Ulinganishi wa miundo ya silabi za lugha ya kiiraqw na kiswahili

No Thumbnail Available
Date
2014
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu ulilenga kulinganisha miundo ya silabi za lugha ya Kiiraqw na Kiswahili. Utafiti unaendeleza mbele hatua za kuzitafiti lugha za Kiiraqw na Kiswahili ambapo kazi hii inatoa maoni zaidi katika kuelezea miundo ya silabi za lugha hizi na kuangalia kufanana na kutofautiana kwa miundo ya silabi hizo. Data zilizotumika katika utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia utafiti wa maktabani na uwandani. Data za uwandani zilikusanywa kwa kutumia njia ya majadiliano katika vikundi vilivyokuwa vimelengwa, hojaji na mahojiano, ili kupata data andishi na simulizi. Uchambuzi, uwasilishaji na ufasili wa data uliongozwa na nadharia ya Umbo Upeo (UU) ya Allan Prince na Paul Smolensky (1993). Data zilichambuliwa na kuwasilishwa kwa mkabala wa kimaelezo na kwa kutumia majedwali. Matokeo yanaonesha kwamba lugha ya Kiiraqw inaelekea kufanana na lugha ya Kiswahili katika idadi ya irabu zake na viyeyusho; lakini lugha hizi zimetofautiana katika idadi na aina za konsonanti zake. Matokeo yanaonesha pia kwamba lugha ya Kiiraqw ina miundo 15 ya silabi ilhali lugha ya Kiswahili sanifu ina miundo 9 ya silabi. Licha ya lugha hizi kuwa na asili tofauti, zimetokea kufanana katika baadhi ya miundo ya silabi zake na katika mpangilio wa baadhi ya mashartizuizi. Miundo ya silabi ambayo imejitokeza katika lugha zote mbili ni pamoja na miundo ya I, KI, YI, KKI, KYI na IK. Ingawa utafiti huu umedokeza kufanana kwa baadhi ya mifumo ya sauti za lugha hizi kama ilivyo katika irabu, tunaona bado kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa kimaabara kuthibitisha kufanana ama kutofautiana kwa irabu za lugha hizi. Pia, kuna kila sababu ya kufanyika utafiti zaidi wa kulinganisha lugha hizi katika vipengele vingine vya kifonolojia.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PJ2556.D46)
Keywords
Iraqw language, Swahili language, Languages, Syllabication, Tanzania
Citation
Deogratius, E. (2014) Ulinganishi wa miundo ya silabi za lugha ya kiiraqw na kiswahili, Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.