatolewa kwa namna gani; kuchunguza maarifa ya walimu kwa ajili ya kutoa EU yenye ufanisi; kuchunguza uelewa wa wanafunzi kuhusu EU; kutathmini mitazamo ya wanafunzi, walimu, na wazazi kuhusu EU; na mwisho, kutathmini changamoto zinazoathiri utoaji wa EU. Utafiti huu ulitumia mbinu mchanganyiko ambapo mikabala yote miwili, yaani ule wa kitakwimu na ule wa kimaelezo, ilitumika. Walengwa wa utafiti walitokana na jumla ya washiriki wapatao 390 ambao walijumuisha wakuu wa shule, wazazi, walimu na wanafunzi. Mbinu za ukusanyaji wa data zilikuwa ni pamoja na uchunguaji, hojaji, usaili/mahojiano, na mapitio ya nyaraka. Data zilichambuliwa na kuwasilishwa kitakwimu na kimaelezo. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba ingawa EU imetoa maarifa fulani kuhusu masuala mbalimbali shuleni, wanafunzi walikosa stadi stahiki ambazo ni muhimu katika kuzuia mimba na maambukizi ya VVU. Matokeo pia yanaonyesha kwamba wakati wanafunzi walionyesha maarifa ya kutosha juu ya VVU/UKIMWI, hawakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya mambo mengine yanayohusiana na ujinsia. Hali hii ilitokana na walimu kukosa maarifa na stadi sahihi za kufundisha kwa ufanisi mada za EU. Hali hiyo pia ilitokana na mijadala finyu ya umma juu ya masuala ya ngono. Kipekee, utafiti unaonyesha kwamba walimu, wanafunzi na wazazi walikuwa na mitazamo chanya juu ya utoaji wa EU katika shule za msingi. Hata hivyo, changamoto mbalimbali ziliwavunja moyo walimu na wanafunzi kujifunza mada za EU. Changamoto hizo ni pamoja na sera duni, ukosefu wa mafunzo, vikwazo vya kiutamaduni, na tabia binafsi. Utafiti unapendekeza hatua kadhaa za kuboresha ufundishaji wa EU katika shule za msingi. Nazo ni pamoja na, miongoni mwa nyinginezo, kuanzisha mafunzo na mafunzo kazini ili kuboresha maarifa na stadi za taaluma ya ufundishaji miongoni mwa walimu ili waweze kufundisha EU kwa ufanisi na hali kadhalika kufundisha EU kwa kutilia mkazo nyanja zote jumuishi ili kuboresha maarifa ya wanafunzi kuhusu EU kwa jumla. Kwa hakika, maudhui kuhusu mimba hayana budi kuanzishwa mapema iwezekanavyo kama ilivyo kwa VVU na UKIMWI. Vilevile inapendekezwa kwamba majadiliano na mijadala ya wazi kuhusu EU miongoni mwa wadau mbalimbali kama vile wazazi, wanafunzi, viongozi wa dini na wanasiasa inapaswa kuhamasishwa na kukuzwa. Utafiti pia unatoa wito kwa tafiti nyingine kuchunguza jinsi wanafunzi wanavyotumia maarifa na stadi za EU kujikinga dhidi ya hatari za kingono, hususani mimba na VVU.
Description
Available in print form
Keywords
Sexuality Education, Pregnancies, Aids (Disease), Tanzania
Citation
Bilinga, M.J (2012),Ufanisi wa elimu ya ujinsia shuleni katika kukuza maarifa na stadi kuhusu kujikinga na mimba na VVU Tanzania , master dissertation, University of Dar es Salaam (available at http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)