Mofosintaksia ya ruwaza ya ukanushi katika vitenzi vya lugha ya kisukuma: lahaja ya Kimunasukuma
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Kazi hii ya kitafiti ilichunguza Mofosintaksia ya Ruwaza ya Ukanushi katika Vitenzi vya Lugha ya Kisukuma: Lahaja ya KimunaSukuma. Malengo ya utafiti huu ni kuchunguza na kubainisha maumbo ya mofimu za ukanushi, kufafanua utokeaji wa mofimu za ukanushi, na kubainisha ruwaza ya utokeaji wa mofimu kanushi katika vitenzi vya Kisukuma: Lahaja ya KimunaSukuma. Data za utafiti huu zilikusanywa kutoka katika kata tatu ambazo ni: Nindo, Tinde na Songwa. Kata hizi zipo katika wilaya za Kishapu na Shinyanga Vijijini, mkoani Shinyanga. Aidha, sampuli ya watafitiwa 60, ilihusishwa katika ukusanyaji wa data. Nadharia ya Umbo Upeo iliyoasisiwa na Prince, A na P. Smolensky (1993) ndiyo iliyoongoza uchambuzi wa data za utafiti huu. Data za msingi zimekusanywa uwandani kwa kutumia mbinu ya mahojiano, pamoja na mbinu ya ushuhudiaji. Vilevile data fuatizi zimekusanywa kutoka maktabani. Pia, maandiko mbalimbali ya Kisukuma, yaani Biblia, na vitabu vya Tenzi za Rohoni vimetumika katika kupata data za utafiti huu. Mkabala usio wa kiidadi umetumika katika uchambuzi wa data kwa kuzingatia mashartizuizi yaliyopo katika lugha ya Kisukuma. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa mofimu kanushi katika lugha ya Kisukuma hujitokeza baada ya mofimu ya nafsi zinapotokea kama mofimu awali, na baada ya mzizi wa kitenzi zinapotokea kama mofimu tamati. Utokeaji huu wa mofimu kanushi ndiyo huruhusu kuzalisha maumbo kanushi yaliyofikia upeo wa ukubalifu katika lugha ya Kisukuma. Aidha, Kisukuma kama zilivyo baadhi ya lugha za Kibantu inaruhusu utokeaji wa mofimu kanushi zenye kubeba dhima nyingine kama vile njeo au hali katika kitenzi husika. Kwa ujumla utafiti huu umebaini kuwepo kwa mofimu saba za ukanushi katika lugha ya Kisukuma. Mwisho, mapendekezo ya tafiti fuatizi yametolewa ambapo imependekezwa utafiti wa kuichunguza lugha ya Kisukuma na lugha nyingine za mbari ya Kibantu ufanyike, kisintagmatiki na kipradigimatiki (yaani uhusiano wa kiulalo “kisilisila” na kiwima) kwa vipengele mbalimbali vya lugha