Matumizi ya kiswahili katika maeneo ya utamaduni vijijini nachingwea
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu unahusu Matumizi ya Kiswahili katika Maeneo ya Utamaduni Vijijini Nachingwea. Utafiti huu umejikita katika malengo makuu matatu ambayo ni kuchunguza kiwango cha matumizi ya lugha ya Kiswahili na Kimwera, kubainisha matumizi ya lugha kwa kuzingatia makundi ya kijamii kwa kuzingatia vigezo vya umri na jinsi, na hatimaye kuonesha kama kuna athari yoyote ya matumizi ya lugha ya Kiswahili katika lugha ya Kimwera. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uchanganuzi wa kimaeneo ambayo iliasisiwa na kutumiwa na Fishman 1972. Nadharia hii inaelezea mazoea ya wazungumzaji ya kupenda kuchagua kutumia lugha fulani katika eneo fulani na lugha nyingine itumike katika eneo jingine. Utafiti huu umefanyika katika vijiji vya Mchangani, Namajuni, na Mkalapa ambavyo vyote viko katika Kata ya Nang’ondo wilayani Nachingwea, mkoa wa Lindi. Watafitiwa 60 walihusika katika utafiti huu ambapo njia ya usampulishaji nasibu tabakishi ndio iliyotumika kuwapata watafitiwa hao 60 kwa kuzingatia vigezo vya umri na jinsi. Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji data ni hojaji, mahojiano, na ushuhudiaji. Matokeo ya Utafiti yanaonesha kwamba katika maeneo manne yaliyofanyiwa utafiti (tambiko, harusi, jando na unyago), lugha ya Kiswahili imeonekana kutumika sana katika maeneo mawili ya jando na unyago kuliko lugha ya Kimwera. Kwa matokeo haya sasa imedhihirika wazi kwamba lugha ya Kiswahili imeanza kuchukua dhima ya lugha ya Kimwera ya kutumiwa katika maeneo ya jando na unyago. Katika maeneo ya tambiko na harusi matokeo yameonesha kwamba, lugha ya Kimwera bado inadumishwa na watafitiwa kwa maana kwamba Kimwera kinatumiwa sana kuliko Kiswahili katika maeneo hayo ya utamaduni. Kwa kuzingatia kwamba watumiaji wengi wa Kiswahili ni vijana, na kwa kuzingatia maendeleo ya kijamii na kiteknolojia yanayoendelea kutokea hata huko vijijini, kuna uwezekano mkubwa katika miaka ijayo Kiswahili kuendelea kutumika hata katika maeneo ya utamaduni ya tambiko na harusi, hivyo kuhatarisha Kimwera kukosa watumiaji na hatimaye kinaweza kutoweka katika matumizi.