Institute of Kiswahili Studies
Permanent URI for this community
Browse
Browsing Institute of Kiswahili Studies by Subject "Africa"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Ujitokezaji wa falsafa ya Kiafrika katika Riwaya za kiethnografia za Kiswahili(University of Dar es Salaam, 2019) Mpalanzi, LameckUtafiti huu unachunguza ujitokezaji wa vipengele vya falsafa ya Kiafrika katika riwaya teule za kiethnografia za Kiswahili. Vipengele vilivyochunguzwa ni dini ya jadi, uganga na uchawi, uzazi, uhai na kifo na uduara wa maisha. Katika kuchunguza vipengele hivyo, riwaya zilizoteuliwa na kuchambuliwa ni Kurwa na Doto, Mirathi ya Hatari na Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka; Ntulanalwo na Bulihwali. Vilevile, utafiti ulilenga kubainisha namna vipengele teule vilivyomo katika riwaya vinavyoakisiwa katika jamii teule za Unguja, Njombe na Ukerewe. Aidha, utafiti ulilenga kuchunguza mwingiliano wa riwaya ya kiethnografia ya Kiswahili na falsafa ya Kiafrika. Kadhalika, utafiti unafafanua mehango wa falsafa ya Kiafrika katika maendeleo ya fani na maudhui ya riwaya teule. Katika kukamilisha malengo haya, data ilikusanywa maktabani na uwandani kwa kutumia mbinu ya udurusu wa maandiko maktabani, mahojiano, hojaji, ushuhudiaji na ushiriki. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili kuanzia nyakati za ukusanyaji data hadi uchambuzi. Nadharia ya kwanza inaitwa Ontolojia ya Kibantu, na ya pili Sosholojia ya Fasihi. Ontolojia ya Kibantu ilituongoza kuchambua masuala yanayohusu falsafa yaKiafrika na Sosholojia ya Fasihi ilitusaidia kuhakiki masuala yanayohusu uhusiano wa fasihi na jamii. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa fasihi hubeba falsafa ya jamii kwa kuwa vipengele teule vya falsafa ya Kiafrika vinadhihirika bayana katika riwaya teule. Utafiti umethibitisha kuwa tambiko linachukua sehemu kubwa ya dini ya jadi, ambayo ndiyo mzizi wa imani ya Waafrika. Jamii hizi zina matambiko mengi, mathalani, jamii ya Wamakunduchi ina tambiko is Mwaka-kogwa, tambiko la kumaliza msiba,tambiko la uzazi, tambiko la unyago na tambiko la mazishi. Jamii ya Wabena ina tambiko la kafara (Kipongo), Nyumbanitu na Amalimilo. Kwa upande mwingine, Wakerewe wana tambiko la kuzaliwa, uzazi na kutanabahi katika pembe, tambiko la kumtoa mtoto nje,tambiko la harusi, tambiko la kuvundika ndizi, tambiko la ugonjwa na tambiko la mazishi. Pia, Wakerewe, wana tambiko la machifu huko Kitare, tambiko katika makumbusho ya Handebezyo na katika "Jiwe Linalocheza." Utafiti umebaini kuwapo kwa imani mseto katika jamii teule inayotokana na mwingiliano wa dini ya jadi na dini za kigeni. Kuwapo kwa imani mseto ni jitihada za jamii teule kutafuta utambulisho na ukubalifu wa kila kundi. Utafiti umebaini kuwa upo mpaka bayana kati ya fani ya uganga na uchawi kwa kuzingatia kigezo cha utendaji, dhima, kiwango cha nguvu-hai, miiko na ufantasia wa fani hizo. Uchunguzi katika riwaya na jamii teule umebaini kuwapo kwa makundi kumi (10) ya waganga na makundi mawili (2) ya wachawi. Utafiti unaonesha kuwa baadhi ya waganga na wachawi wanaishi maisha duni kwa kuwa hutumia gharama kubwa kununua viambato vya uganga na uchawi. Licha ya kufumbata falsafa mbalimbali za maisha, suala la uzazi katika jamii ya Ukerewe ni mfano dhahiri wa kuwapo kwa familia pana ya Kiafrika inayojumuisha watu-hai, waft' na watakaozaliwa. Sanjari na hilo, utafiti huu unaafiki kuwa kifo kwa Mwafrika si mwisho wa maisha kwani mfu huendelea kuwapo kama inavyoelezwa katika Ontolojia ya Kibantu. Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa maisha ya maana na halisi ni ya hapa duniani. Aidha, utafiti huu ulibaini kuwapo kwa uhusiano wa kiduara kati ya mtu, jamii na mfumo uliopo. Kiontolojia, utafiti umethibitisha kuwapo uhusiano wa kiduara kati ya Mungu, mizimu, wahenga, binadamu, wanyama na mimea, na vitu na mahali. Katika kudhihirisha fasihi inavyobeba falsafa ya jamii, utafiti huu umetambua kuwa fasihi na falsafa ya Kiafrika hutenda majukumu yanayofungamana. Mwisho, utafiti huu unabainisha kuwa falsafa ya Kiafrika ni malighafi na nyenzo muhimu katika uandishi wa fani na maudhui ya riwaya ya Kiswahili.Item Usawiri wa dini ya asili katika kazi za fasihi andishi ya kiswahili mifano kutoka kazi za Kitereza (1980) na Ruhumbika (2001)(University of Dar es Salaam, 2014) Selestine, SeveraUtafiti huu unahusu usawiri wa dini ya asili katika kazi za fasihi andishi ya Kiswahili. Pamoja na ushahidi wa wanazuoni mbalimbali waliotafiti dini ya asili katika muktadha wa kijamii na namna ilivyorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kwa njia ya fasihi simulizi, hakuna utafiti ulioangalia kwa kina jinsi dini ya asili ilivyosawiriwa katika kazi za fasihi andishi ya Kiswahili, hususani riwaya. Hivyo, utafiti huu ulikusudia kutafiti usawiri wa dini ya asili kama dhamira katika fasihi andishi ya Kiswahili kwa kutumia mifano kutoka riwaya za Bw. Myombekere na Bi. Bugonoka na Ntulwanalwo na Bulihwali na Janga Sugu la Wazawa. Utafiti huu ulitumia nadharia ya Ontolojia ya Kibantu kama mwongozo katika uchambuzi wa data msingi zilizopatikana katika riwaya mbili zilizotumika katika utafiti huu. Ili kushadidia dhamira zilizojadiliwa kutoka katika riwaya teule, watu kumi na wanane kutoka katika kabila la Wakerewe walihojiwa. Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa, dhamira ya dini ya asili imesawiriwa kwa kujengwa na dhamira kuu ya uzazi unaosawiriwa kama ufufuko unaounganisha wafu na walio hai. Dhamira ya uzazi inakamilishwa na dhamira nyingine za kifo na uhai, matambiko, mwonekano wa mizimu na uganga. Dhamira hizi zimesawiriwa zikihusisha kufa kwa mwanadamu na kuzaliwa tena au kufa na kuendelea kuwako katika ulimwengu wa mizimu na mawasiliano kati ya wafu na walio hai. Ndoa imeoneshwa kama hatua muhimu ya chanzo cha uzazi na mwendelezo wa ukoo. Hivyo, utafiti umebaini kuwa usawiri wa dini ya asili katika riwaya teule ulilenga kutoa elimu kuhusu dini ya asili na kuihifadhi kama utambulisho na amali muhimu kwa Waafrika hususani Wakerewe. Utafiti pia umebaini usawiri wa dhamira ya dini ya asili umefanyika katika hali ya kuonesha changamoto zinazoikabidhi, mojawapo ikiwa matumizi ya dini ya asili kama chombo cha kuleta maovu katika jamii hasa inapochanganywa na dini za kigeni kama Ukristo na Uislamu.