Browsing by Author "Kawonga, Gervas"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Nafasi ya lugha ya kiswahili katika mandhari- lugha ya jiji la Mbeya nchini Tanzania(University of Dar es salaam, 2020) Kawonga, GervasUtafiti huu ulihusu nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Lengo kuu lilikuwa kuchunguza nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Malengo mahususi yalikuwa matatu: kwanza, kubainisha ruwaza za lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Pili, kudhihirisha nafasi ya lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia ruwaza za lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Tatu, kuwianisha sera ya lugha ya Tanzania na nafasi ya lugha kwenye mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Ubeberu wa Kiisimu yenye msingi kwamba katika jamii kuna vipengele vya kimfumo na kiitikadi vinavyosababisha uhusiano usio wa usawa miongoni mwa lugha za jamii mbalimbali. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya upigaji wa picha za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu na mbinu ya usaili. Uchambuzi wa data za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu ulifanyika kwa mbinu ya usomaji wa matini na Programu Tarakilishi ya Takwimu (PTT). Uwasilishaji wa data umefanyika kwa kutumia vielelezo vya majedwali, grafu na picha kwa data za kiidadi za mabango ya makampuni ya mawasiliano ya simu. Nukuu za usaili na ufafanuzi wa kinathari umetumika kwa data za kitaamuli. Matokeo yanaonesha kwamba kuna ruwaza nne za lugha katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Ruwaza zilizobainishwa ni Kiswahili pekee, Kiingereza pekee, Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili. Kiswahili kinajitokeza kwa asilimia 54.5 katika ruwaza ya Kiswahili pekee mbele ya Kiingereza. Kwa kigezo cha ukubwa wa maandishi Kiswahili kinajitokeza cha kwanza kwa asilimia 63 kwa maandishi makubwa zaidi kuliko Kiingereza. Vilevile, kwa kigezo cha idadi ya maneno Kiswahili kinajitokeza katika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 72.23. Kwa hiyo, Kiswahili kinajitokeza katika nafasi ya kwanza kimatumizi katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya nchini Tanzania. Aidha, kuna uwiano baina ya Sera ya Lugha ya Tanzania na nafasi ya matumizi ya lugha katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya. Hata hivyo, tunapendekeza serikali ifanye mapitio ya sera ya lugha ili kuunda kanuni za matumizi ya lugha katika mandhari-lugha na kuweka urari wa matumizi ya lugha katika mandhari-lugha. Vilevile, tafiti fuatishi zifanyike kwa kuchunguza mabango ya makampuni mahususi tofautitofauti ili kupanua uelewa kuhusu ruwaza za lugha, nafasi ya Kiswahili na uwiano wa nafasi ya matumizi ya lugha na Sera ya lugha ya Tanzania.Item Ulinganishi wa kiisimu wa lugha ya Samatengo na ya Kindendeule(University of Dar es Salaam, 2013) Kawonga, GervasMadai kwamba lugha ya Samatengo na ya Kindendeule zinafanana yamekuwapo kwa muda mrefu miongoni mwa wanaisimu, wachunguzi na wazungumzaji wa Samatengo na Kindendeule. Utafiti huu ulihusu Ulinganishi wa Kiisimu wa Lugha ya Samatengo na ya Kindendeule. Tatizo la utafiti lilikuwa ni kutafuta data za kiisimu kutoka uwandani ili kuhakiki madai kwamba lugha ya Samatengo na ya Kindendeule zinafanana. Lengo kuu lilikuwa kuonesha ni kwa kiwango gani Samatengo na Kindendeule zinafanana kiisimu ili kufahamu hadhi ya kila moja katika muktadha wa uhususiano wake. Kulikuwa na malengo mahususi matatu. Moja, kuweka vigezo vya kubainisha msingi wa kufanana kwa Samatengo na Kindendeule. Pili, kueleza mwelekeo unaotokana na kufanana kwa vigezo vilivyowekwa. Tatu, kuthibitisha kama hizi ni lugha mbili tofauti au ni lahaja za lugha moja. Data kwa ajili ya utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia njia tatu ambazo ni maandishi maktabani, hojaji na majadiliano ya vikundilengwa. Mbinu za uchambuzi wa data zilizotumika ni mbinu ya takwimuleksika, mbinu linganishi, na mbinu ya maelezo, ambazo zilikuwa zikikamilishana. Matokeo kwa jumla yamesaidia kujibu maswali ya utafiti na kufikia malengo yaliyowekwa. Lengo la kwanza na swali la kwanza lilihusu vigezo vya kubainisha kufanana kwa Samatengo na Kindendeule. Vigezo viwili vilitumika ambavyo ni msamiati wa msingi na ukubaliano wa sauti. Lengo la pili na swali la pili lilihusu mwelekeo unaotokana na kiwango cha kufanana kwa vigezo vilivyowekwa; imewekwa wazi kwamba mwelekeo ni wa uhusiano wa karibu zaidi kiasi cha kuhitimisha kuwa ni lahaja za lugha moja ya azali. Lengo la tatu na swali la tatu lilihusu kuthibitisha kama hizo ni lugha mbili au ni lahaja za lugha moja. Imethibitishwa kwa vigezo vya kiisimu kuwa Samatengo na Kindendeule ni lahaja za lugha moja. Utafiti unaonesha kwamba Samatengo na Kindendeule zinafanana kwenye kigezo cha msamiati wa msingi kwa 87%. Pia zinafanana katika kigezo cha fonimu za konsonanti kwa asilimia 75% na katika kigezo cha fonimu za irabu kwa 100%. Fasili ya viwango hivyo vya asilimia za kufanana ni kwamba Samatengo na Kindendeule ni lahaja za lugha moja ya azali. Inapendekezwa kwanza, kwa kuwa utafiti huu ulihusu ulinganishi wa Samatengo na Kindendeule, ufanyike utafiti mwingine katika kulinganisha lugha nyingine zinazodaiwa kufanana ili kuweka wazi kiwango cha uhusiano kilichopo baina ya lugha hizo kwa ajili ya kupanua maarifa ya isimu. Pili, inapendekezwa ufanyike utafiti mwingine utakaosaidia kubaini lugha azali kwayo Samatengo na Kindendeule zilitokana nayo. Tatu, utafiti huu ulilinganisha vipengele viwili vya kiisimu yaani msamiati wa msingi na ukubaliano wa sauti. Hivyo ufanyike utafiti mwingine kwa kutumia vigezo vya sintaksia, mofololojia na semantiki ili kubaini kiwango cha kufanana baina ya Samatengo na Kindendeule katika vipengele hivyo. Nne, ufanyike pia utafiti mwingine ili kubaini athari za kihistoria na kiisimujamii katika lahaja za Samatengo na Kindendeule.