Ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya kiswahili katika jamii ya wakinga
Loading...
Date
2016
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Uchunguzi kuhusu ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya pili (kuanzia sasa L2) kumeongezeka katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, chanzo cha ukakamaaji huo bado hakijabainishwa japo kuwa uhawilishaji wa lugha ya kwanza (kuanzia sasa L1) katika kujipatia L2 kuna tajwa sana. Utafiti, huu umeshughulikia suala la ukakamaaji kwa wajifunzaji wa L2 katika jamii ya Wakinga kata za Mbalatse, Ipepo na Lupila. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Usasanyuzi Linganishi (kuanzia sasa NULI) ya Lado (1967). Nadharia hii, inachunguza kufanana, na kutofautiana kwa L1 na L2 ili kuboresha ufundishaji wa L2 na Nadhariatete Teuzi ya Ukakamaaji (kuanzia sasa NATEU) ya Han (2009). Nadhariatete hii inaona kuwa katika kujipatia L2 kuna vipengele fulani vya L2 vina satua ya kukakamaa kuliko vingine kutokana na tofauti kati ya L1 na L2. Data za utafiti huu zilikusanywa kwa njia nne ambazo ni: kuandika insha, kujaza hojaji, mahojiano na ushuhudiaji. Data za insha na hojaji zilikuwa katika mfumo wa kongoo-andishi, wakati data za mahojiano na ushuhudiaji zilikuwa katika mfumo wa kongoo-uneni. Data zilichambuliwa kwa kutumia programu ya Statistical Package for Social Sciences (SPSS) na kutolewa maelezo, vielelezo, majedwali na grafu. Pia, zilichambuliwa kwa njia ya kusoma insha za wajifunzaji L2 na kubainisha vipengele mbalimbali vyenye dosari. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, wajifunzaji wa L2 katika jamii ya Wakinga wamekakamaa. Chanzo kikuu cha ukakamaaji huo ni kutokuwapo kwa mwingiliano kati ya jamii-lugha ya Wakinga na jamii-lugha nyingine. Hii ni tofauti na tafiti tangulizi zilizoonesha kuwa, chanzo kikuu cha ukakamaaji ni uhawilishaji wa L1 katika L2. Pia, tofauti za kifonolojia kati ya lugha ya Kiswahili na Kikinga husababisha ukakamaaji kwa matamshi. Vilevile, kuchelewa kuanza kujipatia lugha ya Kiswahili na muda mwingi kutumia lugha ya Kikinga husababisha hali ya ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili katika jamii hii. Utafiti huu umebaini kuwa, msamiati wenye satua ya kukakamaa ni ule unaohusisha fonimu zifuatazo: /r/, /ð/, /ɵ/, /ɤ/, /č/, /ŋ/ na silabi mwambatano. Ili kuondokana na tatizo la ukakamaaji, utafiti umependekeza kuboresha miundombinu ili kuruhusu mwingiliano na jamii-lugha nyingine. Kadhalika, kuimarisha elimu ya awali, kuhamasisha matumizi mapana ya Kiswahili kumezingatiwa pamoja na kupanua mwingiliano baina ya Wakinga na jamii zingine. Mapendekezo ya tafiti fuatizi: mosi, utafiti mwingine ufanywe ili kuchunguza athari za lugha ya Kiswahili katika Kikinga. Pili, utafiti huu ulifanyika vijijini mwa wilaya ya Makete; utafiti mwingine kama huu unaweza kufanywa mjini Makete ili kubaini kinachojiri huko. Tatu, utafiti mwingine wenye welekeo wa kielimu unaweza kufanywa ili kuchunguza mbinu wanazotumia walimu kufundisha lugha ya Kiswahili, na pia mbinu watumiazo wanafunzi katika kujifunza lugha hii.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8703.5.M3254)
Keywords
Swahili literature, History and criticism
Citation
Gawasike, A. (2016) Ukakamaaji kwa wajifunzaji wa lugha ya kiswahili katika jamii ya wakinga, Tasnifu ya uzamivu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam