Muundo wa silabi katika kimashami

No Thumbnail Available
Date
2014
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
University of Dar es Salaam
Abstract
Utafiti huu ulihusu Muundo wa Silabi za Kimashami kwa kutumia Nadharia ya UU (McCarthy na Prince, 1993; Smolensky na Prince, 1993). Utafiti huu ulifanyika ili kupunguza pengo la uhaba wa maandiko ya kiisimu na kuhifadhi maandishi ya Kimashami. Lengo kuu lilikuwa ni kuchunguza muundo wa silabi katika Kimashami. Malengo mahususi yalikuwa ni mawili. Mosi, kubainisha muundo wa silabi katika Kimashami. Pili, kuchunguza michakato ya kifonolojia inayoathiri sauti katika muundo wa silabi za Kimashami. Katika utafiti huu wa muundo wa silabi katika Kimashami data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za mahojiano na kusikiliza na kurekodi matamshi ya wazungumzaji wa Kimashami. Data za utafiti huu zilichanganuliwa kwa mbinu ya maelezo na majedwali. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa Kimashami kina aina kumi za miundo ya silabi ambazo kwa kuzingatia kigezo cha uzito wa silabi zimegawanywa katika makundi mawili ambayo ni muundo wa silabi nyepesi na muundo wa silabi nzito. Aidha, matokeo ya utafiti yalionyesha kuwepo kwa michakato mbalimbali ya kifonolojia inayoathiri sauti katika muundo wa silabi za Kimashami. Michakato hii ni pamoja na udondoshaji wa irabu, uyeyushaji, muungano wa irabu, uchopezi na unazalishaji. Michakato mingine ni ile inayoathiri sauti za konsonanti ni utamkiaji pamwe wa nazali, udondoshaji mwanzo na usilabishaji wa nazali. Kwa mujibu wa utafiti huu michakato hii huwa inajitokeza katika Kimashami ili kulinda mfuatano wa mashartizuizi ya matamshi ya Kimashami. Vilevile katika utafiti huu ilibainika kuwa michakato inayoathiri sauti za irabu katika muundo wa silabi za Kimashami ni mingi zaidi ikilinganishwa na ile inayoathiri konsonanti. Aidha, muundo wa silabi katika lugha hii, kama ilivyo kwa lugha nyingine za Kibantu, hauishii na konsonanti (HKODA), ni huru. Kisha utafiti huu ulipendekeza kuufanyika utafiti mwingine wa vingele vya fonolojia ya Kimashami kama vile toni, wakaa wa irabu, mkazo, uhusiano baina ya silabi na nguvumsikiko, uhusiano baina ya muundo wa silabi na toni na dhima ya vipamba sauti. Aidha, maeneo mengine ya isimu ni sintaksia, mofolojia, leksikografia, pragmatiki na semantiki ya Kimashami.
Description
Available in print form, East Africana Collection, Dr. Wilbert Chagula Library, Class mark (THS EAF PL8481.4.J82 )
Keywords
Mashami language, Language, Tanzania, Hai district, Kilimanjaro region
Citation
Judica, E. (2014) Muundo wa silabi katika kimashami, Master dissertation, University of Dar es Salaam. Dar es Salaam.