Maana ya majina ya asili katika jamii ya Kiuru

No Thumbnail Available
Date
2013
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu unahusu maana za majina ya asili. Mpaka sasa hakuna utafiti ambao umefanyika kuhusu maana za majina ya asili katika jamii ya Wauru. Kwa hiyo utafiti huu unalenga kuchunguza maana ya majina ya asili katika jamii ya Wauru. Utafiti umejikita katika kubainisha mfumo wa majina ya asili, kuchunguza asili ya majina, maana mahususi ya baadhi ya majina ya jamii ya Wauru, pamoja na umuhimu na mchango wa majina katika utamaduni wa Wauru. Utafiti umefanyika mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Moshi vijijini katika vijiji vya Materuni, Mruwia, Kyaseni na Mwasi. Mbinu zilizotumika katika utafiti huu ni pamoja na: usampulishaji, ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji wa data. Data ya utafiti ni ya kutoka uwandani ambapo mtafiti alikusanya data kupitia hojaji na dodoso kutoka kwa watafitiwa na kuzifanyia uchanganuzi. Kazi imegawanyika katika sura tano. Sura ya kwanza ina utangulizi unaofafanua usuli wa utafiti, tamko la utafiti, malengo ya utafiti, umuhimu wa utafiti, na eneo la utafiti. Sura ya pili inahusika na mapitio ya maandiko na kiunzi cha Nadharia ya Uumbaji iliyotumika kama mhimili wa utafiti huu. Sura ya tatu imehusika na mbinu na njia za utafiti zilizotumika katika kufanikisha utafiti huu. Mbinu zilizotumika ni ya pamoja na kubaini sampuli na kufanya usampulishaji ambapo mtafiti alitumia njia ya mahojiano na hojaji ili kupata taarifa za utafiti huu toka kwa watafitiwa. Sura ya nne, imeshughulikia uchanganuzi na uwasilishaji wa data kama zilivyopatikana kutoka uwandani. Data zimegawanyika katika sehemu nne: ambapo sehemu ya kwanza imebainisha mfumo wa majina ya asili ya jamii ya Wauru, sehemu ya pili imetoa ufafanunuzi kuhusu asili ya majina ya jamii ya Wauru, sehemu ya tatu imetoa ufafanuzi kuhusu maana mahususi ya baadhi ya majina ya jamii ya Wauru na sehemu ya nne imejadili umuhimu na mchango wa majina katika utamaduni wa Wauru. Sura ya tano imegawanyika katika sehemu tatu; sehemu ya kwanza inaelezea matokeo ya utafiti ambapo utafiti umebaini kuwa majina mengi ya asili yanayotolewa katika jamii ya Wauru, yamekuwa yakipungua siku hadi siku kutokana na kuingia kwa majina ya kigeni. Aidha, utafiti umebaini kuwa majina katika jamii ya Wauru hayatolewi kiholela, bali hutolewa kwa kuzingatia mazingira halisi ya uzaliwaji wa mtoto na matatizo ama faraja alizokuwa nazo mama kipindi au/na baada ya ujauzito. Pia, utafiti umegundua kuwa asili ya majina ya Kiuru hufungamana na mambo makuu nne: mosi tabia, maumbile au muonekano wa mtoto pindi anapozaliwa au wakati wa makuzi, pili matukio mbalimbali ya kijamii, tatu vipindi mbalimbali katika jamii ya Wauru, nne misingi ya imani na desturi za jamii ya Wauru.
Description
Keywords
Uru language, Names, Bantu languages, Languages, Tanzania
Citation
Azael, R (2013) Maana ya majina ya asili katika jamii ya Kiuru, Tasinifu ya M.A. (Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Kinapatikana http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)