Matumizi ya majina katika utambulisho wa jamii ya Watanzania

No Thumbnail Available
Date
2011
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu unahusu Matumizi ya Majina katika Utambulisho wa Jamii ya Watanzania, lengo likiwa ni kuchunguza majina yanayofungamana na lugha ya Kiswahili na ambayo yanakubaliwa kutumika katika utambulisho wa jamii ya Watanzania. Utafiti huu umejikita katika majina ya familia, majina ya matukio ya kihistoria na majina ya vivutio vya utalii. Nadharia ya Utambulisho wa jamii ya Tajfel iliyoasisiwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 ilitumika katika kuongoza utafiti huu. Data zilikusanywa kutoka katika Kata tatu za manispaa zote tatu za jiji la Dar es Salaam, yaani Kata ya Segerea iliyoko katika manispaa ya Ilala, Kata ya Mwenge iliyoko katika manispaa ya Kinondoni na Kata ya Mbagala iliyoko katika manispaa ya Temeke. Pia utafiti ulihusisha Jumba la Utamaduni na Makumbusho la Taifa lililoko katika manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, pamoja na Bodi ya Utalii ya Taifa ambayo ofisi zake ziko katika Manispaa ya Ilala. Sampuli ya aina tatu ilihusishwa katika ukusanyaji wa data. Kwanza, walihusishwa watafitiwa 120 ambapo usampulishaji nasibu tabakishi ulitumika kwa kuzingatia vigezo vya umri na jinsi. Vilevile, walihusishwa wafanyakazi wanne, wawili kutoka Jumba la Makumbusho la Taifa na wawili kutoka Bodi ya Utalii ya Tanzania. Katika ukusanyaji wa data, mbinu za hojaji, mahojiano na upitiaji wa nyaraka na kumbukumbu muhimu zilitumika. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba, majina 40 kati ya majina 50 ya familia yaliyoulizwa yanakubaliwa kutumika katika utambulisho wa jamii ya Watanzania. Majina ya familia yanayokubaliwa ni Nyerere, Pinda, Mwinyi, Karume, Kawawa, Mkapa, Sokoine, Migiro, Kikwete, Mkwawa, Sitta, Mirambo, Warioba, Kimweri, Kinjekitile, Msekwa, Makweta, Bibi Titi, Kingunge, Isike, Machemba, Malecela, Jumbe, Fundikira, Makinda, Mwema, Makamba, Nyalali, Nagu, Mrema, Rumanyika, Msuya, Lipumba, Mongela, Kapuya, Sumaye, Bomani, Lowasa, Mbowe na Kolimba. Vilevile, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, majina mengine yanayokubaliwa kutumika katika utambulisho wa jamii ya Watanzania ni Azimio la Arusha, Uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Vita vya Kagera, Vita vya Majimaji, mlima Kilimanjaro, mlima Meru, milima ya Usambara, milima ya uluguru, ziwa Tanganyika, ziwa Nyasa, mto Kagera, hifadhi ya Serengeti, hifadhi ya Mikumi, hifadhi ya Ngorongoro, hifadhi ya Manyara, mji mkongwe wa Bagamoyo, Zanzibar, Bonde la Ufa, mji wa Kilwa na Makumbusho. Ukubalifu wa majina haya una maana kwamba jamii ya Watanzania wana ufahamu na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utaifa na utambulisho hivyo kukubali kutambuliwa kama wamoja kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Description
Available in print form
Keywords
Real estate management, Building management, Outsourcing, Tanzania
Citation
Joho, H.A(2011) Matumizi ya majina katika utambulisho wa jamii ya Watanzania master dissertation, University of Dar es Salaam, Available at http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx