PhD Theses
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing PhD Theses by Author "Hans, Mussa Mohamed"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Mchango wa lahaja katika kukuza na kuendeleza kiswahili sanifu hazina fiche iliyomo katika lahaja za kiswahili za Zanzibar(University of Dar es Salaam, 2014) Hans, Mussa MohamedUtafiti huu ulikusudia kuchunguza msamiati unaohusu majina ya samaki wa baharini katika jamii ya wazungumzaji wa lahaja za Kiswahili zilizoko Zanzibar. Lengo likiwa ni kubaini namna lahaja hizi zinavyoweza kuchangia katika kukuza na kuendeleza Kiswahili Sanifu. Hata hivyo, ilionekana kwamba litakuwa jambo la welekevu iwapo pia historia ya wazungumzaji wa lahaja hizo na mchango wao katika historia ya lugha ya Kiswahili vitachunguzwa kwa kina. Data za utafiti zilipatikana uwandani kwa kuhusisha mbinu mbalimbali ambazo ni ushuhudiaji, usaili, hojaji na majadiliano katika majopo. Baaadhi ya data pia zilipatikana maktabani. Kwa upande wa uchambuzi wa data, palitumika mbinu ya kikompyuta kuchambulia data za kimsamiati na data za kihistoria zilichambuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaelezo. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Mwachano - Makutano ya Lugha za Kibantu pamoja na nadhariatete ya Ndugu na Ndugu wa Mbali iliyoasisiwa na Massamba (2007). Nadharia hii pamoja na nadhariatete inayoishajihisha kwa kiasi kikubwa inawiana na matokeo ya utafiti. Hata hivyo, katika utafiti huu imependekezwa kwamba nadhariatete ya Ndugu na Ndugu wa Mbali ifanyiwe marekebisho kidogo kwa kuongezewa dhana ya Ndugu wa Karibu ili kuakisi vema uhusiano ulioko miongoni mwa lahaja za Kiswahili na pengine lugha mbalimbali za Kibantu. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba wazungumzaji wa lahaja za Kiswahili kupitia katika lahaja zao wana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili hususani katika uwanja wa msamiati unaohusu majina ya samaki wa baharini pamoja na uwanja wa historia ya lugha ya Kiswahili kwa ujumla. Utafiti kuhusu msamiati wa majina ya samaki wa baharini mbali na kutoa taarifa zinazohusu majina ya aina anuwai za samaki na sifa zao, umebainisha pia msamiati mpya ambao haumo katika Kiswahili Sanifu. Katika mjadala huu pia utafiti umeweka bayana tofauti ya kimsamiati baina ya Zanzibar na Tanzania bara, tofauti ambazo pia zinajitokeza katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyoandikwa na TUKI na Kamusi la Kiswahili Fasaha iliyoandikwa na BAKIZA. Hata hivyo imependekezwa kwamba utafiti mwingine katika jamii za wazungumzaji wa lahaja za Kiswahili unaweza kuelekezwa katika msamiati unaohusu nyanja nyingine kama vile utamaduni na tiba. Katika utafiti wa kihistoria, mbali na mambo mengine utafiti umebainisha kwamba chimbuko la wazungumzaji wa lahaja za Kimakunduchi, Kitumbatu na Kipemba ni maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na Kenya hususani maeneo yanayopatikana katika upwa wa Afrika Mashariki. Maeneo hayo ni pamoja na Bagamoyo, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Mombasa. Hata hivyo, kuna baadhi ya watoa taarifa waliodai kwamba chimbuko lao ni Shiraz (Pashia) ingawa hawakuwa na ushahidi usiosailika.