Vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani ya Mrisho Mpoto “mjomba”

Loading...
Thumbnail Image
Date
2018
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu unahusu vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani ya Mrisho Mpoto. Lengo ni kuchunguza vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani ya Mrisho Mpoto na dhima yake. Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha vipengele mahususi vya kifani na kimaudhui vya fasihi ya majaribio vinavyojitokeza katika maghani ya Mrisho Mpoto na kueleza dhima ya kutumia vipengele hivyo katika maghani hayo. Data za utafiti huu zilikusanywa kutoka maghani teule ya Mrisho Mpoto maarufu kama “Mjomba”. Maghani hayo ni matano ambayo ni Nikipata Nauli, Uhuru Wangu Mwanahabari, Chocheeni Kuni, Deni la Hisani na Sizonje. Katika ukusanyaji wa data za utafiti huu mbinu ya maktabani imetumika na ilihusisha usomaji, usikilizaji na utazamaji wa kanda za video na audio za maghani teule kwa lengo la kubainisha vipengele vya kifani na kimaudhui vya fasihi ya majaribio vilivyojitokeza katika maghani hayo huku tukieleza dhima ya kutumia vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani hayo. Uchambuzi wa data za utafiti umefanyika kwa kutumia misingi ya Nadharia ya Usimulizi. Misingi ya Nadharia ya Usimulizi iliyotumika imedondolewa kutoka katika kiunzi cha Nadharia ya Naratolojia kama kilivyoasisiwa na Aristotle kutoka katika kazi kuu ya Poetics (335 KK) na kuendelezwa na Todorov (1969). Nadharia hii imesaidia kubainisha vipengele vya kifani na kimaudhui vya fasihi ya majaribio katika maghani ya Mrisho Mpoto na kueleza dhima ya kutumia vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani hayo. Uchunguzi uliofanyika katika utafiti huu umedhihirisha kuwa maghani teule ya Mrisho Mpoto yamesheheni vipengele vya fasihi ya majaribio vya kifani na kimaudhui. Kwa upande wa fani kuna muundo wa kuanza na kiitikio-simulio-kiitikio, na muundo wa usimulizi wenye uchanganyaji nafsi. Kwa upande wa mtindo kuna kuingiliana kwa tanzu, na kuchanganya kuimba na kuongea. Aidha, kwa upande wa utendaji imebainika kuwa maghani haya hayatungwi papo kwa hapo hutendwa kwa malipo na bila ya kuwapo kiongozi kama hadhira na ni mali ya mtu binafsi, fanani hawezi kubadili matini papo kwa hapo. na hadhira hushindwa kushiriki ipasavyo. Kwa upande wa maudhui, dhamira zilizobainika ni: dhamira ya fantasia na mizungu, dhamira mpya/za kidunia ambazo ni: haki za binadamu, haki za wanyama, haki na uhuru wa kupashana habari, uvunjifu wa sheria, ubadhirifu/ufisadi, ukosefu wa ajira, ulinzi wa maliasili na, utandawazi, dhamira ya ukengeushi, kejeli kwa viongozi wa serikali na wanahabari, ukoloni mamboleo, matabaka, na ukosefu wa ajira. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa, matumizi ya vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani teule ya Mrisho Mpoto yamesaidia kueleza dhima ya fasihi ya majaribio kifani na kimaudhui. Kujitokeza kwa vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani teule ya Mrisho Mpoto, ambayo ni utanzu wa fasihi simulizi, kumesaidia kubaini kuwa fasihi ya majaribio inajitokeza pia katika fasihi simulizi.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8704.T34C53)
Keywords
Swahili literature, Swahili language, Swahili poetry, Maghani ya Mrisho Mpoto, Mjomba
Citation
Chagulani, A. I. (2018). Vipengele vya fasihi ya majaribio katika maghani ya Mrisho Mpoto “mjomba” Tasnifu ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.