Browsing by Author "Sigimba, Jimson Nasson"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Uainishaji wa ngeli za nomino za kikinga: mtazamo wa kimofolojia na kisemantiki Jimson Nasson Sigimba(University of Dar es Salaam, 2014) Sigimba, Jimson NassonMalengo ya utafiti huu yalikuwa ni kuziainisha ngeli za nomino za Kikinga kwa mtazamo wa kimofolojia na kisemantiki na kujua idadi yake. Aidha, ufafanuzi wa mtawanyiko wa nomino zenye asili moja kisemantiki na dhima zinazojitokeza katika viambishi ngeli vya nomino za Kikinga umeshughulikiwa. Utafiti huu umefanyika katika vijiji vya Ikonda, Iwawa, Tandala na Bulongwa Wilayani Makete ambamo watafitiwa 32 kutoka vijiji hivyo waliteuliwa. Njia za ukusanyaji wa data zilizotumika ni hojaji, mahojiano na ushuhudiaji. Nadharia ya Mofolojia Asilia iliongoza utafiti huu ili kuweza kufafanua dhima mbalimbali zinazojitokeza katika viambishi ngeli vya nomino za Kikinga. Utafiti huu umegawanyika katika sura tano. Sura ya Kwanza inahusu maelezo yahusuyo eneo la utafiti, usuli wa tatizo, mfumo wa sauti za Kikinga, historia ya Wakinga, michakato ya kimofolojia, malengo ya utafiti, maswali na umuhimu wa utafiti na msingi wa nadharia. Katika Sura ya Pili, machapisho mbalimbali yaliyohusu uainishaji wa ngeli katika lugha za Kibantu yamepitiwa ili kuweza kujua namna ya kutafiti mada husika kwa kutumia mbinu za wataalamu waliotangulia. Sura ya Tatu inahusu mbinu za utafiti zilizotumika katika ukusanyaji wa data. Uchanganuzi na uwasilishaji wa data iliyokusanywa uwandani umefafanuliwa katika Sura ya Nne. Katika sura hii ngeli za nomino za Kikinga zimeainishwa kwa kutumia kigezo cha kimofolojia na kisemantiki. Utafiti huu umebaini pia kuwa ngeli za Kikinga huanza na Irabu Tangulizi (IT) kisha kufuatiwa na Kiambishi Ngeli (Kng) na Shina (Sh). Kiambishi ngeli cha nomino (Kng) ndicho kilichotumika kuainisha ngeli za nomino za Kikinga na sio irabu tangulizi (IT). Sura ya Tano imeelezea matokeo ya utafiti, mapendekezo ya tafiti fuatishi na hitimisho. Utafiti huu umebaini kuwa lugha ya Kikinga ina ngeli za nomino 19 kwa mtazamo wa kimofolojia. Pia, imeonekana kuna mtawanyiko wa nomino za Kikinga katika ngeli tofauti tofauti isipokuwa ngeli inayohusu watu, nomino za mkopo, vitu dhahania, vitu visivyohesabika, zenye dhima ya udogo na mahali zinapoainishwa kimofolojia na kisemantiki. Zaidi ya hayo imebainika kuwa viambishi ngeli vya nomino za Kikinga vinaweza kubeba dhima ya kuonesha umoja, wingi, uzuri, ubaya, udogo na ukubwa.