Ulinganishi wa tamthiliya ya kiswahili na Kichina: Uchunguzi wa Wakati Ukuta (1971) na Hadithi ya Kijijini Sangshuping (2002)
Abstract
Utafiti huu unahusu ulinganishi wa tamthiliya ya Kiswahili na ya Kichina zisizokuwa na uhusiano wa kihistoria. Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza kufanana na kutofautiana kwa tamthiliya ya Kiswahili na Kichina kwa kuzilinganisha tamthiliya teule mbili: Wakati Ukuta (Hussein, 1971) na Hadithi ya Kijijini Sangshuping (Zhu, 2002). Ulinganishi wa vipengele vya kisanaa vya tamthiliya teule ulikuwa sehemu muhimu ya utafiti huu. Sampuli ya utafiti huu ni tamthiliya mbili, ambazo moja ni ya Kiswahili na nyingine ni ya Kichina. Data zilikusanywa kwa mbinu ya kimaktaba. Uchambuzi wa data ulifanyika kwa kutumia Nadharia ya Utafiti Sambamba wa Fasihi Linganishi (Tapo la Marekani), ambayo inatolewa na wanazuoni wa Marekani Owen Aldridge (1969). Uwasilishaji na uchambuzi wa data ulifanywa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli (wa maelezo). Katika utafiti huu, mtafiti amezingatia vipengele vya wahusika, lugha na ploti. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, ingawa tamthiliya ya Kiswahili na ya Kichina zinatungwa katika mazingira tofauti, vipengele vyake bado vinafanana katika kiwango fulani. Wasomaji wanaweza kuzielewa tamthiliya hizi zinazotoka nchi tofauti na zenye lugha tofauti. Kwa upande mwingine, tofauti za vipengele vya tamthiliya hizi pia zinaweza kukuza maarifa kuhusu fasihi husika. Kwa kuzichambua tofauti za vipengele vya kisanaa vya tamthiliya teule, tofauti za kidhamira zinadhihirika. Jambo hili linasaidia kuleta uelewano wa kitamaduni baina ya jamii hizi mbili tofauti .