Idhini ya kishairi na mchango wake katika kuibua maudhui na fani katika ushairi: uchunguzi wa kazi teule za M.M. Mulokozi.
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuchunguza idhini ya kishairi inavyochangia kuibua maudhui na fani katika ushairi kwa kutumia kazi teule za ushairi za M.M. Mulokozi katika Kunga za Ushairi na Diwani Yetu (1979) na Utenzi wa Nyakiiru Kibi. Malengo mahususi ya utafiti huu ni kubainisha idhini za kishairi, kueleza mchango wake katika kuibua vipengele vya kimaudhui ambavyo ni dhamira, ujumbe na mgogoro. Kadhalika, utafiti huu ulilenga kufafanua mchango wa idhini ya kishairi katika kujenga vipengele vya kifani katika ushairi teule hususan vina na mizani. Utafiti huu ni wa maktabani. Mbinu zilizotumiwa na mtafiti katika ukusanyaji wa data ni pamoja na usomaji wa mashairi na tenzi teule kwa kuzingatia usomaji unavyomwathiri msomaji katika kupata yaliyomo katika matini ya kifasihi. Mbinu nyingine ni kupitia maandiko mbalimbali maktabani. Katika uchambuzi wa data za vipengele vya kimaudhui, mtafiti ametumia Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji iliyoelezewa na Iser (1978) na Fish (1980). Wataalamu hawa wanaeleza kuwa mwitiko wa msomaji humwathiri msomaji kwa kumpa uwezo wa kuibuni maana, kumtofautisha msomaji mmoja na mwingine katika kuelewa maana katika kazi ya kifasihi na humjengea maarifa mapya msomaji wa matini ya fasihi. Katika fani mtafiti ameongozwa na nadharia ya Umuundo iliyoendelezwa na Culler (1975), Hawkes (1977) na Eagleton (1999). Wataalamu hawa wanaeleza kuwa kazi za fasihi upande wa ushairi kifani zina muundo na mpangilio mahsusi wa sauti, wizani na sarufi. Mtafiti ameongozwa na nadharia hii kuchunguza namna idhini ya kishairi inavyochangia kuibua vipengele vya kifani hususan vina na mizani katika kazi teule. Utafiti huu umeonesha kuwa idhini ya kishairi inamwezesha mshairi kupata maneno anayohitaji kwa kubadili maneno kisintaksia au kimofolojia kwa kutumia mbinu mbalimbali. Mathalani, mtafiti amegundua kuwa mtunzi wa kazi teule za utafiti huu ametumia mbinu kama ukiushi, unyambulishaji, uambishaji na uazimaji maneno kuunda idhini za kishairi ambazo zinachangia kuibua vipengele vya maudhui kama dhamira, ujumbe na migogoro katika ushairi teule. Kadhalika, mbinu hizo zimetumika kuunda idhini za kishairi zinazochangia kuibua vipengele vya fani hususan vina na mizani. Katika utafiti huu mtafiti ametumia mkabala wa kitaamuli. Vifaa muhimu vilivyotumika katika utafiti huu ni kompyuta pakatwa, kinyonyi, kalamu na karatasi. Utafiti huu umethibitisha kuwa mtunzi anapobuni idhini ya kishairi inachangia kuibua vipengele vya maudhui na vipengele vya fani. Matokeo ya utafiti yameonesha kufikiwa kwa lengo la kwanza la kubainisha idhini za kishairi zilizotokana na ukiushi wa kisarufi, ukiushi katika maneno kutoka lugha za asili hususani Kihaya na kuchanganya maneno kutoka lugha za kigeni. Pia, matokeo ya utafiti huu yameonesha kufikiwa kwa lengo la pili kwa kuonesha mchango wa idhini za kishairi katika kuibua vipengele vya maudhui ambavyo ni dhamira, ujumbe na migogoro. Vilevile, matokeo ya utafiti huu yamewezesha kufikiwa kwa lengo la tatu la kufafanua idhini ya kishairi zilivyochangia kuibua vipengele vya fani katika ushairi ambavyo ni vina na mizani. Utafiti huu umetoa mapendekezo kadhaa kuhusu idhini ya kishairi kwa watunzi, waandishi, wahakiki na watafiti kuwa idhini ya kishairi ni kipengele kinachohitaji kutafitiwa na kuandikwa zaidi.