Masters Dissertations
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing Masters Dissertations by Subject ", Language policy"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Matatizo katika utekelezaji wa sera ya lugha Tanzania(University of Dar es Slaam, 2011) Mbiling’i, Nelly EzekielUtafiti huu unahusu Matatizo katika Utekelezaji wa Sera ya Lugha Tanzania. Lengo la utafiti huu ni kubainisha matatizo ya msingi yanayosababisha tamko la Kiswahili kutumika kufundishia katika elimu ya sekondari na elimu ya juu lisitekelezwe. Pia utafiti huu una lengo la kubainisha athari zitokanazo na kutotekelezwa kwa tamko hilo na kueleza nini kifanyike ili Kiswahili kitumike kufundishia katika elimu ya sekondari na elimu ya juu Tanzania. Mbinu zilizotumika katika utafiti huu ni pamoja na hojaji, mahojiano na maandiko. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha matatizo ya msingi katika utekelezaji wa sera ya lugha hususani katika tamko linalokitaka Kiswahili kutumika katika kufundishia elimu ya sekondari na elimu ya juu. Matatizo hayo ya msingi yanahusu: Sera ya lugha inayotumika haiko wazi. Viongozi na wanasiasa hawatoi tamko la kutaka kutumia Kiswahili katika elimu. Kasumba ya Watanzania wengi kufikiri kwamba Kiingereza kinafaa zaidi kutumika katika elimu kuliko Kiswahili. Utafiti huu pia umebaini kwamba, hali hii ya kutotumia Kiswahili katika elimu imedumaza maendeleo ya ukuzaji wa lugha ya Kiswahili Tanzania na kuathiri maendeleo ya wajifunzaji kielimu. Kukuza lugha yoyote ile ni lazima lugha hiyo iwe inatumika katika nyanja zote za kimawasiliano. Kutumia Kiswahili katika elimu kutasaidia kuleta maendeleo kwa jamii kwani jamii itapata wataalamu wenye ujuzi wa kutosha katika kila nyanja ambao watasaidia kuinua uchumi wa nchi. Utafiti huu unapendekeza kwamba, kwanza, Katiba ya nchi itamke kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa la Tanzania ili kusaidia matamko ya sera ya lugha yaweze kutekelezwa. Pili, wataalamu wa Kiswahili na wa masomo mbalimbali waandike vitabu vya kiada na ziada vya masomo yote kwa lugha ya Kiswahili na vitabu hivyo vya kiada vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza vitafsiriwe katika lugha ya Kiswahili ili wajifunzaji waweze kuelewa maarifa yaliyomo katika vitabu hivyo. Tatu, lugha za kigeni zifundishwe vizuri ili ziwawezeshe Watanzania wengi kupata maarifa ya elimu yaliyoandikwa kwa lugha hizo za kigeni. Nne, sera ya lugha ijitegemee isiwe ndani ya sera ya utamaduni ya mwaka 1997. Hii itaiwezesha sera ya lugha kutamka masuala mengi yanayohusu lugha kwa ujumla na namna yatakavyotekelezwa.