Browsing by Author "Gawasike, Arnold"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Mfuatano wa mofimu nyambulishi katika vitenzi vya Kikinga(University of Dar es Salaam, 2011) Gawasike, ArnoldSuala la unyambulishaji na mfuatano wa mofimu nyambulishi limewavuta wataalamu wengi. Hata hivyo, hakuna utafiti ambao umefanyika katika lugha ya Kikinga. Kwa hiyo utafiti huu ulikuwa jaribio la kuchunguza unyambulishaji wa vitenzi katika lugha hii na kubainisha kanuni za mfuatano wa mofimu nyambulishi hizo. Aidha, utafiti umechunguza unyambulishi wa aina tano. Utafiti umefanyika katika kata za: Mbalatse, Ipepo na Ukwama, wilaya ya Makete mkoa wa Iringa, Tanzania. Ili kufanikisha kazi hii, Kanuni Tazamishi (KAT) iliongoza utafiti huu, yaani unyambulishaji wa vitenzi kimofolojia unaakisi unyambulishaji wa vitenzi kisintaksia. Mbinu za utafiti zilihusu: usampulishaji, ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Data ya utafiti ni ya kutoka uwandani ambapo vitenzi viliteuliwa na kuwekwa katika kategoria mbili; vitenzi visoukomo katika kundi moja na vitenzi vya silabi moja katika kundi jingine. Kazi imegawanyika katika sura tano. Sura ya kwanza, imeeleza kiini cha utafiti na utaratibu uliozingatiwa katika kufanikisha utafiti. Sura ya pili, imeshughulikia mapitio ya maandiko kuhusiana na unyambulishaji na mfuatano wa mofimu katika lugha. Mapitio haya yamebainisha kuwa minyambuliko na mifuatano ya mofimu katika lugha ipo. Sura ya tatu, imehusu mbinu za utafiti ambapo populesheni, sampuli, usampulishaji pamoja na njia tatu za ukusanyaji data zilibainishwa. Sura ya nne, imeshughulikia uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Kwa ujumla data, iliyopatikana imechanganuliwa kwa njia ya maelezo na kanuni. Kanuni Tazamishi ya Baker (1985) ndiyo iliyoongozo mjadala na uchanganuzi wa data hii. Sura ya tano imeshughulikia matokeo, hitimisho, na tafiti fuatishi. Matokeo ya utafiti yamebainisha minyambuliko mitano na kwamba, lugha ya Kikinga inapangilia mofimu nyambulishi zake kwa mujibu wa Kanuni Tazamishi inayodai unyambulishaji kimofolojia huakisi unyambulishaji sintaksia. Aidha, kanuni ya uukiliwaji iliyoundwa ina tenda kazi pia, katika mfuatano wa mofimu nyambulishi katika lugha ya Kikinga, yaani mofimu moja ikitangulia ina kawaida ya kuukilia mofimu ambazo zinaweza kuifuata na ama kutoifuata yenyewe.Item Ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya kiswahili katika jamii ya wakinga(University of Dar es Salaam, 2016) Gawasike, ArnoldUchunguzi kuhusu ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya pili (kuanzia sasa L2) kumeongezeka katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, chanzo cha ukakamaaji huo bado hakijabainishwa japo kuwa uhawilishaji wa lugha ya kwanza (kuanzia sasa L1) katika kujipatia L2 kuna tajwa sana. Utafiti, huu umeshughulikia suala la ukakamaaji kwa wajifunzaji wa L2 katika jamii ya Wakinga kata za Mbalatse, Ipepo na Lupila. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Usasanyuzi Linganishi (kuanzia sasa NULI) ya Lado (1967). Nadharia hii, inachunguza kufanana, na kutofautiana kwa L1 na L2 ili kuboresha ufundishaji wa L2 na Nadhariatete Teuzi ya Ukakamaaji (kuanzia sasa NATEU) ya Han (2009). Nadhariatete hii inaona kuwa katika kujipatia L2 kuna vipengele fulani vya L2 vina satua ya kukakamaa kuliko vingine kutokana na tofauti kati ya L1 na L2. Data za utafiti huu zilikusanywa kwa njia nne ambazo ni: kuandika insha, kujaza hojaji, mahojiano na ushuhudiaji. Data za insha na hojaji zilikuwa katika mfumo wa kongoo-andishi, wakati data za mahojiano na ushuhudiaji zilikuwa katika mfumo wa kongoo-uneni. Data zilichambuliwa kwa kutumia programu ya Statistical Package for Social Sciences (SPSS) na kutolewa maelezo, vielelezo, majedwali na grafu. Pia, zilichambuliwa kwa njia ya kusoma insha za wajifunzaji L2 na kubainisha vipengele mbalimbali vyenye dosari. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, wajifunzaji wa L2 katika jamii ya Wakinga wamekakamaa. Chanzo kikuu cha ukakamaaji huo ni kutokuwapo kwa mwingiliano kati ya jamii-lugha ya Wakinga na jamii-lugha nyingine. Hii ni tofauti na tafiti tangulizi zilizoonesha kuwa, chanzo kikuu cha ukakamaaji ni uhawilishaji wa L1 katika L2. Pia, tofauti za kifonolojia kati ya lugha ya Kiswahili na Kikinga husababisha ukakamaaji kwa matamshi. Vilevile, kuchelewa kuanza kujipatia lugha ya Kiswahili na muda mwingi kutumia lugha ya Kikinga husababisha hali ya ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili katika jamii hii. Utafiti huu umebaini kuwa, msamiati wenye satua ya kukakamaa ni ule unaohusisha fonimu zifuatazo: /r/, /ð/, /ɵ/, /ɤ/, /č/, /ŋ/ na silabi mwambatano. Ili kuondokana na tatizo la ukakamaaji, utafiti umependekeza kuboresha miundombinu ili kuruhusu mwingiliano na jamii-lugha nyingine. Kadhalika, kuimarisha elimu ya awali, kuhamasisha matumizi mapana ya Kiswahili kumezingatiwa pamoja na kupanua mwingiliano baina ya Wakinga na jamii zingine. Mapendekezo ya tafiti fuatizi: mosi, utafiti mwingine ufanywe ili kuchunguza athari za lugha ya Kiswahili katika Kikinga. Pili, utafiti huu ulifanyika vijijini mwa wilaya ya Makete; utafiti mwingine kama huu unaweza kufanywa mjini Makete ili kubaini kinachojiri huko. Tatu, utafiti mwingine wenye welekeo wa kielimu unaweza kufanywa ili kuchunguza mbinu wanazotumia walimu kufundisha lugha ya Kiswahili, na pia mbinu watumiazo wanafunzi katika kujifunza lugha hii.