Uingizaji wa homonimu,polisemi na sinonimu katika kamusi la kiswahili fasaha(2010)

Date

2016

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu ulihusu uingizaji wa homonimu, polisemi na sinonimu katika Kamusi la Kiswahili Fasaha iliyoandikwa na BAKIZA (2010). Utafiti ulifanyika uwandani na maktabani. Maeneo yaliyohusika zaidi ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hususani katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Kwa Upande wa Zanzibar maeneo yaliyohusika ni Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na Baraza la Kiswahili la Zanzibar. Malengo hasa ya utafiti yalikuwa ni kuhakiki namna homonimu, polisemi na sinonimu zilivyoingizwa katika Kamusi la Kiswahili Fasaha, pamoja na kuchunguza uingizaji na utumikaji wa homonimu, polisemi na sinonimu hizo, namna unavyoakisi kanuni za uingizaji na upangaji wa vidahizo katika kamusi. Data za kukamilisha utafiti huu zilipatikana kupitia hojaji, mahojiano na ujisomeaji binafsi wa mtafiti. Watoa data za utafiti 67 walikuwa chanzo cha data zilizotumika. Vitomeo 24 vilichaguliwa kwa kila kundi la vitomeo vya homonimu, polisemi na sinonimu. Kwa hiyo jumla ya vitomeo ilikuwa 72. Data za utafiti zimechanganuliwa kimaelezo na kiidadi. Kazi nzima imegawanyika katika sura tano. Utafiti umebainisha kuwa uingizaji na utumiaji wa homonimu, polisemi na sinonimu, katika KAKIFA umeakisi nadharia za uingizaji na upangaji wa vitomeo katika kamusi. Matumizi ya tarakimu (misimbo) ni mbinu iliyotawala uingizaji wa fahiwati za vitomeo hivyo; yaani homonimu zimeingizwa kwa kutumia namba za mfumo wa vipeo ili kuonesha kiwima idadi na utofauti mkubwa wa fahiwati zinazotokana na vidahizo vinavyohusika. Vilevile polisemi zimetumia mfumo wa tarakimu za kawaida ili kuonesha kiulalo idadi na uhusiano wa karibu katika fahiwati zinazotokana na vidahizo vinavyohusika. Uingizaji wa sinonimu umezingatia zaidi matumizi ya alama ya sawasawa ili kuonesha visawe vinavyokifafanua zaidi kidahizo kinachohusika. Pia, utafiti umebaini kuwa kwa kiasi fulani KAKIFA imechanganya namna ya uingizaji wa vitomeo homonimu na polisemi kwa sababu baadhi yake zimepambanuliwa tofauti kiuhusiano kama ilivyo ukweli wake halisi. Yaani, baadhi ya homonimu zimeingizwa kama polisemi vilevile zipo polisemi zilizoingizwa kwenye kamusi kama ni homonimu.

Description

Available in print form, EAF collection, Dr. Wilbert Chagula Library (THS EAF PL8703.A62)

Keywords

Swahili language, homonyms, Synonyms, Dictionaries, Swahili

Citation

Andrew, Jeremiah S (2016) Uingizaji wa homonimu,polisemi na sinonimu katika kamusi la kiswahili fasaha(2010) ,Masters Dissertation,University of Dar es Salaam, Dar es Salaam.