athari za matamshi ya msamiati wa Kiswahili sanifu katika kimakunduchi

No Thumbnail Available
Date
2012
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
The university of Dar es Salaam
Abstract
Suala la kuathiriana kwa lugha limejadiliwa na wataalamu wengi. Hata hivyo hakuna utafiti uliofanywa juu ya athari za matamshi ya Kiswahili sanifu katika lahaja ya Kimakunduchi. Utafiti huu ulinuiliwa kuchunguza athari za matamshi ya Kiswahili sanifu katika Kimakunduchi. Sura ya kwanza inaeleza kuhusu lahaja inayotafitiwa kuwa ni Kimakunduchi na inazungumzwa Unguja katika Mkoa wa Kusini na Wilaya ya Kusini katika kijiji cha Makunduchi. Tatizo kubwa katika uchunguzi ilikuwa upande wa matamshi hususani katika sauti ikiwemo ubadilikaji uchopekeji na udondoshaji. Madhumuni ya uchunguzi huu ni kuchunguza athari za matamshi ya Kiswahili sanifu katika Kimakunduchi na sababu za kutokea kwa athari hizo. Mada hii imechaguliwa kwa sababu, watafiti wameangalia vipengele hivyo vya matamshi lakini wamevifananisha na kuvitofautisha kutoka lahaja moja na nyingine. Hivyo kutokana na upeo wa mtafiti hakuna utafiti uliofanywa kuhusu mada hii. Utafiti huu utakuwa na manufaa kwa watafiti wa lugha kiisimu, walimu na wanafunzi wa Kimakunduchi wanaojifunza Kiswahili sanifu. Sura ya pili ya utafti inashughulikia mapitio na machapisho mbalimbali yanayochukuzana na mada. Sura ya tatu inashughulikia mbinu za utafiti na ukusanyaji wa data. Aidha malengo ya utafiti yalifikiwa na kukidhiwa haja maridhawa. Zana za utafiti zilitumika katika kukusanyia na kuchambulia data. Aidha utafiti ulitumia mbinu za uwandani na maktabani. Data ilikusanywa kwa njia ya mahojiano, hojaji na ushuhudiaji. Mbali na mbinu hizi, utafiti uliongozwa na nadharia ya Muachano na Makutano ambayo inadai kuwa; Jamii lugha moja inapoingiliana na jamiilugha nyingine, lugha za wanajamii hawa huathirika na kuanza kutokea athari katika vipengele kadhaa vya kiisimu vya lugha hiyo na hatimaye kuwa lugha moja.Sura ya nne, inawasilisha matokeo ya utafiti. Kutokanana na utafiti huu imebainika kuwa; lahaja ya Kimakunduchi imeathiriwa na Kiswahili sanifu katika vipengele vya matamshi ya maneno yake, kwa kubadilisha sauti, matumizi ya maneno ya Kiswahili sanifu badala ya Kimakunduchi na michakato mingine ya kifonolojia kama vile; udondoshaji na uchopekaji wa sauti na kutokana na athari hizo, hatimaye msamiati huo hutamkwa sawa na Kiswahili sanifu. Sanjari na hayo, utafiti huu umeweka bayana sababu za kuathiriwa Kimakunduchi, ambapo miongoni mwake ni pamoja na muingiliano wa wanajamii tofauti tofauti kutokana na sababu za kiuchumi na kijamii, kuenea kwa vyombo vya habari, Serikali kusisitiza matumizi ya Kiswahili sanifu badala ya lahaja ya Kimakunduchi, mtazamo hasi juu ya matumizi ya lahaja hii na ukaribu wa kijiografia kutoka Mjini Unguja na Makunduchi. Sura ya tano inatoa matokeo ya utafiti, hitimisho pamoja na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha utafiti unaohusu kuathiriana kwa lugha na isimu kwa jumla.
Description
Available in print copy
Keywords
kimakunduchi
Citation
Khamis, M.(2012). athari za matamshi ya msamiati wa Kiswahili sanifu katika kimakunduchi. Master dissertation, university of Dar es Salaam Available at ( http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/search.aspx?formtype=advanced)