Dhima ya takriri ya kidhamira katika riwaya za watoto za m.m. mulokozi
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu ulihusu Dhima ya Takriri ya Kidhamira katika Riwaya za Watoto za M.M. Mulokozi. Tatizo la utafiti lilitokana na kushamiri kwa marudio ya dhamira katika kazi za M.M. Mulokozi, hivyo mtafiti kutaka kujua dhima ya urudiaji huo wa dhamira katika kazi husika. Malengo mahususi ya utafiti huu yalikuwa; kuchambua dhamira, kubainisha takriri ya kidhamira na kueleza dhima ya takriri ya kidhamira katika kazi teule za M. M. Mulokozi. Aidha, maswali ya utafiti yalikuwa; Je, kazi teule za M.M. Mulokozi zimesheheni dhamira gani? Je, takriri ya kidhamira imejibainishaje katika kazi teule za M.M. Mulokozi? Je, takriri ya kidhamira iliyojitokeza katika kazi teule za M.M. Mulokozi ina dhima gani? Mbinu mbalimbali za utafiti zilitumika ambazo ni usomaji wa kazi teule na uchambuzi wa kazi teule. Riwaya tatu za M.M. Mulokozi ambazo ni Ngoma ya Mianzi, Ngome ya Mianzi na Moto wa Mianzi zilitumika kama sampuli. Kutokana na utafiti wa awali uliofanywa na mtafiti kwa kusoma vitabu na nyaraka mbalimbali, imebainika kuwa hakukuwa na tafiti iliyokwisha kufanywa juu ya takriri ya kidhamira. Tafiti zilizopatikana kama za Lyimo (2004, 2009) na Muhamed (2009), zilijikita kuchunguza takriri kama kipengele cha kifani. Hali hiyo ilimfanya mtafiti kujihoji maswali mbalimbali kama vile: Je, takriri ni kipengele cha fani pekee? Je, ikijitokeza katika maudhui huwa na dhima gani? Hili ni tatizo la kiuchambuzi na kiuhakiki lililohitaji kutolewa majibu kitafiti hivyo mtafiti kulazimika kuchunguza dhima ya takriri ya kidhamira katika riwaya teule za M.M.Mulokozi. Vitabu teule vilisomwa na kuchambuliwa ili kukidhi malengo ya utafiti. Data za utafiti zilichakatwa na kuchambuliwa kwa kuongozwa na Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, riwaya za watoto za M.M.Mulokozi zimejengwa na dhamira mbalimbali ambazo ni uzalendo, ujasiri, utayari, ukarimu, nafasi ya mwanamke na upendo wa dhati. Pia, dhamira kama vile kujitoa muhanga, ushirikiano, imani kwa miungu, uvumilivu, usaliti, umuhimu wa uzazi, na udadisi zilibainishwa. Aidha, utafiti huu umethibitisha kuwa, riwaya teule za M.M. Mulokozi zimesheheni takriri ya kidhamira kwa kiasi kikubwa. Takriri husika ni pamoja na takriri ya dhamira kuu ambayo ni uzalendo na takriri ya dhamira ndogondogo ambazo ni ujasiri, utayari, ukarimu, nafasi ya mwanamke, upendo wa dhati, kujitoa mhanga, ushirikiano, uvumilivu, imani kwa miungu na udadisi. Vilevile, imebainika kuwa takriri ya kidhamira ina dhima anuai kama vile; kusisitiza mawazo ya mwandishi kwa hadhira, kukamilisha kisa au hadithi, kuonesha mtazamo wa mwandishi juu ya maisha, kuonesha muktadha wa utendaji au usimulizi, kuweka kumbukumbu ya matukio muhimu ya jamii, kuonesha mtindo wa masimulizi ya kifasihi simulizi na kuibua hisia kwa hadhira. Kwa ujumla, utafiti umebaini kuwa, takriri kama kipengele cha kisanaa siyo kipengele cha fani pekee bali huweza kijitokeza pia katika maudhui. Aidha, umeeleza dhima mbalimbali za takriri katika kazi ya sanaa mbali na dhima ya kusisitiza ujumbe wa msanii iliyoelezwa na wataalamu mbalimbali wa fasihi. Mwisho, baada ya kuwasilisha matokeo ya utafiti, mtafiti ametoa mapendekezo juu ya nini kifanyike zaidi kutokana na matokeo hayo.