Matumizi ya lugha ya kisukuma katika kiswahili cha mazungumzo

Date

2014

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu umechunguza matumizi ya lugha ya Kisukuma katika Kiswahili cha mazungumzo. Utafiti huu ulifanyika wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga na ulihusisha kata nne ambazo ni Mwadui/Luhumbo, Songwa, Mondo na Seke/Bugoro. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha matumizi ya matamshi ya lugha ya Kisukuma katika Kiswahili cha mazungumzo, kubainisha na kufafanua makundi ya kijamii yanayotumia mara kwa mara vipengele vya matamshi ya lugha ya Kisukuma katika Kiswahili cha mazungumzo na lengo la tatu lilikuwa kueleza kwa nini makundi hayo ya kijamii yanapendelea kutumia vipengele hivyo katika Kiswahili cha mazungumzo. Jumla ya watafitiwa 64 walihusishwa katika utafiti huu. Watafitiwa hao walichaguliwa kwa kutumia usampulishaji nasibu tabakishi kwa kuzingatia vigezo vya umri, jinsi, kazi na elimu. Mtafiti alitumia mbinu za hojaji, mahojiano na ushuhudiaji katika ukusanyaji data na kufafanuliwa kwa njia ya kimaelezo na kiidadi. Mkabala wa kinadharia wa Uchanganuzi wa Kieneo ndio ulioongoza utafiti huu ambao unachunguza nani anatumia lugha gani, anatumia na nani na kwa sababu gani. Nadharia hii imemsaidia mtafiti kujua kundi la kijamii linalotumia lugha ya Kisukuma, linazungumza na nani, pamoja na sababu za kutumia lugha hiyo katika Kiswahili sanifu. Utafiti huu umebaini kuwa baadhi ya wazungumzaji wa Kisukuma wanatumia matamshi ya Kisukuma katika Kiswahili cha mazungumzo. Makundi ya kijamii yanayotumia vipengele vya Kisukuma katika Kiswahili cha mazungumzo ni pamoja na wasiosoma shule, wazee, wakulima, wanawake, wanaume na rika la kati. Sababu za kutumia vipengele hivyo zinatokana na kuathiriwa na lugha ya kwanza. Mwisho utafiti huu unapendekeza watafiti wengine kufanya utafiti katika maeneo ya kimuundo, kimsamiati pamoja na athari za matamshi ya Kisukuma katika Kiswahili sanifu.

Description

Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8694.S94J32)

Keywords

Sukuma language, Swahili language, Tanzania

Citation

Jackson, H. (2014) Matumizi ya lugha ya kisukuma katika kiswahili cha mazungumzo, Master dissertation, University of Dar es Salaam, Dar es Salaam