Uainishaji wa ngeli za nomino katika lugha ya Kinyakyusa kimofolojia na kisemantiki
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuainisha ngeli za nomino za lugha ya Kinyakyusa kimofolojia na kisemantiki, kufafanua mtawanyiko wa nomino kwa uzingatizi wa kisemantiki na kueleza dhima za viambishi ngeli vya nomino kimtawanyiko. Utafiti huu umefanyika katika kata za Isange, Luteba na Mpombo, wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, nchini Tanzania. Utafiti huu, uliongozwa na Nadharia ya Mofolojia Asili (NMA) ili kufanikisha malengo yake. Nadharia hii imetumika kubaini viambishi awali vya nomino na dhima zake kwa kuangalia maana ya viambishi hivyo. Aidha, nadharia hii imetumika kujua maana ya nomino zilizoainishwa katika ngeli mbalimbali ili kueleza mtawanyiko wa nomino hizo. Kazi imegawanyika katika sura tano. Sura ya kwanza, imeeleza kiini cha utafiti na utaratibu uliozingatiwa katika utafiti. Sura ya pili, imeshughulikia mapitio ya maandiko kuhusiana na uainishaji wa ngeli za nomino. Sura ya tatu, imeshughulikia mbinu za utafiti ambapo populesheni, sampuli, usampulishaji na njia tatu zilizotumika kukusanya data zimebainishwa. Sura ya nne, imeshughulikia uchanganuzi na uwasilishaji wa data iliyokusanywa uwandani. Katika uchanganuzi huo ngeli za nomino zimeainishwa kwa kigezo cha kimofolojia kwa kuzingatia mkabala wa jozi ya viambishi vya umoja na wingi. Aidha, kigezo cha kisemantiki kimetumika ili kufafanua mtawanyiko wa nomino katika ngeli tofauti. Sura ya tano, imeshughulikia matokeo, hitimisho na mapendekezo ya tafiti fuatishi. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kuwa lugha ya Kinyakyusa ina ngeli za nomino 12. Pia utafiti huu umebainisha kuwa nomino za Kinyakyusa zenye sifa za kisemantiki zinazofanana zimetawanyika katika ngeli tofauti zikiainishwa kwa kigezo cha kimofolojia. Vilevile utafiti huu umebainisha kuwa viambishi ngeli vya nomino za Kinyakyusa vina dhima zaidi ya umoja, wingi, ukubwa na udogo. Dhima hizo ni ubaya, uzuri, udhaifu, urefu, wembamba, ufupi, tabia mbaya na tabia nzuri.