Athari ya mhariri katika mswada: uchunguzi wa machapisho teule ya kifasihi ya Kiswahili

Date

2017

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu umelenga kuchunguza Athari ya Mhariri katika Miswada ya Kifasihi ya Kiswahili. Hii inatokana na kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya waandishi juu ya namna wahariri wanavyohariri miswada yao. Malalamiko hayo husababisha kuwapo kwa mgongano baina ya wahariri na waandishi. Hoja ya msingi katika utafiti huu ni kuwa mhariri ni kiungo muhimu sana katika tasnia ya uchapishaji licha ya kuwapo kwa dosari ndogondogo zinazojitokeza kwa wahariri wasiokuwa makini. Mtafiti ameongozwa na malengo mahususi, yaani kubaini sifa za mhariri wa miswada ya kifasihi ya Kiswahili, kufafanua majukumu ya mhariri wa miswada ya kifasihi ya Kiswahili na jinsi anavyozingatia majukumu yake na kubainisha athari za mhariri katika miswada ya kifasihi ya Kiswahili. Katika ukusanyaji wa data za uwandani na maktabani katika wilaya za Kinondoni, Ubungo na Ilala, mtafiti ametumia mbinu za mahojiano na uchambuzi na uchanganuzi wa matini teule. Kwa kutumia Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji, Nadharia ya Uhariri na baadhi ya Kanuni za Uhariri zimeweza kubainika athari chanya na athari hasi za mhariri. Athari chanya ni kuboresha lugha ya mwandishi; kuboresha msuko wa hadithi na kuboresha maudhui ya kitabu. Kwa upande mwingine athari hasi ni kubadili jina na umbo la kitabu; kucheleweshwa kwa miswada; athari za kidhana na kimaana; kubadili sauti ya mwandishi na kukosekana kwa ushikamani, uthabiti na muwala. Licha ya kuwapo kwa malalamiko mengi ya waandishi juu ya namna wahariri wanavyohariri kazi zao, na kuonesha kuwa kwa sehemu kubwa wahariri wanaharibu miswada yao. Mtafiti amegundua kuwa mengi ya malalamiko hayo siyo ya msingi, na yanatokana na waandishi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na taaluma ya uchapishaji, hususan kipengele cha uhariri.

Description

Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8702.P323)

Keywords

Swahili language, Grammar, Editing

Citation

Pacho, P.J. (2017) Athari ya mhariri katika mswada: uchunguzi wa machapisho teule ya kifasihi ya Kiswahili. Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.