Dhima ya mhusika mlevi na muakiso wa uhalisi wa kauli zake: mifano kutoka lina ubani na mabepari wa bongo

Date

2012

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu umejadili kuhusu Mhusika mlevi na uhalisi wa kauli na matendo yake katika fasihi andishi ya Kiswahili, kwa kutumia mifano kutoka Lina Ubani na Mabepari wa Bongo. Tatizo lililojenga utafiti ni kutokana na muonekano wa mlevi wa kila siku katika jamii, na matumizi ya mhusika mlevi katika kazi za fasihi. Mlevi siku zote huonekana kama punguani, mtu dhalili, na msema ovyo, mtu aliyejishindwa na anayeshindwa kuzuia hisia zake pindi anapolewa. Swali tunalojiuliza ni kwa nini watunzi wa fasihi wanamtumia katika katika kazi zao ili hali wanajua hali yake? Dhima yake halisi ni ipi katika jamii husika? Utafiti huu ulitumia mbinu ya maktabani, ambapo matini nyingi zilisomwa ili kupata ruwaza ya jumla kuhusu mhusika mlevi na uhalisi wa kauli na matendo yake katika fasihi andishi. Utafiti huu umeongozwa na nadharia mbili, nadharia ya Ucheshi na nadharia ya saikochanganuzi. Utafiti umebaini kuwa kuna uhalisi fulani katika baadhi ya matendo na kauli za mhusika mlevi. Ingawa mlevi mara nyingi hasikilizwi, lakini ni mtu anayeeleza yale ambayo mhusika mwingine wa kawaida hawezi kuyaeleza. Hii ni kwa sababu watu wengi humuona mlevi kama mtu aliyepoteza urazini na hivyo huongea tu kama mwendawazimu, kwa minajili hiyo wengi wanampuuza lakini kwa hakika ni mtu anayeakisi uhalisi wa jamii yake bila woga. Utafiti huu umependekeza kuwa, ijapokuwa mlevi huonekana kama mwendawazimu, hata hivyo anapaswa kusikilizwa na asipuuzwe asilani. Mwisho utafiti umependekeza maeneo mengine yanayostahili kufanyiwa utafiti zaidi: matumizi ya mhusika mlevi yatafitiwe katika riwaya, ushairi na fasihi simulizi ili kubaini dhima yake katika fasihi.

Description

Available in print form

Keywords

Swahili literature, Lina ubani, Mabepari wa bongo

Citation

Mlelwa, L. (2012). Dhima ya mhusika mlevi na muakiso wa uhalisi wa kauli zake: mifano kutoka lina ubani na mabepari wa bongo. Master dissertation, University of Dar es Salaam. Available at (http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/search.aspx)