Mabadiliko ya kiutendaji na kidhamira ya nyimbo za ibada za Kikatoliki.

Loading...
Thumbnail Image
Date
2016
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu umefanyika ili kuchunguza Mabadiliko ya Kiutendaji na Kidhamira ya Nyimbo za Ibada za Kikatoliki kuanzia miaka ya 1980 hadi 2015. Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko katika nyimbo za Kikatoliki tukilinganisha na miaka ya 1980 ambapo hapakuwa na uchezaji, lakini siku hizi kumekuwa na uchezaji. Hali hii imetusukuma kufanya utafiti ili kuona ni nini kimesababisha mabadiliko haya, pia kuona kama mabadiliko haya ni chanya au hasi. Utafiti huu umetumia njia za utafiti wa nyaraka na wa uwandani. Katika njia ya nyaraka tumepitia nyaraka mbalimbali kama Kanuni za Kanisa Katoliki kuhusu nyimbo, na kuchunguza maandiko yanayohusiana na nyimbo za dini katika maktaba zilizopo Wilaya za Temeke na Kinondoni. Utafiti wa uwandani ulifanyika katika Wilaya ya Ilala ukihusisha kwaya ya Mtakatifu Yosefu na Mtakatifu Fransisko, zilizopo jijini Dar es Salaam. Mtafiti alitumia mbinu ya mahojiano huru na ushuhudiaji kupata data za msingi za uwandani. Nadharia zilizoongoza utafiti huu ni Nadharia ya Uhalisia iliyotumika kuchunguza uhalisia wa dhamira zilizojitokeza katika nyimbo zilizotafitiwa tukilinganisha na jamii ya Kitanzania, na Nadharia ya Utendaji katika Fasihi iliyotumika kuchunguza vitendo vya waimbaji, lugha, mavazi, matumizi ya vifaa na muktadha wa uwasilishaji. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwapo kwa mabadiliko makubwa yenye athari chanya na hasi. Baadhi ya athari chanya ni kuongezeka kwa waumini wanaovutiwa na muziki, ongezeko la kipato katika kwaya husika na Kanisa, kuwasaidia waumini kukua kimaadili, kujenga shabaha ya kumtukuza Mungu, na kuwapunguzia waumini wenye matatizo huzuni pamoja na kuwaburudisha. Athari hasi ni kama vile: upotoshaji wa lugha inayotumika katika nyimbo za ibada, kubadilika kwa ladha ya uimbaji wa Kikatoliki, kugeuzwa kwa Makanisa kama sehemu ya ibada na kuwa kama kumbi za starehe, pia kufanya nyimbo za ibada kuwa biashara badala ya kutumika kumtukuza Mungu. Utafiti huu pia ulibaini sababu za mabadiliko ya nyimbo kuwa ni baadhi ya walimu wa nyimbo kutokuwa na elimu ya nyimbo za Kikatoliki, kukua kwa biashara ya nyimbo za dini, uzembe wa baadhi ya viongozi wa Kanisa waliopewa jukumu la kusimamia uimbaji unaofaa, kuiga uimbaji wa madhehebu mengine pamoja na mwingiliano wa jamii zenye tamaduni tofautitofauti.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8703.5.M452)
Keywords
Folk literature, Swahili, Church music, Catholic church
Citation
Mgaya, G. (2016). Mabadiliko ya kiutendaji na kidhamira ya nyimbo za ibada za Kikatoliki. Tasnifu ya Uzamili, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.