Usawiri wa mhusika mtoto katika riwaya ya kiswahili: mifano kutoka katika riwaya za ngome ya mianzi na marimba ya majaliwa

Date

2013

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Tasinifu hii imechunguza namna mhusika mtoto anavyosawiriwa katika riwaya ya Kiswahili kwa kutumia riwaya za Ngome ya Mianzi (1990) na Marimba ya Majaliwa (2008). Tasinifu hii imejielekeza katika kuonyesha sifa zinazompambanua mhusika mtoto katika riwaya za Ngome ya Mianzi na Marimba ya Majaliwa. Pia, kubainisha dhamira zinazoibuliwa na mhusika mtoto katika riwaya za Ngome ya Mianzi na Marimba ya Majaliwa. Utafiti huu umeegemezwa katika nadharia mbili, nadharia ya uhalisiamazingaombwe na nadharia ya uhalisia. Utafiti huu umetumia mbinu ya kujisomea katika kukusanya data. Vifaa vilivyotumika katika ukusanyaji na uchakataji wa data ni shajara, kalamu, penseli, kompyuta na kinyonyi. Sampuli iliyotumika ni sampuli lengwa ambayo ni riwaya za Ngome ya Mianzi na Marimba ya Majaliwa. Uchanganuzi wa data katika utafiti huu ulifikiwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vya kumsawiri mhusika katika kazi za fasihi. Utafiti huu umeonyesha kwamba, mhusika mtoto anajipambanua kama: mfariji, askari vitani, mlezi, mtu mwenye mapenzi ya dhati kwa wazazi wake, mwelimishaji, msaguzi wa kijinsia, mtu mwenye kipaji cha usanii, mtu mwenye bidii na mwaminifu kazini, mtalii, mtetezi wa haki, mtu mwenye imani za kishirikina, mtu anayepigania uhuru wa kujitegemea na kifikra. Pia, utafiti huu umebaini dhamira mbalimbali zilizowasilishwa na mhusika mtoto kama vile: ukombozi, uzalendo, faraja, mapenzi, athari za vita, umoja na mshikamano, kifo, bidii na kuheshimu maadili ya kazi, imani katika Miungu, utii, ushirikina, dhuluma, uhuru wa kifikra na kujitegemea, na tatizo la watoto wa mitaani na athari zake.

Description

Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8703.5.M452)

Keywords

Swahili literature, Children in literature, Ngome ya Mianzi, Marimba ya Majariwa

Citation

Mgani, T. (2013) Usawiri wa mhusika mtoto katika riwaya ya kiswahili: mifano kutoka katika riwaya za ngome ya mianzi na marimba ya majaliwa, Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.