Ulinganishi wa mwanamke mwanamapinduzi katika tamthilia za kiswahili za nguzo mama (1982) na ngoma ya ng’wanamalundi (1988)

No Thumbnail Available
Date
2014
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza nafasi ya mwanamke mwanamapinduzi katika tamthilia za Nguzo Mama (1982) na Ngoma ya Ng’wanamanalundi (1988). Malengo mahususi yalikuwa matatu nayo ni kuchunguza jinsi waandishi wa tamthilia za Nguzo Mama (1982) na Ngoma ya Ng’wanamalundi (1988) walivyomsawiri mwanamke mwanamapinduzi; kubainisha tofauti zinazojitokeza kumhusu mhusika mwanamke mwanamapinduzi kati ya waandishi wawili tofauti na pia kuainisha sababu za kijamii na kiujumi zinazowafanya waandishi wa kazi teule kumsawiri mwanamke mwanamapinduzi kwa jinsi walivyomsawiri. Nadharia ya Ufeministi hasa wa Afrika ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data ya tasnifu hii. Mbinu za ukusanyaji wa data maktabani kwa kusoma maandiko na machapisho mbalimbali kwenye magazeti, majarida, vitabu vinavyohusu mada husika, makala na pia mtandao ndizo zilizotumika katika utafiti huu. Tasnifu mbalimbali za mwanzo zilizozumgumzia usawiri wa mwanamke kwa namna mbalimbali pia zilitumika kupata taarifa, hasa kuhusu mwanamke. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba waandishi wamemsawiri mwanamke kama mwanamapinduzi wa kifikra na kiitikadi kupitia elimu, matabaka, utamaduni na haki za wanawake na watoto. Vilevile utafiti huu umebaini kwamba ingawa waandishi wote wanatumia dhamira zinazofanana, wanatofautiana katika usawiri wa wahusika hasa mitazamo yao kuhusu nani anayestahili kuleta maendeleo ya kweli katika jamii. Mbogo ambaye ni mwandishi mwanaume (1988) anamsawiri mwanamke kama mwanamapinduzi lakini katika hali ya kumbeza; tofauti na Muhando (1982) ambaye ni mwandishi mwanamke, anamsawiri mwanamke mwanamapinduzi kama mdadisi wa mambo ambaye safari yake ya ukombozi inaanza kwa mchakato wa kujifunza kutokana na ugumu wa maisha anayopitia katika mfumo dume. Hali kadhalika, utafiti huu umebaini kwamba Mbogo anatumia mfumo dume kama sababu za kijamii katika kumsawiri mwanamke mwanamapinduzi. Katika kufanya hivi, anamchora mwanamume kuwa mtu wa kwanza kupata utambuzi na baadaye kumjuza mwanamke. Hii ni tofauti na Muhando ambaye anaonekana kujaribu kuupinga mfumo dume na kusawiri usawa wa kijinsia, akionesha kuwa hakuna mfumo bora kuliko mwingine. Anasisitiza kuanzishwa kwa usawa wa kijinsi na kijinsia.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8704.S67)
Keywords
Swahili literature, Swahili fiction, Women in Literature, Nguzo mama, Ngoma ya Ng'wanamalundi
Citation
Sosoo, F. K (2014) Ulinganishi wa mwanamke mwanamapinduzi katika tamthilia za kiswahili za nguzo mama (1982) na ngoma ya ng’wanamalundi (1988), Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.