Lugha inayotumika katika masoko ya nguo za mitumba jijini Dar es salaam

Date

2013

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

University of Dar es Salaam

Abstract

Utafiti huu umeshughulikia lugha inayotumika katika masoko ya nguo za mitumba jijini Dar es Salaam. Malengo ya utafiti huu yalikuwa manne. Mosi, kubainisha sifa za pekee za lugha hiyo. Pili, kueleza sababu zinazoibua uwepo wa matumizi hayo ya lugha katika masoko ya nguo za mitumba. Tatu, kuonyesha umuhimu wa lugha hiyo katika kuitambulisha na kuifanikisha biashara na nne, kubashiri mchango wa biashara hiyo katika kukuza au kudumaza lugha ya Kiswahili. Utafiti umefanyika Dar es Salaam katika masoko ya Kongo-Kariakoo, Mwenge, Ilala-Boma, Mchikichini, Tandale, Manzese na Tandika. Data ya utafiti huu ilipatikana kwa mbinu za kushuhudia, hojaji na dodoso. Kutoka uwandani tulipata jumla ya msamiati mia moja na tisini na tatu (193) uliokusanywa kisha kuchanganuliwa ili kubaini sifa za lugha ya nguo za mitumba. Ushuhudiaji ulimsaidia mtafiti kupata data zaidi kuhusu sifa za lugha ambazo ni: matumizi ya misimu, utohoaji, nahau, misemo, methali, ufupishaji, ushairi, monolojia, tashihisi, uradidi na kejeli. Kupitia hojaji na dodoso tuliweza kubaini sababu zinazoibua uwepo wa lugha hiyo kuwa ni: mazingira husika, mitindo ya mavazi, kutaka kuwavuta wateja na kurahisisha mawasiliano na kuokoa muda. Lugha hiyo huitambulisha biashara kwa kupambanua wauzaji na bidhaa. Inaifanikisha biashara kwa kurahisisha uuzaji, kuongeza kipato na kupanua mipaka ya biashara. Aidha biashara ya mitumba inachangia kukuza lugha ya Kiswahili kwa kupanua muktadha wa matumizi, kuongeza watumiaji na kuongeza msamiati katika lugha ya Kiswahili. Kwa upande mwingine lugha inadumaa kwa kuvurugika utaratibu wa sarufi na kuchafuliwa kutokana na matumizi ya lugha isiyo sanifu. Nadharia ya rejesta inayohusu matumizi ya lugha kulingana na muktadha imekidhi utafiti huu kwani tumeweza kubaini na kuonyesha wazi kuwa lugha ya mitumba iko hivyo kutokana na udhibiti wa muktadha wa soko-mitumba. Mchango mpya wa utafiti huu ni kubainishwa kwa rejesta ambayo tumeiita rejesta ya soko-mitumba ambayo ni tofauti na lugha nyingine katika masoko au biashara isiyo ya nguo za mitumba. Utafiti huu unapendekeza kuwa kipengele cha matumizi ya lugha kulingana na muktadha hasa katika masoko mbalimbali kichunguzwe zaidi kwani kuna hazina kubwa ya matumizi ya lugha ambayo inahitaji kuchimbuliwa na kuchunguzwa ili kuidumisha na kuiendeleza lugha adhimu ya Kiswahili.

Description

Available in print form, University of Dar es Salaam at Dr. Wilbert Chagula Library (THS EAF PL8702.N456)

Keywords

Swahili language, Style

Citation

Ngole, C(2013)Lugha inayotumika katika masoko ya nguo za mitumba jijini Dar es salaam, Master dissertation, University of Dr es Salaam, Dar es Salaam