Mabadiliko ya kifonolojia katika nomino za Kiswahili zilizotoholewa kutoka lugha ya Kiingereza: mifano kutoka kamusi ya kiingereza - Kiswahili (TUKI, 2006) na kamusi ya isimu na falsafa ya lugha (Massamba, 2016)
Loading...
Date
2019
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Lugha ya Kiswahili ina sauti zake, miundo yake ya silabi na mfuatano wa sauti unaotofautiana na ule wa lugha ya Kiingereza. Hivyo basi, nomino zinapotoholewa kutoka lugha ya kiingereza kuingia katika Kiswahili hulazimika kufanyiwa mabadiliko ili ziendane na mahitaji ya fonolojia ya lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, utafiti huu unachunguza mabadiliko ya kifonololojia katika nomino za Kiswahili zilizotoholewa kutoka lugha ya kiingereza zilizomo katika kamusi ya kiingereza-kiswahili (TUKI, 2006) na kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (Massamba, 2016). Data ya utafiti huu ilikusanywa kutoka maktabani na uwandani. Data ya maktabani ilikusanywa kutoka katika kamusi teule kwa kutumia mbinu ya usomaji makini na data ya uwandani ilikusanywa kutoka kwa wanafunzi wa Shahada ya Awali katika Kiswahili mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kutumia mbinu ya usaili na kurekodiwa kwa kinasasauti. Data hii ilichambuliwa na kuchanganuliwa kwa mkabala wa kimaelezo ambapo yalitolewa maelezo ya ufafanuzi wa mabadiliko ya kifonolojia katika nomino za Kiswahili zilizotoholewa kutoka lugha ya kiingereza. Aidha, programu ya praat nayo ilitumika kuchambua mabadiliko ya wakaa na mkazo katika nomino hizo na kuonesha uchambuzi huo kwa kutumia vielelezo. Uchambuzi wa data ya utafiti huu uliongozwa na misingi na mihimili ya kiunzi Rasmi cha Fonolojia zalishi kinachosisitiza matumizi ya sheria na kanuni za ukokotozi wa vipengele vya lugha. Imebainika kuwa nomino za Kiingereza zinapotoholewa katika lugha ya Kiswahili hufanyiwa mabadiliko ya kifonimu na kiarudhi ili ziendane na sarufi ya lugha ya Kiswahili. Mabadiliko ya kifonimu yaliyobainika ni ubadilikaji wa sauti (yaani konsonanti na irabu), usahilishaji wa irabuunganifu, udondoshaji wa sauti, uchopekaji wa irabu, uongezaji wa silabi mwishoni mwa nomino na usififishaji wa konsonanti. Aidha, utafiti huu unaeleza kuwa ili kugundua mabadiliko ya kifonimu katika maneno yanayotoholewa ni vema tuchunguze matamshi na wala siyo othografia ya maneno hayo. Kwa upande wa viarudhi, tumechunguza wakaa na mkazo. Imebainika kuwa nomino za kiingereza zinapotolewa katika lugha ya Kiswahili hufupishwa irabu ya silabi ya mwisho na irabu ya silabi nyinginezo zenye irabu ndefu kabla ya kutoholewa \, isipokuwa katika silabi yenye mkazo msingi, ingawa, pia kuna vighairi vichache vinajitokeza na kukata kanuni hii. Pia nomino za kiingereza zinapotoholewa katika lugha ya Kiswahili hurefushwa irabu ya silabi ya pili kutoka mwisho. Vilevile, mkazo husogezwa katika silabi ya pili kutoka mwisho kutoka katika silabi nyingine ulipokuwa kabla ya kutoholewa. Utafiti huu unaweka bayana kuwa nomino moja huweza kupitia badiliko zaidi ya moja kutegemeana na namna vijenzi vyake vinahitaji mabadiliko hayo husababishwa uhitaji wa kufidia sauti za kiingereza zisizopatikana haja ya kukidhi matakwa ya matamshi ya lugha ya Kiswahili, haja kudhibiti muundo wa silabi funge na mkururo wa sauti utokanao na maneno ya kiingereza zilizopatikana katika lugha ya Kiswahili, urahisishaji wa matamshi wa nomino zinazotoholewa, haja ya kukidhi matakwa ya matamshi ya lugha ya Kiswahili, haja kudhibiti muundo wa silabi funge na mkururo wa sauti utokanao na maneno ya kiingereza na kubadilika kwa lafudhi ya utamkaji. Aidha, utafiti huu umependekeza maeneo mengine yanayohitaji utafiti zaidi, hususan katika kipengele cha urefushaji wa irabu katika vitenzi vilivyotoholewa kutoka lugha za kigeni. Pia, utafiti huu umependekeza namna ya kuzifanyia marekebisho baadhi ya nomino ambazo utohozi wake haukuzingatia utamkaji sahihi wa lugha ya Kiswahili.
Description
Available in print form, East Africana collection, Dr. Wilbert Chagula Library, class mark (THS EAF PL8701.T34N385)
Keywords
Language and languages, Language and acquisition, Swahili language, English language, Phonology, Nouns, Dictionary
Citation
Ndumiwe, Elishafati Jonathan (2019) Mabadiliko ya kifonolojia katika nomino za Kiswahili zilizotoholewa kutoka lugha ya Kiingereza: mifano kutoka kamusi ya kiingereza - Kiswahili (TUKI, 2006) na kamusi ya isimu na falsafa ya lugha (Massamba, 2016), Tasnifu ya MA (Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.