Mwitiko wa hadhira ya tamthilia: mifano toka tamthilia ya nguzo mama
No Thumbnail Available
Date
2012
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu unahusu mwitiko wa hadhira ya tamthilia kwa kutoa mifano kutoka katika tamthilia ya Nguzo Mama. Utafiti ulijikita zaidi katika kuangalia mwitiko wa hadhira ya mchezo wa tamthilia jukwaani na utafiti huu umegawanyika katika sura tano tofauti tofauti. Sura ya kwanza ni utangulizi wa utafiti ambapo usuri wa tatizo umewasilishwa ambapo umeeleza kwa kifupi tafiti zilizotangulia kuhusiana na tamthilia hii na kubaini pengo lililosababisha kufanyika kwa utafiti huu. Tatizo la utafiti limebainishwa, malengo na maswali ya utafiti yaliyoongoza utafiti huu pia umuhimu, mawanda na mpangilio mzima wa utafiti huu vimeelezewa katika sura hii. Sura ya pili inahusu mapitio ya machapisho mbalimbali pamoja na tafiti zilizofanywa kuhusiana na mada hii ya utafiti. Pia sura hii imejadili kiini cha nadharia kilichoongoza utafiti na uchambuzi wa data za utafiti huu. Sura ya tatu imejadili mbinu mbalimbali za utafiti pamoja na mbinu hizo imewasilisha vifaa vilivyotumika katika kukusanya data. Pia sura hii imeonyesha vyanzo vya data, sampili ya utafiti pamoja na changamoto mbalimbali alizokabiliana nazo mtafiti wakati wa kukusanya data. Katika sura ya nne uchambuzi na data na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti umefanyika. Katika uchambuzi huo imebainika kuwa vipo vipengele mahususi vinavyosababisha mwitikio wa hadhira ya tamthilia ikiwa inatendwa jukwaani, vipengele hivyo husababisha hadhira kuitikia matini ya kazi ya fasihi kwa namna tofauti tofauti. Aidha katika tamthilia ya Nguzo Mama vipengele mahususi hivyo ni mandhari ,matumizi ya mwanga, matumizi ya muziki na nyimbo, ubunifu na muonekano wa wahusika jukwaani, matumizi ya mhusika sauti- kivuli, vitendo vya wahusika jukwani na matumizi ya maleba. Pamoja na vipengele mahususi hivyo vilivyojibainisha katika tamthilia ya Nguzo Mama, kuna namna anuai za mwitiko ambazo hadhira katika tamthilia ya Nguzo Mama waliweza kubainisha. Nazo ni mwitiko wa moja kwa moja kama kuimba, kushiriki katika mazungumzo na wahusika jukwaani, mfano pale hadhira iliposhirikishwa na mhusika msimulizi kusimulia hadithi mwanzo na mwisho wa hadithi ya kijiji cha Patata ambako Nguzo Mama imelala, kupiga makofi, kucheka na kushangilia ili kuonyesha ushabiki kwa wahusika jukwaani, kulia na kutoa machozi katika matukio yaliyoleta huzuni moyoni . Pia upo mwitiko usio wa moja kwa moja ambapo hadhira hufanya kama kuonyesha hisia za moyoni na akilini. Aidha uchambuzi wa tamthilia ya Nguzo Mama umebaini kuwa, kuna dhima kubwa ya mwitiko wa hadhira ya mchezo wa tamthilia jukwaani. Dhima hiyo ni pamoja na kuwaimarisha wahusika watendaji jukwaani moja kwa moja kupitia mazungumzo na vitendo vya hadhira kama tulivyoona katika miitiko yao. Pia kuongeza uhai wa mchezo wa tamthilia ambao huhitaji fanani / au na wahusika na hadhira, maneno na vitendo vya papo kwa papo. Dhima nyingine ni kuvuta usikivu wa hadhira kwa kujua kuwa anashiriki katika kukamilisha mchezo jukwani kumpa hadhira uwezo wa kukabiliana na kazi ya fasihi toka mwanzo hadi mwisho wa onyesho jukwaani hatimaye kuelewa au kupata maana ya kazi ya fasihi kulingana na muktadha wa hadhira yenyewe bila kutazamishwa na mwandishi au mhakiki wa tamthilia husika. Mwisho limetolewa hitimisho la utafiti mzima pamoja na mapendekezo ya maeneo yanayohitaji kutafitiwa zaidi ili kuweza kukuza uwanja wa mwitiko wa hadhira ya tamthilia na fasihi kwa ujumla.
Description
Available in print form
Keywords
Swahili drama, Nguzo mama
Citation
Msemwa, K. (2012).Mwitiko wa hadhira ya tamthilia: mifano toka tamthilia ya nguzo mama. Master dissertation, University of Dar es Salaam. Available at (http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)