Ulinganishi wa kiisimu wa lugha ya Samatengo na ya Kindendeule

No Thumbnail Available
Date
2013
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Madai kwamba lugha ya Samatengo na ya Kindendeule zinafanana yamekuwapo kwa muda mrefu miongoni mwa wanaisimu, wachunguzi na wazungumzaji wa Samatengo na Kindendeule. Utafiti huu ulihusu Ulinganishi wa Kiisimu wa Lugha ya Samatengo na ya Kindendeule. Tatizo la utafiti lilikuwa ni kutafuta data za kiisimu kutoka uwandani ili kuhakiki madai kwamba lugha ya Samatengo na ya Kindendeule zinafanana. Lengo kuu lilikuwa kuonesha ni kwa kiwango gani Samatengo na Kindendeule zinafanana kiisimu ili kufahamu hadhi ya kila moja katika muktadha wa uhususiano wake. Kulikuwa na malengo mahususi matatu. Moja, kuweka vigezo vya kubainisha msingi wa kufanana kwa Samatengo na Kindendeule. Pili, kueleza mwelekeo unaotokana na kufanana kwa vigezo vilivyowekwa. Tatu, kuthibitisha kama hizi ni lugha mbili tofauti au ni lahaja za lugha moja. Data kwa ajili ya utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia njia tatu ambazo ni maandishi maktabani, hojaji na majadiliano ya vikundilengwa. Mbinu za uchambuzi wa data zilizotumika ni mbinu ya takwimuleksika, mbinu linganishi, na mbinu ya maelezo, ambazo zilikuwa zikikamilishana. Matokeo kwa jumla yamesaidia kujibu maswali ya utafiti na kufikia malengo yaliyowekwa. Lengo la kwanza na swali la kwanza lilihusu vigezo vya kubainisha kufanana kwa Samatengo na Kindendeule. Vigezo viwili vilitumika ambavyo ni msamiati wa msingi na ukubaliano wa sauti. Lengo la pili na swali la pili lilihusu mwelekeo unaotokana na kiwango cha kufanana kwa vigezo vilivyowekwa; imewekwa wazi kwamba mwelekeo ni wa uhusiano wa karibu zaidi kiasi cha kuhitimisha kuwa ni lahaja za lugha moja ya azali. Lengo la tatu na swali la tatu lilihusu kuthibitisha kama hizo ni lugha mbili au ni lahaja za lugha moja. Imethibitishwa kwa vigezo vya kiisimu kuwa Samatengo na Kindendeule ni lahaja za lugha moja. Utafiti unaonesha kwamba Samatengo na Kindendeule zinafanana kwenye kigezo cha msamiati wa msingi kwa 87%. Pia zinafanana katika kigezo cha fonimu za konsonanti kwa asilimia 75% na katika kigezo cha fonimu za irabu kwa 100%. Fasili ya viwango hivyo vya asilimia za kufanana ni kwamba Samatengo na Kindendeule ni lahaja za lugha moja ya azali. Inapendekezwa kwanza, kwa kuwa utafiti huu ulihusu ulinganishi wa Samatengo na Kindendeule, ufanyike utafiti mwingine katika kulinganisha lugha nyingine zinazodaiwa kufanana ili kuweka wazi kiwango cha uhusiano kilichopo baina ya lugha hizo kwa ajili ya kupanua maarifa ya isimu. Pili, inapendekezwa ufanyike utafiti mwingine utakaosaidia kubaini lugha azali kwayo Samatengo na Kindendeule zilitokana nayo. Tatu, utafiti huu ulilinganisha vipengele viwili vya kiisimu yaani msamiati wa msingi na ukubaliano wa sauti. Hivyo ufanyike utafiti mwingine kwa kutumia vigezo vya sintaksia, mofololojia na semantiki ili kubaini kiwango cha kufanana baina ya Samatengo na Kindendeule katika vipengele hivyo. Nne, ufanyike pia utafiti mwingine ili kubaini athari za kihistoria na kiisimujamii katika lahaja za Samatengo na Kindendeule.
Description
Available in print form
Keywords
Bantu languages, Matengo language, Ndendeuli language, Languages, Tanzania
Citation
Kawonga, G (2013) Ulinganishi wa kiisimu wa lugha ya Samatengo na ya Kindendeule, Tasinifu ya M.A (Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Kinapatikana http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)