Ruwaza na maana za utendeka na utendana katika vitenzi vya Kihehe

Date

2013

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu ulioshughulikia Ruwaza na Maana za Utendeka na Utendana katika lugha ya Kihehe ulifanyika mkoani Iringa katika wilaya ya Mufindi vijiji vya Rungemba, Maduma na Waasa. Malengo ya utafiti yalikuwa ni kubainisha maumbo, mfuatano na maana zinazoukiliwa na mofimu nyambulishi hizo. Data za utafiti huu zilipatikana uwandani kwa watafitiwa wapatao sabini na wawili (72) kwa kutumia mbinu ya ushuhudiaji, mahojiano na hojaji. Aidha, utafiti huu uliongozwa na Kanuni Akisi (KA) ya Baker (1985): Unyambulishaji wa kimofolojia sharti uakisi unyambulishaji wa kisintaksia.Matokeo ya utafiti huu yamebaini kuwa unyambulishaji tendeka katika lugha ya Kihehe unawakilishwa na mofimu //-isik-// katika vitenzi vya silabi moja na mofimu //-ik-// kwa vitenzi viso-ukomo. Aidha, matokeo ya utafiti huu yanabainisha mofimu //-kwi-// na //-an-// kuwa ni maumbo yanayodokeza unyambulishaji tendana katika lugha ya Kihehe. Mofimu //-kwi-// inatokea kabla ya mzizi ilhali mofimu //-an-// hunyambulishwa baada ya mzizi au shina la kitenzi. Vilevile, utafiti huu umeeleza na kuunda kanuni zinazoongoza utokeaji wa unyambulishaji tendeka na tendana. Pia, katika utafiti huu imebainika kuwa mfuatano wa mofimu nyambulishi za utendeka na za utendana haukubaliki. Mfuatano unaokubalika ni ule unaohusu mofimu nyambulishi ya utendana na tendeka //-an- + -ik-// katika vitenzi viso-ukomo, hususani kwa umbo //-an-// pekee. Aidha, matokeo yanaonesha maana zinazodokezwa na mofimu tendeka ni pamoja na uwezekano wa jambo kufanyika na urahisi wa kutenda jambo fulani. Mofimu ya utendana //-kwi-// na //-an-// inahukilia maana ya ushirikiano. Pia, mofimu hizo hufungamana na maana ya kinahau ambapo ili kupata maana huhitaji urejelezi wa muktadha wa kimatumizi. Utafiti pia umependekeza tafiti nyingine kufanyika kuhusu unyambulishaji wa mofimu nyambulishi nyingine ili kubaini maumbo, mfuatano na maana zinazodokezwa na mofimu nyambulishi hizo katika lugha hii.

Description

Keywords

Ruwaza, Utendeka na utendana, Kihehe

Citation

Mashaka, A (2013) Ruwaza na maana za utendeka na utendana katika vitenzi vya Kihehe, Tasinifu ya M.A. (Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Available at http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx?parentpriref=)