Matumizi ya kipemba katika shughuli za kielimu na mawasiliano ya nyumbani kwa wapemba waliohamia Unguja

No Thumbnail Available
Date
2014
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia “Matumizi ya Kipemba katika Shughuli za Kielimu na Mawasiliano ya Nyumbani kwa Wapemba Waliohamia Unguja”. Utafiti umefanyika katika shehia ya Kinuni na Mtopepo, Mkoa wa Mjini Magharibi, Wilaya ya Magharibi Unguja. Watafitiwa walipatikana kwa kutumia njia ya Usampulishaji nasibu tabakishi, kwa kuzingatia vigezo vya umri na jinsi. Aidha, mbinu zilizotumika katika ukusanyaji data ni: hojaji, mahojiano, usikilizaji, kujichunguza na ushiriki. Utafiti ulilenga kubainisha kiwango, kubainisha sababu na kujadili athari za matumizi ya Kipemba katika shughuli tajwa. Ili kufanikisha kazi hii, utafiti huu uliongozwa na Nadharia Jumuishi ya Giles (1979) na Nadharia ya Uchanganuzi wa Kimaeneo ya Fishman (1972). Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa matumizi ya Kipemba MKM kwa watafitiwa wanafunzi yamechukuwa nafasi kubwa ya kutumiwa na wanafunzi wakiwa ndani na nje ya darasa bila ya usimamizi wa mwalimu, kinyume na wawapo na mwalimu. Sababu zilizoelezwa ni pamoja na: kutomudu vema Kiswahili Sanifu na kuathiriwa na lugha yao ya kwanza (Kipemba). Kuhusu matumizi ya Kipemba MCH, ni kutokana na hofu ya kuchekwa na baadhi ya wanafunzi wenzao, hamu ya kumudu vema lugha inayopaswa kutumika shuleni na kuhofia kupungua kwa alama za ufaulu kwa masomo kwa vile Kiswahili Sanifu ndiyo lugha ya kufundishia. Kuhusu mawasiliano ya nyumbani, Kipemba kimeonekana kutumika zaidi dhidi ya lugha nyingine za jamii. Sababu za matumizi hayo ni pamoja na Kipemba kuwa lugha ya kwanza na ya utambulisho wa Wapemba. Kwa kuzingatia matokeo hayo ya matumizi ya Kipemba, kuna dalili kwamba lugha za jamii zinaweza kuchukuwa nafasi ya kutumika katika maeneo rasmi na yasiyo rasmi yenye kundi kubwa la jamii-lugha fulani. Hivyo ni vizuri kwa wizara ya elimu pamoja na sera ya lugha nchini Tanzania kusimamia kwa ukaribu matumizi sahihi ya Kiswahili Sanifu na lugha za jamii nchini.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8704.Z9S24)
Keywords
Swahili language, Pemba Island (Tanzania), Unguja, Tanzania, Languages
Citation
Salim, S. A (2014) Matumizi ya kipemba katika shughuli za kielimu na mawasiliano ya nyumbani kwa wapemba waliohamia Unguja, Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.