Browsing by Author "Sosoo, Felix Kwame"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Ulinganishi wa mwanamke mwanamapinduzi katika tamthilia za kiswahili za nguzo mama (1982) na ngoma ya ng’wanamalundi (1988)(University of Dar es Salaam, 2014) Sosoo, Felix KwameLengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza nafasi ya mwanamke mwanamapinduzi katika tamthilia za Nguzo Mama (1982) na Ngoma ya Ng’wanamanalundi (1988). Malengo mahususi yalikuwa matatu nayo ni kuchunguza jinsi waandishi wa tamthilia za Nguzo Mama (1982) na Ngoma ya Ng’wanamalundi (1988) walivyomsawiri mwanamke mwanamapinduzi; kubainisha tofauti zinazojitokeza kumhusu mhusika mwanamke mwanamapinduzi kati ya waandishi wawili tofauti na pia kuainisha sababu za kijamii na kiujumi zinazowafanya waandishi wa kazi teule kumsawiri mwanamke mwanamapinduzi kwa jinsi walivyomsawiri. Nadharia ya Ufeministi hasa wa Afrika ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data ya tasnifu hii. Mbinu za ukusanyaji wa data maktabani kwa kusoma maandiko na machapisho mbalimbali kwenye magazeti, majarida, vitabu vinavyohusu mada husika, makala na pia mtandao ndizo zilizotumika katika utafiti huu. Tasnifu mbalimbali za mwanzo zilizozumgumzia usawiri wa mwanamke kwa namna mbalimbali pia zilitumika kupata taarifa, hasa kuhusu mwanamke. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba waandishi wamemsawiri mwanamke kama mwanamapinduzi wa kifikra na kiitikadi kupitia elimu, matabaka, utamaduni na haki za wanawake na watoto. Vilevile utafiti huu umebaini kwamba ingawa waandishi wote wanatumia dhamira zinazofanana, wanatofautiana katika usawiri wa wahusika hasa mitazamo yao kuhusu nani anayestahili kuleta maendeleo ya kweli katika jamii. Mbogo ambaye ni mwandishi mwanaume (1988) anamsawiri mwanamke kama mwanamapinduzi lakini katika hali ya kumbeza; tofauti na Muhando (1982) ambaye ni mwandishi mwanamke, anamsawiri mwanamke mwanamapinduzi kama mdadisi wa mambo ambaye safari yake ya ukombozi inaanza kwa mchakato wa kujifunza kutokana na ugumu wa maisha anayopitia katika mfumo dume. Hali kadhalika, utafiti huu umebaini kwamba Mbogo anatumia mfumo dume kama sababu za kijamii katika kumsawiri mwanamke mwanamapinduzi. Katika kufanya hivi, anamchora mwanamume kuwa mtu wa kwanza kupata utambuzi na baadaye kumjuza mwanamke. Hii ni tofauti na Muhando ambaye anaonekana kujaribu kuupinga mfumo dume na kusawiri usawa wa kijinsia, akionesha kuwa hakuna mfumo bora kuliko mwingine. Anasisitiza kuanzishwa kwa usawa wa kijinsi na kijinsia.Item Ushujaa katika motifu ya safari ya msako: ulinganishi wa ngano za kiewe kutoka ghana na riwaya za Shaaban robert kutoka Tanzania.(University of Dar es Salaam, 2018) Sosoo, Felix KwameUtafiti huu ulihusu ushujaa katika motifu ya safari ya msako ulinganishi ukiwa katika ngano za Kiewe kutoka Ghana na riwaya teule za Shaaban Robert kutoka Tanzania. Tulifanya utafiti kutokana na mgongano wa kinadharia ambapo kuna wataalamu wa fasihi wanaoona kuwa, kwa vile kila jamii ina utamaduni wake, kazi zao za fasihi hutofautiana na wengine wanaoona kuwa jamii zenye mfanano mkubwa wa kiutamaduni huweza kuwa na kazi za fasihi zinazofanana. Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza na kulinganisha ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako kwenye ngano za Kiewe na riwaya teule za Shaaban Robert. Aidha, utafiti huu ulikuwa na malengo mahususi manne ambayo ni: Kubainisha ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako katika ngano za Kiewe na riwaya teule za Shaaban Robert; kueleza kufanana na kutofautiana kwa ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako kwenye ngano za Kiewe na riwaya teule za Shaaban Robert; kufafanua jinsi ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako unavyobainisha utamaduni na falsafa ya Kiafrika katika ngano za Kiewe na riwaya teule za Shaaban Robert; na kubainisha dhima ya ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako kwenye ngano za Kiewe na riwaza teule za Shaaban Robert katika maendeleo ya fasihi. Ili kuweza kutimiza malengo hayo, data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za aina mbili, ambazo ni majadiliano/mahojiano ya vikundi na udurusu matini. Mkabala wa uchambuzi uliotumika ni ule wa kitaamuli. Aidha, uchambuzi huo ulifanywa kwa kutumia ruwaza ya shujaa, nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika na nadharia ya Mwingilianomatini. Kuhusu matokeo ya utafiti, imebainika kuwa ngano za Kiewe na riwaya teule kwa kiasi kikubwa zimesheheni ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako. Aidha, imebainika kuwa, kuna mfanano mkubwa baina ya ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako katika ngano za Kiewe na riwaya teule. Pia, utafiti huu umebaini kuwa ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako katika tanzu husika unabainisha utamaduni na falsafa ya Kiafrika. Mwisho, utafiti huu umebainisha dhima ya ushujaa unaosawiriwa katika motifu ya safari ya msako kwenye ngano za Kiewe na riwaza teule za Shaaban Robert katika maendeleo ya fasihi teule. Mbali na kufafanua masuala hayo, bado utafiti wa kina unahitajika katika maeneo mbalimbali. Kwanza, kuna haja ya kufanya utafiti utakaohusisha ngano nyingi zaidi na riwaya nyingine zaidi ya zilizotumika katika utafiti huu. Pia, utafiti zaidi utakaohusisha tanzu nyingi zaidi unahitajika ili kutoa mahitimisho ya kimajumui.