Dhima ya sifo za kijadi katika harusi : Uchunguzi wa Majigambo katika Sherehe za Harusi za Waha

Date

2012

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu ulilenga kuchunguza dhima ya sifo za kijadi katika harusi za Waha wa Kibondo kwa kuchunguza majigambo yanayotambwa katika sherehe za harusi za kabila hilo. Tafiti nyingi kuhusu sifo za kijadi (Vail na White, 1991) zinadai kuwa dhima ya sifo za kijadi katika jamii za Kiafrika ilikuwa ni kudumisha ushujaa, uhodari na ujasiri wa wanaume katika kuimarisha mamlaka ya utawala wa chifu au mtemi. Aidha, kutokana na uchunguzi wetu katika jamii ya Waha, hasa wa wilaya ya Kibondo, tumebaini kuwa utanzu huo wa sifo za kijadi (yaani majigambo) ulikuwa ukijitokeza sana katika michakato kadhaa iliyoambatana na sherehe za harusi, kwa mfano, wakati wa kutoa na kupokea mahari, wakati wa kukabidhiana mke, wakati wa safari ya kuelekea nyumbani kwa muoaji, na kadhalika. Muktadha wa harusi ulitufanya tujiulize kuwa, kama utanzu wa sifo za kijadi ulikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mamlaka za kitawala kama zisemavyo tafiti nyingine, je, sifo za kijadi zilizokuwa zinatambwa katika sherehe za harusi zilikuwa zinaingia wapi? Hili lilikuwa ni tatizo la kinadharia lililohitaji kutatuliwa kitafiti hasa kwa kuchunguza dhima ya sifo za kijadi katika muktadha huu tofauti. Tulianza kwa kufanya utafiti wa maktabani, baadaye tukaenda kukusanya data za uwandani katika kata sita za wilaya ya Kibondo. Vifaa vilivyotumika katika kukusanya data ni pamoja na shajara, kalamu na daftari, kamera ya picha tuli na sogezi, pamoja na kompyuta. Pia data zilipatikana kwa mbinu ya kuunda muktadha wa majigambo tendwa (baada ya kukosa matukio ya harusi yenye utambaji halisi wa majigambo), kufanya usaili/mahojiano binafsi, na majadiliano ya vikundi. Data zilichakatwa na kuchambuliwa kwa kuongozwa na mwega wa nadharia ya Uhalisia na mkabala wa Kisosiolojia. Baada ya hatua zote hizo, tumebaini kuwa majigambo katika harusi za Waha yalikuwa na dhima ya kuchochea ushujaa katika jamii, kukuza na kueneza itikadi ya udume, kutunza kumbukumbu ya mambo muhimu katika jamii, kuwezesha mazungumzo ya kijadi, kuburudisha hadhira, kuonesha kuridhika, kuonesha moyo wa shukurani kwa wazazi na jamii, kutoa tangazo la uhalali wa ndoa, kujitambulisha kinasaba, kuashiria furaha kutoka moyoni, kuenzi wahenga wa jadi, kuonesha kujali mke, kutegua mikosi njiani, kumfanya mwari awe mtii kwa mume wake, kuonesha uelekeo katika safari na kuhifadhi lugha ya Kiha katika uasilia wake. Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa sifo za kijadi katika jamii ya Waha, hasa wa Kibondo, hazikuwa na dhima ya kuimarisha utawala wa mtemi au chifu. Kwa jamii ya Waha, sifo zilikuwa zinawahusu watu wote kutokana na miktadha mbalimbali. Mwisho, baada ya kuwasilisha na kuchambua matokeo ya utafiti, tumejadili na tukatoa mapendekezo juu ya nini kifanyike zaidi kutokana na matokeo hayo.

Description

Available in print form

Keywords

Waha (African people), Wedding ceremonies, Tanzania

Citation

Herman, L.(2012). Dhima ya sifo za kijadi katika harusi : Uchunguzi wa Majigambo katika Sherehe za Harusi za Waha. Master dissertation, University of Dar es Salaam. Available at (http://41.86.178.3/internetserver3.1.2/detail.aspx)