Ukiushi wa kaida za kluandishi katika fasihi andishi ya kiswahili: uchunguzi ktfani katika kazi teule

Loading...
Thumbnail Image
Date
2018
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu umekusudia kuchunguza ukiushi wa kaida za kivandishi katika fasihi andishi ya Kiswahili. Kaida za kivandisi ni kanuni ambazo waandishi wanapaswa kuzizingatia katika uandishi wao, ukiwamo uandishi wa kazi za kifasihi. Ukiushi ni dhana inayomaanisha kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa. Kwa muktadha huu, ukiushi wa kaida za kivandishi ni kuandika kwa kutumia baadhi ya kanuni za kivandishi kinyume au tofauti na vile ambavyo taratibu zinaelekeza. Kuna mgongano wa kimawazo baina ya asasi na waandishi wanaoshughulika na nadharia ya uandishi kwa upande mmoja na wananadharia wa uandishi wa kifasihi kwa upande mwingine. Wakati asasi na waandishi hao wanaoshughulikia nadharia ya uandishi wakisisitiza kuzingatia kanuni za kivandishi katika uandishi ukiwamo ule wa kazi za kifasihi, baadhi ya waandishi wanaoshughulika na uandishi wa kifasihi wanabainisha kuwa katika uandishi wa kifasihi si lazima kuzingatia kaida za kivandishi. Matilaba ya utafiti huu ni kuangalia ukiushi wa kaida hizo za kivandishi na nafasi yake katika uandishi wa kifasihi. Utafiti huu umechunguza ikiwa ukiushi wa kaida za kivandishi unaofanywa na baadhi ya waandishi wa kazi za kifasihi ni ubanangaji katika uandishi au una kusudio fulani maalumu. Kwa hivyo, katika utafiti huu tumechunguza ukiushi huo kwa malengo makuu ya kubaini sababu na dhima ya ukiushi huo katika fasihi andishi. Katika kufanya hivyo, tumetumia kazi teule za fasihi andishi ya Kiswahili, moja kutoka kila kumbo ya fasihi andishi yaani tamthiliya, riwaya na ushairi. Kazi teule zilizotumika kupata data ya msingi ya utafiti huu ni tamthiliya ya Kinjeketile (Hussein, 1969), riwaya ya Nyota ya Rehema (Mohamed, 1976/2004) na diwani ya Kaza Macho (Wamitila, 2014). Utafti huu umeongozwa na Nadharia ya Usanifishaji (BAKITA, 2013) na Nadharia ya Mchomozo (Leech na Short, 1981) na Leech (2013). Data za utafiti huu zimekusanywa maktabani wilayani Ubungo, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mtafiti ametumia mbinu ya usomaji matini na uchambuzi wa matini teule. Kwa kutumia nadharia tajwa, utafiti huu umeweza kubaini dhima mbalimbali za ukiushi wa kaida za kivandishi katika fasihi andishi ya Kiswahili. Dhima hizo ni: Ukiushi huvuta umakini, hushtua na kuibua hisia za msomaji, huweka msisitizo au uzito katika maudhui yanayowasilishwa, husaidia kuibua maudhui kwa uwazi na urahisi, huakisi mandhari halisi ya utokeaji wa tukio, hubainisha mtindo wa mwandishi, hufanya kazi ya kifasihi kuwa na mvuto wa pekee/ujumi, na kuonesha asili au tabaka la watumiaji wa lugha. Dhima nyingine za ukiushi wa kaida za kivandishi ni: Kuleta athari ya kisaikolojia kwa hadhira, kujenga dhana ya ukubwa, idadi na kuonesha hall isiyo ya kawaida katika maudhui yanayowasilishwa, na kutofautisha kauli na hall mbalimbali za mhusika/wahusika ndani ya kazi ya kifasihi. Ingawa ukiushi wa kaida za kivandishi umekuwa ukichukuliwa kama ubanangaji wa lugha na baadhi ya watu, katika utafiti huu tumebaini kuwa ukiushi ni kipengele muhimu cha kimtindo ambacho kina dhima mbalimbali muhimu katika kazi andishi kulingana na matakwa ya mwandishi, hususani katika kazi za kifasihi andishi. Kwa hivyo, ni wajibu wa asasi zinazoshughulika na lugha, wataalamu wa nadharia ya uandishi, wasomaji, wahariri na mashirika ya uchapishaji kutambua kwamba ukiushi si ubanangaji wa lugha bali ni kipengele muhimu cha kimtindo katika uandishi chenye dhima anuwai kifani na kimaudhui katika kazi za kifasihi
Description
Available in print form, Dr. Wilbert Chagula Library, EAF collection, class mark (THS EAF PL8703.5.T34D88 )
Keywords
Swahili literature, Uchunguzi kifani katika kazi teule
Citation
Duwe, E.J ( 2018 ) Ukiushi wa kaida za kluandishi katika fasihi andishi ya kiswahili: uchunguzi ktfani katika kazi teule, Masters dissertation, university of Dar es Salaam, Dar es Salaam