Michakato ya kifonolojia katika lugha ya Kiw’oso

Date

2013

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu unazungumzia fonolojia ya Kiw’oso, hususani michakato ya kifonolojia na athari zake katika sauti za lugha hiyo. Ama kwa hakika hiki ni kipengele ambacho kimeshughulikiwa katika lugha nyingi za Kibantu isipokuwa lugha ya Kiw’oso. Katika kulishughulikia suala hili, kazi hii imegawika katika sura nne. Sura ya kwanza inatoa maelezo mafupi kuhusu lugha ya Kiw’oso, tatizo la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti na mawanda ya utafiti. Aidha, inatoa maelezo mafupi juu ya kiunzi cha nadharia, ambapo imetumika nadharia ya Umbo Upeo iliyoasisiwa na Alan Prince na Paul Smolensky (1993). Halikadhalika inaeleza mbinu zilizotumika katika utafiti na sampuli iliyotumika. Data zilikusanywa katika vijiji vya Uri na Omarini vilivyoko wilaya ya Moshi Vijijini, mkoa wa Kilimanjaro. Data hizo zilikusanywa kwa kutumia kinasasauti aina ya MP3 IC Recorder na kufanyiwa unukuzi kwa ajili ya uchanganuzi. Sura ya pili inaeleza mambo ya msingi yanayojitokeza katika lugha hiyo. Mambo hayo ni pamoja na mfumo wa sauti, yaani irabu na konsonanti na muundo wa silabi. Halikadhalika inaelezea kwa ufupi mfumo wa mofolojia ya nomino na vitenzi. Sura ya tatu inabainisha mashartizuizi yanayopatikana katika Kiw’oso. Aidha, inajadili michakato ya kifonolojia inayoathiri irabu na konsonanti, ambapo imebainika kuwa michakato inayoathiri irabu ni mingi kuliko ile inayoathiri konsonanti katika lugha hii. Sura ya nne inatoa majumuisho na muhtasari wa utafiti mzima. Inajibu maswali ya utafiti ikiwa ni pamoja na kutoa hitimisho, maoni na mapendekezo kuhusu utafiti utakaofuata katika lugha hii hapo baadaye.

Description

Available in print form

Keywords

Chagga language, W'oso language, Phonology

Citation

Habibu, M (2013) Michakato ya kifonolojia katika lugha ya Kiw’oso, Tasnifu ya M.A. (Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Kinapatikana http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)