Nafasi ya lugha ya kiswahili katika mandhari- lugha ya jiji la Mbeya nchini Tanzania

Loading...
Thumbnail Image
Date
2020
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es salaam
Abstract
Utafiti huu ulihusu nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Lengo kuu lilikuwa kuchunguza nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Malengo mahususi yalikuwa matatu: kwanza, kubainisha ruwaza za lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Pili, kudhihirisha nafasi ya lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia ruwaza za lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Tatu, kuwianisha sera ya lugha ya Tanzania na nafasi ya lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Ubeberu wa Kiisimu yenye msingi kwamba katika jamii kuna vipengele vya kimfumo na kiitikadi vinavyosababisha uhusiano usio wa usawa miongoni mwa lugha za jamii mbalimbali. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya upigaji wa picha za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu na mbinu ya usaili. Uchambuzi wa data za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu ulifanyika kwa mbinu ya usomaji wa matini na Programu Tarakilishi ya Takwimu (PTT). Uwasilishaji wa data umefanyika kwa kutumia vielelezo vya majedwali, grafu na picha kwa data za kiidadi za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu. Nukuu za usaili na ufafanuzi wa kinathari umetumika kwa data za kitaamuli. Matokeo yanaonesha kwamba kuna ruwaza nne za lugha katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Ruwaza zilizobainishwa ni Kiswahili pekee, Kiingereza pekee, Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili. Kiswahili kinajitokeza kwa asilimia 54.5 katika ruwaza ya Kiswahili pekee mbele ya Kiingereza. Kwa kigezo cha ukubwa wa maandishi Kiswahili kinajitokeza cha kwanza kwa asilimia 63 kwa maandishi makubwa zaidi kuliko Kiingereza. Vilevile, kwa kigezo cha idadi ya maneno Kiswahili kinajitokeza katika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 72.23. Kwa hiyo, Kiswahili kinajitokeza katika nafasi ya kwanza kimatumizi katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Aidha, kuna uwiano baina ya Sera ya Lugha ya Tanzania na nafasi ya matumizi ya lugha katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya. Hata hivyo, tunapendekeza serikali ifanye mapitio ya sera ya lugha ili kuunda kanuni za matumizi ya lugha katika mandhari-lugha na kuweka urari wa matumizi ya lugha katika mandhari-lugha. Vilevile, tafiti fuatishi zifanyike kwa kuchunguza mabango ya makampuni mahususi tofautitofauti ili kupanua uelewa kuhusu ruwaza za lugha, nafasi ya Kiswahili na uwiano wa nafasi ya matumizi ya lugha na Sera ya lugha ya Tanzania.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr.Wilbert Chagula Library, class mark (THS EAF PL8701T34K396)
Keywords
Bantu languages, Swahili language, Mbeya Municipal, Tanzania
Citation
Kawonga, G (2020) Nafasi ya lugha ya kiswahili katika mandhari- lugha ya jiji la Mbeya nchini Tanzania, Doctoral dissertation , University of Dar es Salaam, Dar es Salaam.
Collections