Masters Dissertations
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Masters Dissertations by Author "Adolph, Editha"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Utohozi wa istilahu za kiingereza katika Kiswahili: uchunguzi kifani wa taaluma za tiba na compyuta(University of Dar es Salaam, 2019) Adolph, EdithaKila lugha huwa na utaratibu wake wa ukuzaji na uendelezaji wa msamiati. Katika mchakato wa kupata msamiati wa lugha husika, mbinu mbalimbali hutumika. Utohozi ni mbinu moja wapo ambayo lugha hutumia katika kujitajirisha kimsamiati. Ili msamiati uweze kukubalika katika mbinu hii, kuna michakato mbalimbali inayopitiwa. Michakato hiyo huweza kusababisha athari katika lugha pokezi. Utafiti huu umechunguza utohozi wa istilahi za fani ya tiba na kompyuta za kiingereza katika lugha ya Kiswahili kwa kuangazia michakato na athari zake. Utafiti umefanyika katika jiji la Dar es Salaam hususan katika chuo kikuu cha Dar es Salaam kilichoko Wilaya ya Ubungo pamoja na baraza la Kiswahili la taifa lililopo wilaya ya Kinondoni. Nadharia zilizoongoza utafiti huu ni nadharia ya Fonolojia Zalishi (NFZ) iliyoasisiwa na Naomi Chomsky na Moris Halle (1968) pamoja na andharia ya mofolojia Leksika (NML). Ambayo mwasisi wake ni Kiparsky (1982). Aidha, data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia mbinu za hojaji na uchambuzi wa matini. Data iliyokusanywa ilichambuliwa kwa kutumia mkataba wa maelezo na wa kitakwimu. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa lugha ya Kiswahili imetoa istilahi za fani ya tiba na kompyuta kutoka katika kiingereza. Pia, utafiti umebaini kuwa wakati wa utohozi wa istilahi katika Kiswahili, michakato mbalimbali ya kifonolojia, kimofolojia na kisintaksia hufanyika. Michakato hufanyika kadiri kanuni na taratibu za lugha ya Kiswahili ili istilahi ziweze kukubalika. Michakato ya kifonolojia iliyobainishwa katika utafiti huu ni pamoja na mchakato wa udondoshaji, uchopekaji, usahilishaji wa irabu uangalifu kuwa irabu sahili na mchakato wa ufupishaji wa irabu ndefu. Michakato ya kimofolojia iliyoonekana kutokana na uchambuzi wa data ni pamoja na uambishaji ambao unafungamana na upangaji wa istilah za Kiingereza katika ngeli za Kiswahili uchakataji wa istilahi zenye muundo wa maneno ambatani Kisintaksia, imabainika kuwa istilahi hutoholewa kwa kuhusisha mchakato wa kuchopeka vihusishi kati ya istilahi za Kiingereza. Halikadhalika, utafiti huu umebaini kuwa utohozi wa istilahi za fani ya tiba na kompyuta za kiingereza za kiingereza katika Kiswahili una athari chanya na hasi katika lugha ya Kiswahili. Athari chanya zilizobainika ni pamoja na zile za kifonolojia, kisemantiki na kileksia. Athari za kifonolojia zilizoonekana katika utafiti huu ni pamoja na muundo mpya wa silabi katika Kiswahili na athari za kimatamshi zinazoambatana na ufifishaji wa sauti. Athari za kisemantiki zilizobainika ni pamoja na upatikanaji wa dhana za kisayansi pamoja na visawe vinavyotokana na utohozi. Kwa upande wa athari za kileksika, imedhihirika kuwa baadhi ya istilahi za fani za tiba ya compyuta zimeonekana kuongezeka katika Kiswahili. Athari hasi zilizobainika ni pamoja na pamoja na zile za kimofolojia, kisemantiki na kileksika. Kimofolojia imeonekana kuwa utohozi umesababisha muundo wa istilahi ndefu na zenye kutatanisha katika matamshi. Halikadhalika, Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kisemantiki kumezuka mfumuko wa visawe katika Kiswahili. Kileksika imebainika kuwa zipo istilahi za tiba na kompyuta zinazotumika mara chache. Utafiti huu umependekeza kwamba utohozi wa istilah za lugha mbalimbali ufuate kanuni na taratibu zinazowekwa katika Kiswahili. Aidha kuna haja ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kutumia istilahi za Kiswahili hata kama kuna istilahi zinazotoholewa. Hivyo mtafiti anapendekeza kuwa pawepo na uhamasishaji wa matumizi ya istilah za Kiswahili zilizopo ili kuepuka mfumko wa istilahi nyingi zinazorejelea dhana moja. Mtafiti kuwa kuna haja ya kufanya uchunguzi zaidi kuhusu utohozi wa istilahi za kiingereza katika Kiswahili kwa miaka ijayo kwa kuwa ni bayana kuwa mchakato wa utohozi ni endelevu.Item Utohozi wa nomino za kiswahili na athari yake katika ngeli za kihaya(University of Dar es Salaam, 2014) Adolph, EdithaUtafiti huu umechunguza utohozi wa nomino za Kiswahili katika Kihaya na athari yake katika ngeli za Kihaya. Utafiti umefanyika katika kata za Izigo, Mayondwe na Muhutwe wilayani Muleba mkoa wa Kagera nchini Tanzania. Kazi hii iliongozwa na Nadharia ya Mofolojia Leksika ya Kiparsky (1982). Aidha, data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia mbinu za hojaji, mahojiano, ushuhudiaji pamoja na njia za uwandani na maktabani. Halikadhalika, mkabala usio wa kiidadi ulitumika katika ukusanyaji na uchambuzi wa data ya utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa lugha ya Kihaya imekopa baadhi ya nomino kutoka katika Kiswahili. Baada ya nomino za Kiswahili kutoholewa katika Kihaya, zimefanyiwa michakato ya kifonolojia na kimofolojia kadiri ya kanuni na taratibu za lugha ya Kihaya ili ziweze kukubalika katika lugha ya Kihaya. Vilevile utafiti huu umebaini kuwa kuna athari ya kingeli inayotokana na utohozi wa nomino za Kiswahili katika lugha ya Kihaya. Kwa mfano, athari ya nomino za asili za Kihaya kubadili ngeli zake. Aidha, katika utafiti huu inapendekezwa kwamba uchunguzi ufanyike kuhusu mabadiliko ya ngeli yaliyotokea kuanzia zama za Mame-Bantu. Pia, mtafiti anapendekeza maeneo mengine yafanyiwe tafiti, mfano, uainishaji wa lahaja za Kihaya, fonolojia, semantiki, sintaksia na mofolojia ya Kihaya. Aidha, kuna haja ya kufanya uchunguzi tena kuhusu utohozi wa nomino za Kiswahili katika Kihaya kwa miaka ijayo kwani ni wazi kuwa mchakato wa ukopaji na utohozi ni endelevu.