Tofauti za visawe vya nomino za Kiswahili kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Loading...
Thumbnail Image
Date
2016
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu unahusu tofauti za visawe vya nomino za Kiswahili kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Data iliyojadiliwa katika utafiti huu imekusanywa kutoka Mikoa mitatu, ambayo ni Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania Bara, na kwa upande wa Zanzibar ni Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Kusini Pemba. Pia, malengo mahususi matatu yameainishwa ambayo ni: Kuainisha aina za visawe vya nomino za Kiswahili ambao unapatikana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kujadili sababu zinazochangia tofauti za visawe hivyo pamoja na kufafanua athari zinazoweza kujitokeza kutokana na tofauti hizo. Utafiti huu umehusisha watoa taarifa 25 kutoka kila mkoa na kufanya sampuli kuwa na watoa taarifa 75. Data za utafiti huu zimekusanywa maktabani na uwandani ambapo kwa upande wa data za uwandani mbinu za hojaji na usaili zimetumika. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Uhusiano wa Maana iliyoasisiwa na Lyons inayodai kuwa, hakuna vipashio vinavyoweza kuwepo nje ya uhusiano wa vipashio vingine, ambapo nadharia hii imetoa uangavu mkubwa katika kuchanganua vipashio vinavyohusiana na kutofautiana katika utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba kuna visawe kamili na visawe visivyo kamili, ambapo visawe kamili vinaweza kutoana katika mazingira yote, wakati visawe visivyo kamili haviwezi kutoana sehemu zote katika tungo. Miongoni mwa sababu zilizojadiliwa ambazo husababisha tofauti za msamiati wa visawe ni pamoja na ukopaji wa msamiati, makundi rika katika jamii na jinsia, tofauti za kilahaja na mwingiliano wa lugha moja na nyingine. Vilevile, utafiti umebaini kuwepo kwa tofauti hizo kuna athari ambazo zinajitokeza zikiwemo kutoelewana, utambulisho, kukua kwa lugha na mfumuko wa visawe. Aidha, katika utafiti huu, yametolewa mapendekezo kadhaa. Kwanza, utafiti unaweza kufanywa kwa kuchunguza kategoria nyingine za maneno kama vile: vitenzi, vielezi, viunganishi, vihusishi na vihisishi ili kubaini iwapo kuna tofauti za kimatamshi, maumbo na matumizi ya maneno katika lugha ya Kiswahili kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Pili, utafiti kama huu unaweza kufanywa katika maeneo mengine yanayotumia lugha hii kama vile Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Visiwa vya Komoro. Tatu, uchunguzi unaweza kufanywa ili kubaini maneno ambayo yana maumbo sawa lakini yana maana tofauti kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8702.584)
Keywords
Swahili language, Grammar, Nouns, Zanzibar, Tanzania Bara
Citation
Suleiman, H. A. (2016). Tofauti za visawe vya nomino za Kiswahili kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Tasnifu ya Uzamili, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.