Dhima ya taswira katika hadithi za watoto: uchambuzi wa vitabu vya hadithi vinavyosomeshwa Zanzibar
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu umechunguza Dhima ya Taswira katika Hadithi za Watoto: Uchambuzi wa vitabu vya hadithi vinavyosomeshwa Zanzibar. Utafiti huu uliongozwa na malengo mawili. Lengo la kwanza lilikuwa kubainisha aina za taswira zinazojitokeza katika hadithi za watoto za Zanzibar kwa kupitia hadithi teule. Lengo la pili lilihusu kueleza dhima ya taswira katika hadithi za watoto za Zanzibar kwa kutumia hadithi teule. Nadharia ya Semiotiki na Mwitiko wa Msomaji ziliongoza utafiti huu na zilitumika katika uchanganuzi wa data. Data za utafiti huu zilikusanywa kutoka Zanzibar katika visiwa viwili vya Unguja na Pemba kutoka vitabu vitatu vya hadithi za watoto zinazosomeshwa shule za Zanzibar, walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Data hizo zilichanganuliwa kwa njia ya kimaelezo. Mbinu ya uchambuzi matini, hojaji na mahojiano ndizo zilizotumika katika uwasilishaji wa data za utafiti. Utafiti ulibaini kupitia hadithi teule kuwa, kuna aina mbalimbali za taswira zinazojitokeza katika hadithi za watoto zinazosomeshwa shule za Zanzibar. Taswira hizo ni taswira za matendo ya wahusika, taswira zinazoonekana, taswira za kiishara, taswira za sitiari, taswira za tashbiha na taswira za hisi. Kwa upande wa dhima, utafiti umeonesha kuwa, taswira katika hadithi za watoto zina dhima kifani na kimaudhui. Kifani taswira zina dhima ya kuvuta usikivu kwa watoto, kuwavutia watoto, kufupisha hadithi na kujenga mandhari. Kwa upande wa dhima za taswira kimaudhui ni kujenga dhamira na migogoro mbalimbali. Kwa ujumla, katika utafiti huu ilionekana kuwa, matumizi ya taswira katika hadithi za watoto ni kipengele muhimu sana, kwa sababu taswira hizo huwajenga watoto na kuwakuza kifikra na kiakili. Aidha, taswira husaidia watoto kujua mienendo ya maisha katika kujifunza mambo mbalimbali, pia kuwaelimisha na kuwaonya mambo ambayo ni maovu kwa jamii yao nzima.