Uchunguzi wa semantiki na taratibu za utoaji wa majina ya kijita

Date

2013

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu unachunguza Semantiki na Taratibu za utoaji wa majina ya Kijita. Utafiti ulifanyika katika Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma Mjini; katika kata za Buhare, Makoko, Mwigobelo Kigera na Nyamatare. Jumla ya watafitiwa 60 walihusishwa katika utafiti huu. Watafitiwa hao walichaguliwa kwa kutumia sampuli nasibu tabakishi. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia mbinu za hojaji, mahojiano na maktabani. Data ilichambuliwa kwa kutumia mkabala wa maelezo. Nadharia ya tendo uneni ya Austin (1962) na nadharia jumuishi ya Uumbaji ya Sapir na Whorf (1958) zilitumika kuongoza utafiti huu. Utafiti huu umebaini kuwa majina ya Kijita hayatolewi kiholela bali yanafuata taratibu mbalimbali zilizofumbata falsafa, mila na desturi za Kijita. Utafiti umebaini kuwa maana za majina mengi ya Kijita zimekitwa katika kazi, matukio, vyakula, vitoweo na unasibishi wa majina ya wanyama. Vilevile utafiti umebaini kuwa sababu zinazoukilia majina ya Kijita zimefungamana sana na maana za majina hayo. Kwa mfano, jina Bulenga (me) lina maana ya mvivu. Sababu iliyochochea mtu huyu kuitwa jina hili ni tabia ya uvivu aliokuwa nao mtu mwenye jina hili au mmojawapo wa wazazi wake. Halikadhalika, utafiti umebaini kuwa majina ya Kijita yanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utoaji na matumizi yake katika jamii. Aidha, utafiti umebaini kuwa changamoto zinazokabili majina ya Kijita zinaweza kukabiliwa kwa pamoja kijamii kwa kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutumia majina ya asili, kufahamu maana na sababu za majina hayo pamoja na taratibu za utoaji na utumiaji wa majina hayo.

Description

Available in print form

Keywords

Jita language, Semantics

Citation

Nyangaywa, M (2013) Uchunguzi wa semantiki na taratibu za utoaji wa majina ya kijita, Tasnifu ya M.A. Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Kinapatikana http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/search.aspx)