Mchango wa lahaja ya kipemba katika kukuza kiswahili sanifu: mifano kutoka Istilahi za Tiba na Uuguzi
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Wataalamu mbalimbali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa lahaja za Kiswahili zina hazina kubwa inayoweza kuchangia katika kukuza msamiati na istilahi katika Kiswahili sanifu endapo zitatumiwa ipasavyo. Hivyo, wanatoa wito wa kufanyika kwa utafiti wa kina katika lahaja za Kiswahili ili kuziwezesha kuchangia katika kukuza na kuendeleza Kiswahili sanifu. Kutokana na wito huo utafiti huu ulilenga kuchunguza namna lahaja ya Kipemba inavyoweza kuchangia katika kukuza na kuendeleza Kiswahili sanifu, msisitizo ukiwa katika tasnia ya tiba na uuguzi. Data za utafiti huu zilipatikana uwandani na maktabani. Katika kukusanya data za uwandani, mtafiti alitumia mbinu za usaili, hojaji na ushuhudiaji. Data za maktabani zilikusanywa kupitia Kamusi ya Tiba iliyoandikwa na Mwita na Mwansoko (2003) na Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Tatu iliyoandikwa na TUKI (2013). Data hizi za maktabani zilijikita zaidi katika kubainisha upungufu wa istilahi za tiba na uuguzi unaojitokeza katika Kiswahili sanifu. Data za utafiti huu zimechambuliwa kwa kutumia mikabala ya kimaelezo na kitakwimu. Data zimechambuliwa kwa kuzingatia Nadharia ya Vikoa vya Maana ambapo istilahi za tiba na uuguzi zilizopatikana kutoka katika lahaja ya Kipemba zimewekwa kulingana na kikoa kinachohusika. Mathalani, tuna kikoa cha magonjwa ya watoto, magonjwa ya wanawake na magonjwa ya jumla. Kwa upande wa vikoa vya madawa tuna madawa ya kunywa, kujipaka, ‘kujiamba’, kufukiza na kuogeshea watoto. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba lahaja ya Kipemba ina mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza Kiswahili sanifu hususani katika tasnia ya tiba na uuguzi. Lahaja hii, mbali na mambo mengine imetuwezesha kupata istilahi ambazo zikisanifishwa zinaweza kukabiliana na upungufu wa idadi ya istilahi za tiba na uuguzi katika Kiswahili sanifu.